30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI TULIKUWA NA KINGUNGE?


Na KABWE ZITTO|

NILIKUTANA na Mzee Kingunge mwaka 2005, bungeni nikiwa mbunge wa kuchaguliwa kutoka Kigoma Kaskazini na yeye akiwa mbunge wa kuteuliwa.

Tulipoanza Bunge la 9 Mzee wetu huyu ambaye sasa ametangulia mbele ya haki alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano ya Jamii na Siasa. Baadaye alipumzishwa na kuendelea kuwa mbunge wa kawaida.

Sikuwa na ukaribu naye, japokuwa tulikuwa tunaukaribu kifikra, kwa maana ya itikadi ya Ujamaa. Sikuwa nakunywa naye kahawa kama ilivyokuwa kwa Mzee Prof. Philemon Sarungi au Marehemu Jackson Makweta. Lakini tulikuwa tunasalimiana kwa bashasha na akipenda ukorofi wangu bungeni.  Baadaye nilijifunza kuwa naye alikuwa mkorofi sana enzi za ujana wake.

Siku moja mwaka 2009 kulikuwa na mzozo bungeni kuhusu mjadala wa mahakama ya kadhi. Wabunge Waislam wakiongozwa na mbunge wa zamani wa Singida Kusini, Mohamed Misanga (marehemu), na wabunge Wakristo wakiongozwa na Godfrey Zambi wakiipinga. Lugha zilizokuwa zikitumika zilikuwa za mgawanyiko mno na Bunge lilikuwa mubashara kwenye luninga. Nikaogopa sana namna viongozi wanaongea lugha za kugawa wananchi kidini. Nikasimama kuongea. Nikafoka sana kuhusu lugha tunazotumia kujenga hoja bila kujali madhara yake kwa raia wetu. Pia nikawalaumu wabunge wakongwe kwa kukaa kimya bila kukemea. Mjadala ukabadilika na kuwa wa staha.

Tulipotoka nje ya Bunge nikakutana na Ezekiel Kamwaga, mwandishi wa habari ambaye enzi hizo hakuwa mwandamizi. Ezekiel akaniambia “Nimemhoji Mzee Kingunge kuhusu lawama zako kwao. Ameniambia wewe umechelewa sana kuzaliwa. Ulipaswa kuzaliwa wakati Mwalimu Nyerere. Una maoni?”. Nikamjibu Kamwaga kuwa wazee waliniudhi kukaa kwao kimya. Hata hivyo nimefarijika sana kuwa Mzee Kingunge alikuwa ananisikiliza. Tangu siku hiyo kila nilipokutana na Mzee Kingunge nilikuwa nataniana naye kuhusu ‘intervention’ ile bungeni.

Nimekuwa na kawaida ya kuandika tanzia kila mtu wa karibu yangu ama mtu ninayemheshimu anapofariki. Wakati mwingine huwa napata tabu sana kuandika kutokana na ukaribu ama uzito wa mtu mwenyewe. Tangu asubuhi jana(juzi) nilipoletewa ujumbe wa simu kuwa Mzee Kingunge hatunaye nimekuwa natafakari kuwa naandika nini kuhusu jabari hili la siasa za nchi yetu? Naandika nini kuhusu kizazi cha dhahabu cha wanasiasa wazalendo wa nchi yetu? Naandika nini kuhusu ‘ideologue’ wetu huyu ambaye hajaweza kuzibwa nafasi yake na yeyote?

Ni kama vile mtu anayetaka kuandika kuhusu maisha ya Komredi Marcelino Dos Santos wa FRELIMO. Ni kazi ngumu zaidi kwa sisi ambao hatukuwa na ukaribu mkubwa sana na Mzee huyu. Hata hivyo, nimeona lazima nimuage Komredi Kingunge kwa namna ninayoweza, nayo ni kueleza kizazi cha sasa ni nani Kingunge Ngombale – Mwiru, na ni kwanini nchi yetu ilikuwa na raia huyu?

Maisha ya Komredi Kingunge ni taswira ya historia ya Chama kilichotukomboa kutoka makucha ya ukoloni mkongwe, TANU na Nchi ya Tanganyika. Mwaka 1957 ilikuwa dhahiri kwa chama cha TANU kuwa punde tu, miaka michache mbele, Uhuru wa Tanganyika ungepatikana, hamasa ya wananchi ilikuwa juu mno, na uungwaji mkono wa TANU ulikuwa mkubwa nchi nzima. Katika wakati husika viongozi wenye maono wa TANU wakaamua kuliandaa Taifa na kukiandaa Chama chao kuendesha nchi.

Changamoto kubwa katika wakati husika ilikuwa ni rasilimali watu, wasomi wachache wa Kiafrika ambao pia walikuwa viongozi wa TANU hawakutosha kushika nafasi zote muhimu za kuliongoza Taifa. Hivyo haja ya kusomesha wasomi wa Tanganyika kwaajili ya kusaidia kuliongoza Taifa mara baada ya Uhuru ikaibuka. Rais wa 19 wa Liberia, William Vacanarat Shadrach Tubman na chama chake cha True Whig Party (TWP) wakawa kimbilio la TANU, Rais wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere, akiomba nafasi za masomo ya elimu ya juu (skolashipu) kwaajili ya vijana wa Tanganyika.

Komredi Kingunge alikuwa mtu wa 5 kupata Skolashipu hizo, mwaka 1958. Awali, mwaka 1957, mzee Muharram Macatta Mwinyimtwana na Balozi Paul Malyago Rupia walikuwa ndio kundi la kwanza la wanafunzi kupata Skolashipu za kwenda kusoma elimu ya juu kupitia Chama cha Ukombozi cha TANU, katika Chuo Kikuu cha Cuttington, Suacoco, Maili 120 Kaskazini ya Mji Mkuu wa Liberia, Monrovia. Muharram na Paul walikuwa watoto wa wafadhili wa chama cha TANU, mzee Macatta Mwinyimtwana wa Ngamiani Tanga, na Mzee Paul Rupia wa Misheni Ilala, Dar es Salaam.

Kundi la pili lilihusisha wanafunzi watatu, ambao pia walikuwa ni wafanyakazi wa kujitolea katika makao makuu ya TANU, hao ni Komredi Kingunge, Mzee Ghysla Mapunda, aliyekuwa waziri wakati wa Mwalimu Nyerere, pamoja Shaaban Nyelwa Kissenge, ambao wao walikwenda masomoni mwaka 1958.

Kundi la tatu lilikuwa kubwa zaidi, likihusisha idadi ya watu zaidi ya kumi, lilikwenda masomoni mwaka 1959. Kundi hili likiwahusisha Amani Samuel Mshote, Dk. John Kasiga, Martin Kayuza, Chifu Nhindilo Humbi Ziota, Dk. Kassim Guluri, Charles Buzuka, Dk. William Kimweri Madundo, Dk. Mbaga, Joshua Mpogolo, Mjabuzi, pamoja na Edmund Luganga. Hivyo kufanya jumla ya watu wote waliopelekwa masomoni na TANU kufikia 16, katika kipindi kifupi cha kati ya mwaka 1957 – 1961. Wote hawa kwa nyakati tofauti walishika dhamana mbalimbali ndani ya nchi yetu.

Jambo hili la TANU kuandaa vijana wa kuendesha nchi ni historia muhimu ya Taifa letu, inajenga msingi wa namna vyama vya siasa vya wakati wa ukombozi vilivyojikita katika ujenzi wa Nchi. Kwa Zanzibar, chama cha Umma Party nacho kilifanya jambo hili la kuwaandaa vijana, kwa kuwatafutia mafunzo kutoka sehemu mbalimbali, duniani, kuanzia Cuba, Ujerumani, USSR mpaka Misri. Hivyo vijana wa kizazi cha awali cha Tanzania, kina Komredi Kingunge na Dk. Salim Ahmed Salim, walipikwa na kuandaliwa vyema kuja kuliongoza Taifa na vyama vyao, jambo ambalo vyama vya siasa vya sasa havifanyi kabisa.

Taswira kuu ya mzee Kingunge ni kuwa alikuwa ni Tanuri la kupika fikra zilizozaa sera na maamuzi ya nchi yetu. Ramani ya maendeleo ya nchi yetu Tanzania, kwa miongo 3 ya mwanzoni ilichorwa kwa kutumia nyaraka 3; Azimio la Arusha, Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971 na Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981. Nimechungulia nyaraka zangu ili kusoma muhtasari wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU wa Januari, 1967 uliopitisha Azimio, sikuona jina la Komredi Kingunge. Mkutano huo ndio uliiweka nchi yetu kwenye ramani ya nchi za kijamaa. Mzee Kingunge hakuwamo kwenye ule mkutano wa Arusha. Hata hivyo huwezi kuzungumzia utekelezaji wa Azimio hilo bila kutaja miongozo niliyotaja hapo juu ambayo aliindika yeye. Kwa hiyo miaka minne baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha unaanza kumwona gwiji la itikadi “The Ideologue” Kingunge Ngombale – Mwiru.

Hivi karibuni niliona taarifa kutoka Davos, Uswizi, ambapo mkutano wa mabepari wa dunia hufanyika. Taarifa ile ilisema Tanzania ndiyo nchi inayoongoza Afrika kwa kuwa na Uchumi jumuifu (inclusive economy). Kwa watu wa fikra fupi walikimbilia kusambaza habari hizi bila kuzipa muktadha wake stahili. Muktadha wake ni Azimio la Arusha la 1967. Hili ndio lilikataa unyonyaji na kujenga uchumi usio na matabaka (inequality).

Katika kitabu kilichopewa jina la ‘Miongozo Miwili: Kupaa na kutunguliwa kwa Azimio la Arusha’, kilichochapishwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kingunge anaeleza kwa ufasaha namna Mwongozo wa 1971 ulivyobuniwa na kutekelezwa.

Nanukuu “Mwongozo wa TANU wa 1971 ulitolewa na kutangazwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU ya dharura mwanzoni mwa Februari, 1971  Dar es Salaam. Januari mwaka 1971 Jeshi la Uganda chini ya Iddi Amin Dada, liliangusha serikali ya Rais Milton Obote na kutwaa madaraka. Kufika Agosti kitendo cha uchokozi kisicho cha kawaida kilitokea, kikosi cha Jeshi la Iddi Amin kilikivamia kikosi cha doria cha polisi wa Tanzania mpakani Mutukula na kumteka nyara Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na kumtoroshea Uganda”. [ Kamanda huyu aliyeuawa hatimaye aliitwa Hans Pope, baba mzazi wa huyu Hans Pope wa Simba Sports Club inayoifunga funga Yanga kila wakikutana].

“Kitendo hiki cha uhasama kutoka kwa nchi jirani kilihitaji kupatiwa jibu la haraka na la kimkakati. Ndipo nilipoitwa ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa, ambaye nilimkuta na Meja Hashim Iddi Mbita (wakati ule Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU). Kawawa alinieleza kwa kifupi kuwa Mwalimu alimwagiza aniarifu kuwa ameamua mimi niongoze timu ya viongozi wa vijana kadhaa wa TYL (TANU Youth League) kwenda Mkoa wa Ziwa Magharibi kufanya kazi ya kuhamasisha wananchi kisiasa na kiulinzi na usalama ili waweze kukabiliana ipasavyo na chokochoko zozote zile kutoka nchi jirani.

Pamoja na kukubali jukumu nililopewa na kuahidi kuanza maandalizi mara moja, nilitoa rai kwa Makamu wa Pili wa Rais kwamba kwa kuwa tishio kwa usalama wa nchi kutoka Uganda ni sehemu tu ya tishio kwa taifa, maana kuna tishio kubwa zaidi kwenye Ukanda wa Kusini, la majeshi ya Wareno, na uhasama wa Wareno, pamoja na wa dola za Afrika ya Kusini na Rhodesia (sasa Zimbabwe), ingekuwa busara kuitisha kikao cha NEC kutafakari juu ya ulinzi na usalama wa Taifa. Kawawa alikubaliana na pendekezo langu na palepale aliondoka akifuatana na ndugu Hashim Mbita, kwenda kuonana na Mwalimu Ikulu. Walirejea baada ya nusu saa na kunitaarifu kuwa Mwalimu amekubali pendekezo nililolitoa na tayari ameagiza NEC iitishwe kwa dharura.” Mwisho wa kunukuu.

Komredi Kingunge si tu alipokea kazi na kuitekeleza kwa utii, bali pia alishauri kuipanua na kuipa baraka ya vikao vya Chama. Hebu fikiria, unaitwa na Kawawa unapewa kazi aliyoagizwa na Nyerere halafu wewe mpewa kazi unashauri kwanza nini kifanyike. Si tu ni ujasiri bali ni kujiamini kulikopita kiasi cha kawaida. Hebu fikiria leo unaitwa na Rais kupewa kazi halafu unajifanya kujua, eti itisha Halmashauri Kuu kwanza, thubutu! Kingunge ni darasa tosha la wanasiasa wa sasa.

Kwa taarifa tu kwa vijana ni kwamba moja ya zao lililodumu la mwongozo wa mwaka 1971 ni jeshi la mgambo. Ilipotokea vita dhidi ya Nduli Idi Amini, wanamgambo walioandaliwa kutokana na mwongozo wa mwaka 1971 walipigana bega kwa bega na wanajeshi wengine na kumshinda adui. Ukiona mwanamgambo popote ni alama ya fikra za Mzee Kingunge atakayezikwa Februari 5, mwaka huu siku ambayo kilizaliwa Chama ambacho yeye ni miongoni mwa waasisi wake. Kwa hakika nchi yetu inaweza kumuenzi Mzee wetu huyu kwa kuanzisha Kingunge Brigade ndani ya jeshi la mgambo ili vizazi na vizazi wajue wazo hili lilitoka kwa nani.

 Pia mwongozo wa mwaka 1971 ulisisitiza sana suala la maendeleo ya watu. Jambo ambalo ni mwafaka wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ule katika nchi yetu. Mwongozo ulisema “Kwa hiyo katika kufikiria maendeleo ya Taifa letu na katika kupanga mipango ya maendeleo wakati wote mkazo mkubwa uwekwe kwenye maendeleo ya watu na si ya vitu… (watu) wenyewe lazima washiriki katika kufikiria, kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo yao”.

Hii ni kauli inayoishi na kudumu milele. hupimi maendeleo ya Taifa kwa madaraja, ndege, wala njia za reli, bali kwa namna ambavyo watu wa Taifa hilo wameelimika na kuwa na afya tele inayowapa uwezo wa kuzalisha mali na kuongeza utajiri wa nchi.

Dhana hii ya ‘Maendeleo ya Watu’ Mzee Kingunge aliiamini mpaka mwisho wa uhai wake. Nakumbuka wakati wa mijadala ya Bunge Maalumu la Katiba aliamsha mjadala mzito juu ya jambo hilo, na aliandika eneo maalumu la uchumi ili kutoa ‘Dira ya namna uchumi wa Taifa letu unapaswa kuwa’. Eneo hili limewekwa kama sehemu ya tatu ya Katiba Pendekezwa, likijikita katika kuelezea namna dola inavyopaswa kuwa wakala wa ukombozi wa wananchi.

Miaka 10 baadaye mwongozo wa mwaka 1981 ulitangazwa, ambao pia ni zao la fikra za Komredi Kingunge. Katika kitabu cha Miongozo Miwili hilo pia limeelezwa vizuri na Kingunge mwenyewe. Nanukuu “Mwongozo wa 1981, kama ulivyokuwa mwongozo wa TANU wa 1971, ulikuwa ni mwendelezo wa fikra na matarajio ya Ujamaa na Kujitegemea uliotangazwa na Azimio la Arusha. Mwongozo huu ni matokeo ya mila iliyokuwa imejengwa ndani ya Chama ya kutumia vikao vikuu vyake, hususan NEC, kujadili na kuchambua masuala mazito ya nchi, ya siasa, uchumi na jamii, na kuyatolea maelekezo ya kisera, kiufafanuzi na kiutekelezaji.

Wakati Mwongozo wa TANU wa 1971 ulijielekeza kwenye mapambano dhidi ya Ukoloni, Ukoloni-Mamboleo na Ubeberu ili kufanikisha Ukombozi wa Afrika na wa Mwafrika na kuweka mkakati wa ulinzi na usalama wa umma ili nchi iwe na uwezo wa kukabiliana na uvamizi wowote kutoka kwa ubeberu au na vibaraka vyake, Mwongozo wa 1981 umejikita katika kufanya uchambuzi kosoa wa kina na mpana juu ya hali ya kisiasa na kiuchumi iliyokuwepo nchini, hali ya maendeleo ya demokrasia nchini na ndani ya chama, n.k., na kutoa mapendekezo ya kuimarisha na kupanua demokrasia katika Chama na nchi”. Mwisho wa kunukuu.

Jambo kubwa tunalojifunza hapa ni Chama cha siasa kuwa chombo cha mijadala na maamuzi ya watu badala ya kuwa chombo cha kupitisha amri za wakubwa. Kwamba Chama kinaweza kufanya uchambuzi kosoa ili kujikosoa. Na kwamba vikao vikuu vya chama vinapaswa kuwa na ajenda ya kudumu ya kujadili hali ya uchumi na siasa ya nchi. Sisi ACT Wazalendo tuliiga jambo hili, ndio maana katika kila kikao kikuu cha chama chetu, ni lazima tujadili hali ya nchi (kiuchumi na kisiasa) na kutoa taarifa ya mwongozo wa kisera kwa chama.

Jambo hilo ni muhimu sana, hasa katika zama za sasa ambapo hata kukosoa ni dhambi, na vikao vya vyama hukaa kwa dakika masaa machache sana kupokea amri tu za wakuu wa vyama hivyo. Kwa vyovyote vile vyama vya namna hiyo vinahesabu siku zake. Ni vema kutumia siku za kuomboleza kifo cha Komredi Kingunge kujitafakari kama tunafuata misingi ya mwongozo wa mwaka 1981 kuhusu uchambuzi kosoa ili kujenga msingi madhubuti wa ujenzi wa vyama vyetu vya siasa, pamoja na kupanua demokrasia nchini.

Mzee Kingunge ametuachia usia kwenye andiko lake nililonukuu sana kwenye makala haya. Mwenyewe ameziita changamoto na ninaomba niziweke kama alivyoziweka yeye;

– Unapoisoma miongozo hii miwili, wa TANU wa 1971 na wa 1981, huwezi kukosa kubaini kuwa fikra, nadharia na tafakuri kubwa zilitumika katika utunzi wake. Haya ni matokeo ya viongozi wa chama wanapokaa pamoja na kufikiri pamoja. Hii ni aina mojawapo ya uhai wa chama iliyo muhimu sana kwa uhai wa jumla wa chama cha siasa.

– Je, mila hii iliyokuwa imejengeka huko nyuma CCM ya sasa inaiendeleza? Je vyama vingine vya siasa nchini vinajaribu kujenga tabia ya viongozi wake kuketi pamoja na kufikiri pamoja na kuchambua pamoja hali ya nchi yetu na namna vitakavyozikabili changamoto mbalimbali?

– Huu umasikini wetu wa sasa wa falsafa unaotuathiri vibaya unatokana na nini?

Mzee Kingunge alikuwa mtu mwenye kusimamia anayoyaamini, amefariki dunia akiwa ameondoka katika Chama chake alichoshiriki kukiasisi. Tunaambiwa kuwa hakujiunga na Chama kingine cha siasa, ingawa alitoa msaada kwa Chama kilichokuwa kinapingana na Chama chake. Hili laweza kubakia kuwa jambo la mjadala mkali katika miaka inayokuja. Inawezekana mjadala huo ukafunika kabisa mchango wake kwenye ujenzi wa Taifa letu. Hatuwezi kukwepa hilo kuwa mjadala lakini tunaweza kukwepa kulikuza na kulifanya lifunike mambo makubwa aliyoyafanya kwa nchi yetu.

Sina hakika kama Komredi Kingunge aliandika kitabu kuhusu maisha yake. Hii ni changamoto kubwa kwa viongozi wetu wengi. Hawapendi kuandika hivyo kuondoka duniani na maarifa yao bila kuyarithisha kwa vizazi vya mbele yao. Kuna mambo mengi ambayo vizazi vingependa kujifunza kutoka kwa watu kama Kingunge Ngombale Mwiru lakini kwa sababu hatuandiki, basi vizazi vinaikosa hiyo fursa.

Kwa mfano, miaka ya 1970 Komredi Kingunge alikuwa ni Mkuu wa Mkoa, Katibu wa TANU wa Mkoa, na hivyo kuwa pia Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aligombana na Mzee Kawawa kuhusu kwenda kinyume na msimamo wa Serikali bungeni ilhali yeye ni mkuu wa mkoa wa Serikali hiyo hiyo, kwa jambo la Serikali ambalo yeye hakukubaliana nalo. Mwalimu Nyerere alimfukuza kazi Kingunge.

Habari hii haijaweza kuelezwa kwa namna ambayo itakaa kwenye vichwa vya vijana kama funzo la kuwa na msimamo. Mzee Kingunge hakujali cheo chake, alisimamia kile alichokiamini bila kujali cheo chake. Alifukuzwa kazi baadaye alirudi, na kuwa mjumbe wa kamati iliyoandika Katiba ya kuunganisha vyama vya ASP na TANU. Aliheshimiwa kwa msimamo wake. Jambo hili hulioni kwa wanasiasa wa sasa. Limefanywa kuwa gumu zaidi pia kutokana na uongozi wa sasa pia ambao ni wa kiimla na hauruhusu mawazo pinga.

Tabia ya kuwa msimamo Kingunge ameiishi maisha yake yote, tangu chuo kikuu kule Liberia. Katika kundi la wanafunzi wale 16, ni kuwa ni kundi la kwanza tu, wazee wetu Muharram Mwinyimtwana tu na Paul Rupia, ndio waliomaliza masomo yao mwaka 1960, wanafunzi 13 waliobaki chini ya Uongozi wa Komredi Kingunge walifukuzwa chuo wakitetea uonevu dhidi ya wanafunzi wenzao, jambo lililozusha vurugu kubwa Chuo Kikuu cha Cuttington, na hivyo wanafunzi hao kuhamishiwa Dakar, Senegal, kisha kuendelea na masomo katika nchi za USSR.

 

Ningefurahi kusoma visa vyote hivi kutoka kwenye kitabu cha Komredi Kingunge mwenyewe. Natarajia kuwa ameacha mahala hazina ya maandiko ya historia hii muhimu kwa Taifa, na kuwa watafiti na wanazuoni wataweza kuiweka hazina hiyo kwenye kitabu. Kwa hakika nchi yetu imepoteza jabali la siasa. Profesa Issa Shivji amejitahidi kumweka wazi Mzee Kingunge kwenye maongezi yao yaliyochapishwa kwenye jarida la Nyerere Chair miaka tisa iliyopita. Maongezi haya  yanatosha kuanzia kuandika kitabu cha Kingunge. Nawasihi watu wote msome maongezi yale. Yamesheheni historia ya nchi yetu ndani ya historia ya Mzee Ngombale.

Buriani Mzee Kingunge Ngombale – Mwiru. Ulisomeshwa na TANU nawe ukalisomesha Taifa. Uliandaliwa kuongoza Taifa letu, umetuongoza vema.

Pumzika kwa Amani Komredi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles