31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MGHWIRA JENGA NYUMBA ACHANA NA WAGOMBEA FITO

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Elisha Mghwira

Na Victor Makinda,

WAHENGA Walikuwa na misemo mingi yenye hekima na weledi. Moja ya semi za hekima za wahenga ni huu. “Tunajenga nyumba moja, kwa nini tugombee fito?

Ndiyo, Tanzania ni yetu sote. Ukiwauliza Watanzania  nini mahitaji yao na kiu yao kubwa, wote watakujibu kwa sauti kuu “ Tunataka Maendeleo’. Naam, Watanzania wanataka maji safi, barabara nzuri zinazopitika misimu yote ya mwaka. Watanzania wanataka huduma za afya zilizoboreshwa kwa kupatikana dawa na watoa tiba katika zahanati na hospitali zao. Wanataka elimu bora na si bora elimu. Wanataka urahisi wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mipango madhubuti ya kuiinua sekta hii mama. Watanzania wanataka viwanda vya kusindika mazao yao ya kilimo ili kuyaongeza thamani sambamba na masoko ya uhakika.

Sijui kama kuna Mtanzania anayeitaka ACT, CCM, Chadema au CUF.  Watanzania wanaitaka Tanzania yenye Watanzania wenye ustawi wa maendeleo. Vyama vya siasa vinapigania kuishika dola kwa mintaarafu ya kuwaletea maendeleo wananchi na si vinginevyo.

Kumbe vyama hivi navyo lengo lake kubwa ni maendeleo tu basi. Vinapambana usiku na mchana kushika dola ili viwaletee maendeleo Watanzania. Hawapiganii kushika dola ili kuishia kushika dola basi, vinapigania  kushika dola kwa lengo madhubuti la kuwaletea maendelea Watanzania.

Ikiwa ni hivyo na ikiwa hilo ndilo lengo la chama chochote cha siasa, kwa nini tunapiga kelele pale iwe ni mwanachama au kiongozi wa chama cha upinzani anapoteuliwa kuuungana na Serikali iliyopo madarakani kuwaletea maendeleo Watanzania?

Ukweli ni kwamba chama kama hakijashika dola hakiwezi kuunda Serikali. Chama kinachounda Serikali kina uwezo wa kuangalia nani kutoka chama pinzani anao uwezo wa kuungana na Serikali ya chama tawala kufanya kazi ya kuleta maendeleo.

Uteuzi wa Anna Mghwira Mwenyekiti wa  chama wa ACT- Wazalendo, ambaye pia alikuwa mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015,  kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, umezua gumzo kubwa nchini.

Wapo Wanaoilalamikia hatua hiyo ya Rais John  Magufuli kumteua kiongozi wa chama cha upinzani kuwa mkuu wa mkoa wakielezea hatua hiyo kuwa ni ama kuua upinzani na wengine wamekwenda mbali zaidi kwa kukiita chama alichokuwa akikiongoza  Mama Anna Mughwira ni CCM B, kwa kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wameteuliwa kuwa viongozi katika Serikali inayoundwa na CCM.

Aliyeanza kuteuliwa kushika wadhifa serikalini kutoka ACT- Wazalendo ni aliyekuwa Mshauri Mkuu wa chama , Prof. Kitila Mkumbo, kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Sasa amefuata Anna Mghwira ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Said Meck Sadick.

Sioni kama kuna tatizo katika hili. Tena umefika wakati katika mazingira ya upinzani uliopo nchini ipo haja ya Katiba yetu, kama si kuendelea na mchakato wa kuiandika upya na kupata Katiba Mpya basi ifanyiwe marekebisho makubwa ili iwe na kipengerle chenye kukilazimisha chama kinachotawala kuunda Serikali ya mseto kwa kuwateua  viongozi  na wanachama kutoka vyama vya upinzani walio na uwezo mzuri wa kuongoza kushika nafasi mbali mbali  serikalini.

Sioni kama kuna sababu ya kuendelea kuendesha nchi kwa umimi na upekee eti kwa sababu tu chama fulani kimepata ridhaa ya kuunda dola na kuwaacha wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani, ambao wanao uwezo mkubwa wa kiuongozi wakibaki kupiga kelele pasipo kuwapa fursa ya kuongoza. Hatua hii  inachelewesha maendeleo.

Ninampongeza sana  Anna Mghwira, kwanza kuaminiwa na  Rais na  kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Ninampongeza pia Rais kwa kuanza kutazama nje ya ulingo wa chama chake CCM na kuanza kuangalia wanachama na viongozi wenye uwezo wa uongozi na kuwateua kumsaidia kuongoza Serikali kwa lengo la kuharakisha maendeleo. Japo hatua hii imenung’unikiwa hata na baadhi ya wanachama wa CCM.

Binafsi sina shaka na Mghwira, ni mwanamke jasiri, shupavu mwenye upeo mpana na mpenda maendeleo. Anathubutu pasi na woga na ni mfano wa  wanawake wanaoweza hata pasipo kuwezeshwa.

Sote tunaukumbuka uwezo wake mkubwa wa kufafanua, kuchanganua na kuainisha vipaumbele vya maendeleo. Akiwa mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,  tunakumbuka namna alivyoweza kulimudu vyema jukwaa la siasa. Namna alivyokuwa mahiri wa kunadi sera za chama chake. Sina shaka sasa ni wakati ambao Anna Mghwira anakwenda kuyafanyia kazi yale yote ambayo alikuwa akiyapigia kelele jukwaani.

Mimi na Watanzania wengine tunawashangaa wanaopinga  na kuponda uteuzi wa Mghwira.Tunakishangaa chama cha ACT- Wazalendo kwa hatua yao ya kumvua uongozi wa uenyekiti wa chama chao Mghwira. Tunajiuliza u wapi uzalendo wa ACT- Wazalendo.? Au ACT- Wazalendo hawajui maana ya uzalendo wanaouhubiri.?

Uzalendo maana yake ni ile hali ya mtu  kuipenda, kuwa tayari  kuilinda na kuitumikia nchi yake. Ikiwa hiyo ndiyo tafsiri halisi ya uzalendo kwa nini ACT wameona kuna tatizo  Mghwira kuitumikia nchi yake?

Hapa kuna tatizo kwa baadhi ya viongozi wa chama hiki cha ACT-Wazalendo. Nilidhani hatua ya chama hiki kupata teuzi za mara kwa mara kwa makada wake kuwa viongozi wa serikali, chama kingelijivunia kwa kuwa na makada mahiri wa chama ambao Serikali inawakubali na kuwaaamini.

ACT-Wazalendo huu ndio ulikuwa mwanya mzuri kwao wa kuonesha umahiri wa viongozi wao kiutendaji ili kesho wakipanda jukwaani waweze kuwa na mifano hai ya kiutendaji uliotukuka kupitia viongozi wake walioteuliwa kuwa viongozi wa Serikali. Kama ACT-  Wazalendo wapo kinyume na hayo, Watanzania wanahoji u wapi uzalendo wao?

Ndiyo sababu nasema, Mghwira, fanya kazi Kilimanjaro. Tekeleza uliyokuwa unayapigania na yaliyokupelekea kuamua kugombea urais.

Sina shaka hukushinikizwa kugombea nafasi ya urais. Ninaamini kuwa ulisukumwa na dhamira ya dhati ya kizalendo. Ninaamini una masuala na ajenda ambazo zinakunyima usingizi, ajenda za maendeo. Huu ndio wakati mwafaka wa wewe kuzitekeleza na kuikata kiu yako ya kuona Watanzania waishio Mkoa wa Kilimanjaro wanapata maendeleo.

Mkoa wa Kilimanjaro una rasilimali nyingi. Ni mkoa wenye ardhi yenye rutuba na unaokaliwa na watu wanaopenda maendeleo. Wahamasishe zaidi watu wa Kilimanjaro, wasimamie wazidi kupata maendeleo.

Simamia rasilimali zilizopo mkoani humo na uzigeuze kuwa chanzo cha wanakilimanjaro na Watanzania kwa ujumla kupata maendeleo. Tekeleza ilani ya CCM, ambayo hakuna mwenye shaka kuwa ni ilani nzuri mno na ikiwa itapata mtekelezaji mzuri wa ilani hiyo basi kuyafikia maendeleo si muujiza.

Shirikiana na Serikali na chama kilichopo madarakani kuijenga Tanzania. Achana na wagombea fito wasiozingatia kuwa sote tunaijenga nyumba moja, nyumba inayoitwa Tanzania.

Mungu ibariki Tanzania.

 [email protected],  0717809933

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles