22 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

NINI KITATOKEA RAILA ODINGA AKIGUSA MBONI YA UHURU KENYA


Na Hafidh Kido | 

UKISOMA kitabu cha Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo ‘Jecha’ kilichoandikwa na mwanamama Minael-Hosanna O Mdundo (1999), kinaeleza kwa ufasaha namna Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalivyofanyika kimzahamzaha.

Sheikh Thabit Kombo anaeleza kuwa, mipango ya mapinduzi ilifanyika chini chini kwa kushirikisha watu mbalimbali.

Usiku huo wa kuamkia mapinduzi watu wa ng’ambo (nje ya mji) waliingia mjini kwa lengo la kuhudhuria ngoma.

Ngoma hiyo maalumu iliandaliwa kwa ajili ya kuwapumbaza watawala, wakati vurugu na kelele za wacheza ngoma zikiendelea mapinduzi yakaanza kutekelezwa kwa kuiba silaha kwenye maghala ya askari.

Kwa kiufupi hivyo ndivyo Mapinduzi ya Zanzibar yalivyofanyika, mengine yanahitaji takwimu. Wakubwa waliyapanga yakapangika, watu walitumika kupiga kelele za shangwe usiku waonekane wanasherehekea ngoma.

Tukio hilo halina tofauti na kinachotaka kutokea Kenya. Kiongozi wa upinzani kupitia umoja wa Nasa, Raila Odinga, amelazimisha kuapishwa kuwa ‘Rais’ wa Kenya. Kimsingi ingawa siijui Katiba ya Kenya, lakini hili ni kosa la uhaini. Ni sawa na mapinduzi.

Kosa la uhaini katika mataifa mengi ni kunyongwa hadi kufa, ila katika baadhi ya nchi zinazoongozwa na demokrasia adhabu ya uhaini ni kifungo. Baadhi wanatoa kifungo cha maisha, wengine kifungo kirefu kinachozidi miaka 10.

Anachokitafuta Raila kwa Rais Uhuru Kenyatta, bila shaka atakipata.

Katika miaka ya hivi karibuni Taifa la Kenya limeingia dosari baada ya mauaji yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Vurugu zilitokea baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mwai Kibaki, kulazimisha ushindi dhidi ya Uhuru Kenyatta, tukio hilo  lilisababisha Uhuru na wenzake kadhaa kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague, nchini Uholanzi.

Siwezi kuweka takwimu za waliouawa, itoshe tu kusema maisha ya wananchi wasio na hatia yalipotea, waliojeruhiwa, waliochomewa nyumba, magari, mashamba na maduka hawana idadi. Hasara iliyopatikana kwa nchi ni kubwa, hata leo ukitaka kumtoa machozi Mkenya aliyeshuhudia kadhia ile basi mkumbushe au mtajie sentesi hii ya kimombo: ‘Post election violence.’

Ni tukio baya na la aibu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki baada ya mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda, yaliyopoteza roho zaidi ya milioni moja kwa miezi kadhaa tu. Hatutaki haya yajirudie kwa namna yoyote ile na ndiyo maana katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Kenya hivi karibuni, kaulimbiu kubwa ilikuwa ni kukaa mbali na kilichotokea mwaka 2007.

Agosti 8, mwaka jana, Kenya iliingia katika Uchaguzi Mkuu wa kihistoria. Uhuru Kenyatta alimwaga sera nyingi za kumalizia ahadi alizoweka katika awamu ya kwanza ya uongozi wake wa miaka minne, huku Raila Odinga akimwaga sera za kuleta mabadiliko nchini humo.

Matokeo yalipotoka, ilionekana Uhuru kupitia Chama cha Jubilee aliongoza kwa kura 8,203,290, sawa na asilimia 54.27, huku mpinzani wake mkuu, mgombea wa Muungano wa Upinzani wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga akipata kura 6,762,224, sawa na asilimia 44.74.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka- IEBC, Wafula Chebukati, alisema ni asilimia 78 ya wapiga kura milioni 19 waliosajiliwa pekee walioshiriki katika shughuli hiyo ya kidemokrasia.

Furaha ya wafuasi wa Jubilee kwa ushindi wa Uhuru Kenyatta haikudumu, kwani Raila alipinga matokeo mahakamani, wengi walitarajia Uhuru angeachana na hilo, kisha aamue kuapishwa kuchukua nchi kama wanavyofanya viongozi wengi wa nchi za Afrika.

Mambo yalikuwa tofauti, Uhuru Kenyatta alikuwa muungwana na kusema hiyo ni haki ya kila Mkenya kutaka haki mahakamani kama inavyotamka Katiba yao. Mchuano ulikuwa mkali mahakamani, hatimaye Jaji wa Mahakama ya Juu ya Kenya, David Maraga, alifuta matokeo na kuamuru uchaguzi urudiwe ndani ya siku 60.

Kinyume na matarajio ya wengi, Rais Uhuru Kenyatta alikunja mikono akasema ‘Hewallah Bwana’, akakubali uchaguzi urudiwe. Katika hali ya kushangaza, Raila huyo huyo ambaye alipeleka kesi mahakamani ili uchaguzi ufutwe akaamua kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26, 2017, siku ya kuzaliwa Rais Kenyatta.

Uchaguzi ulifanyika na matokeo yalipotangazwa Uhuru alishinda kwa asilimia 98, kama alivyoahidi Raila Odinga, hakushiriki uchaguzi, lakini kulikuwapo na viashiria vya hila za kutaka kuuvuruga uchaguzi baada ya kuonekana baadhi ya wananchi wakichana karatasi za kupigia kura, kuvunja masanduku ya kuhesabia kura pamoja na kuweka vizuizi kwenye milango ya kuingilia kwenye vituo vya kupiga kura.

Hali ilipoanza kutulia, Jaji Maraga akatangaza tarehe ya kumwapisha Uhuru Kenyatta, ghafla Raila Odinga akaibuka na kuanza kupiga kelele akisema hatambui ushindi wa Uhuru Kenyatta, bila kukumbuka kuwa, alipewa nafasi ya kurudia uchaguzi, lakini akaikataa kwa madai kuwa Tume ya Uchaguzi nchini humo haikuwa ya kihalali.

Baada ya kuona kelele zake hazisikilizwi, akaamua kugeukia mpango wa pili wa kutaka naye aapishwe kuwa rais wa Kenya, jambo ambalo halikuwezekana, kwani nchi moja haiwezi kuwa na marais wawili. Pengine Raila angeomba tu kuwepo na serikali ya mseto ambako nchini humo wanaiita serikali ya nusu mkate.

Suala la serikali ya mseto si geni nchini Kenya, kwani baada ya vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 iliamuliwa kuundwa kwa serikali ya mseto na safu ya uongozi ilikuwa hivi: Rais Mwai Kibaki, Waziri Mkuu, Raila Odinga na Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta.

Nadhani Raila bado anakumbuka ulinzi, viyoyozi na saluti alizokuwa akipewa kipindi akiwa Waziri Mkuu wa Kenya. Hilo linamtia wazimu kwa sababu kulingana na umri wake wa miaka 73, anaona hawezi kuendelea kusubiri hadi mwaka 2021 kugombea tena, wakati huo atakuwa na miaka 77. Hivyo anataka liwezekanalo leo lisingoje kesho. Raila Odinga amezicheza vibaya karata zake.

Majaribio mawili ya kutaka kuapishwa yamewahi kusitishwa na vikosi vya kutuliza ghasia nchini humo, yeye akisindikizwa nyumbani kwake bila kufanywa chochote na dola. Anachokifanya Raila Odinga ni kujaribu kuigusa mboni ya jicho la Rais Kenyatta, bila shaka akiendelea hivyo, Rais Kenyatta atashindwa kumvumilia na mambo yanaweza  kuwa mabaya si kwa Raila tu, bali kwa Taifa la Kenya.

Rais Kenyatta na Raila Odinga wana historia ya kifamilia, wazee wao, yaani Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga, ndio wazazi wao Raila na Uhuru, walikuwa marafiki wakubwa kabla ya Uhuru wa Kenya kupatikana mwaka 1963. Baada ya uhuru, Mzee Kenyatta akiwa Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jaramogi alikuwa Makamu wa Rais Kenya, wote wakiwa wanachama wa KANU. Siasa ziliwafarakanisha wakawa maadui wakubwa hata kufikia Mzee Jaramogi kuunda chama cha upinzani Kenya People’s Union (KPU) mwaka 1966.

Hata ukiangalia historia ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ni watu waliokuwa pamoja katika harakati za kisiasa ndani ya chama cha KANU, baadaye walipoanza kuingiwa na tamaa ya madaraka ndipo walipokuwa maadui hadi sasa. Hivyo historia inataka kujirudia kwa njia nyingine.

Hata hivyo, huenda maneno ya baba yake ndiyo yanayomrudisha nyuma Rais Uhuru, alipata kutamka jukwaani kuwa anamstahi Jaramongi Oginga Odinga kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kutokana na maneno ya hovyo anayoyatoa hadharani dhini yake, angeweza kumweka ndani na hakuna wa kumtoa.

Pamoja na mambo hayo yote, hili analolitengeneza Raila Odinga ni la hatari zaidi, hivyo Waafrika wazidishe sala  kumwombea Rais Uhuru Kenyatta asipungukiwe uvumilivu.

Afrika ni yetu, jambo lolote linalotokea katika ukanda wa Afrika linawatia doa Waafrika wote!

Mungu ibariki Afrika, wabariki viongozi wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles