NINI KINAFUATA KWA THERESA MAY?

0
510
Theresa May

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Uingereza, Teresa May, alishuka chati. 

Teresa May alifanikiwa kuwa maarufu kwa kipindi cha mwaka mmoja tu baada ya kuukwaa uwaziri Mkuu wa Uingereza na uongozi wa chama cha Conservative, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa na vyeo hivyo kabla yake, David Cameron.

Kilichomuondoa Cameron wakati huo, kilikuwa ni kushindwa kwake katika kampeni ya kuitaka Uigereza ibaki kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU).  Cameron aliamua kuitisha kura ya maoni ili wananchi wachague wenyewe ama kuendelea kuwa wanachama wa EU, au kujiondoa.  Alipigia sana debe Uingereza kuendelea kuwa EU, lakini matokeo ya kura yalipotoka, kampeni yake ilishindwa.

Kutokana na hilo, Cameron alitangaza kujiuzulu na Teresa May aligombea uongozi wa chama cha Conservative na kushinda na hivyo kupata ridhaa ya kuwa Waziri Mkuu wa pili mwanamke nchini humo.

Alianza vizuri  na kutokana na hali ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea nchini mwake, licha ya ratiba ya uchaguzi kuwa bado, Mama May aliamua kuuitisha ili aweze kupata viti vingi zaidi vya ubunge kwa ajili ya chama chake na hivyo kuwa na nguvu katika uamuzi wa majadiliano ya nchi yake kujitoa katika Jumuiya ya Ulaya.

May alikuwa na uhakika wa kuwamaliza wapinzani na kuzoa viti vingi. Kutokana na uhakika huo, hakujisumbua sana na kampeni na hata mdahalo wa wagombea ulipoandaliwa, aliamua kutuma mwakilishi badala ya yeye mwenyewe kuhudhuria.

Hata hivyo, tofauti na matarajio yake, tunaweza kusema kwamba Teresa May ameshindwa katika uchaguzi huo.

Ni kweli kwamba bado chama chake cha Conservative kina viti vingi zaidi vya ubunge na ni kweli kwamba ana uhalali wa kuendelea kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.  Hata hivyo, ni kweli pia kwamba azma yake ya kutaka kujizolea viti zaidi imemtokea puani, kwani badala ya kupata zaidi ya vile alivyokuwa navyo, amepoteza.

Hivi sasa Waziri Mkuu huyu anatakiwa kuingia makubaliano na chama kidogo kilichopo Ireland ya Kaskazini, Democratic Unionist, ili aweze kupata wafuasi wengi zaidi kwenye Bunge la Uingereza.

Kipigo hiki kimekuwa kibaya zaidi kwani yapo majimbo ambayo yalishikiliwa na Conservative kwa miongo mingi, lakini sasa yameenda katika mikono ya Labour.  Ikumbukwe pia kwamba Mama May aliitisha uchaguzi huu makusudi kabisa kwa lengo la kupata nguvu katika majadiliano kuhuku Uingereza kujiondoa EU, maarufu kama Brexit…na hivyo hajapata nguvu hiyo na badala yake, ile ndogo aliyokuwa nayo imeendelea kupungua.

Na kutokana na hilo, kuna uwezekano mkubwa kwa Uingereza kuwa na uchaguzi mwingine wa haraka haraka na hili linaweza likatokea hata ndani ya mwaka mmoja tu.  Hatuelewi kama wananchi watakuwa tayari kutumia muda wao kwenye uchaguzi mwingine. Ikikumbukwa kwamba mwaka 2015 walikuwa na uchaguzi mkuu, mwaka 2016 wakawa na kura ya maoni ya kujitoa ama kutojitoa EU, mwaka 2017 wakawa na uchaguzi mwingine…kwa mtu wa kawaida, inachosha!

Ndio maana tunasema kwamba Mama May ameshindwa katika uchaguzi huu aliouitisha haraka haraka na amejikuta akilazimika kuomba msamaha kwa wale wanachama wenzake waliopoteza viti vyao kutokana na uamuzi wake huo.

Wanachama wenzake wamekasirishwa, wasaidizi wake wamejiuzulu, wapinzani wake wanadai Uingereza kwa sasa haina  uongozi makini  na wengi wanamshutumu kwa kuendelea na nafasi yake ya Uwaziri Mkuu, badala ya kujiuzulu na kumpisha mtu mwingine kuiongoza Uingereza.

Hayo ndiyo yanayoendelea Uingereza.  Wakati wengine wanamshutumu vikali Mama May kwa kutoamua kuwajibika mapema na kujiuzulu wadhifa wake, wengine tunawaza, nini kitafuata?  Aliitisha uchaguzi pasipokuwa na ulazima, amesababisha wabunge wa chama chake  kupoteza viti vyao, na amedhoofisha zaidi nguvu ya Uingereza katika kuijadili Brexit.  Hatima yake itakuwa nini?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here