25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YAFUNGUA PAZIA MIKUTANO YA HADHARA

jaji-kaijage

JOHANES RESPICHIUS Na BRIGHITER MASAKI (TSJ)

-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, ametangaza ratiba ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Dimani, lililopo Zanzibar na mwingine wa nafasi za udiwani katika Halmashauri za Manispaa 20 zilizoko Tanzania Bara.

Jaji Kaijage alitangaza ratiba hiyo katika ofisi za NEC, ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Dk. John Magufuli kumteua zi na kumuapisha Ikulu, Dar es Salaam jana.

Duru za siasa zinadai kuwa hatua ya Jaji Kaijage kutangaza ratiba ya kampeni hizo zinazoonyesha kuanza jana Desemba 23, mwaka huu hadi Januari 21, mwakani ni fursa kwa vyama vya siasa, hasa vya upinzani vilivyosimamisha wagombea wa uchaguzi huo kuanza kufanya mikutano ya hadhara iliyopigwa marufuku hadi mwaka 2020.

Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ilipigwa marufuku Juni, mwaka huu na Magufuli, kwa kile alichokisema kuwa muda wa kufanya siasa umeshamalizika kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana umekwisha na viongozi waachwe wafanye kazi za kuwatumikia wananchi.

Hata hivyo, agizo hilo lilipingwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliyemtaka Magufuli ajiandae kwa lolote, ikiwamo kuongeza magereza baada ya kuvikataza vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa hadi baada ya miaka mitano ijayo, lakini baadaye Jeshi la Polisi likaviruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya ndani na si ya hadhara.

Duru hizo zinaendelea kudai kuwa, kitendo cha mikutano ya hadhara kuzuiliwa kwa miaka mitano na hatua ya kuanza kwa kampeni hizo zilizotangazwa na Jaji Kaijage pengine itatoa nafasi kwa vyama vya siasa kujipanga na kuwatumia viongozi wao wa kitaifa kufanya kampeni Dimani na katika kata 20 na kutumia mikutano hiyo kukosoa mwenendo wa Serikali ya Magufuli.

Pia duru hizo zinasema kuwa, uchaguzi mdogo utakuwa wa aina yake kama vyama vya upinzani vitawatumia viongozi wao wa kitaifa katika kampeni hizo.

Lakini Jaji Kaijage amevitaka vyama vya siasa na wagombea wake kufanya kampeni za kistaarabu ili kufanikisha uchaguzi huo wa marudio utakaofanyika Januari 22, mwakani.

“Kwa mujibu wa kanuni za maadili, kampeni zinatakiwa kuwa za kistaarabu na zinapaswa kuanza saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni. Kamati za maadili zinaundwa katika ngazi mbalimbali ambapo zitakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa maadili katika kipindi chote cha kampeni,” alisema Jaji Kaijage.

Pia alisema pale penye malalamiko, kamati hizo zitatoa uamuzi ili kuweka usawa katika uwanja wa kampeni.

“Vyama vya siasa vinakumbushwa kuzingatia maadili na ratiba za kampeni katika maeneo husika kwa mujibu wa ratiba iliyoratibiwa na msimamizi wa uchaguzi.

“Ratiba hii ilikubaliwa na vyama vinavyoshiriki uchaguzi na kwa mujibu wa sheria iliwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya uchaguzi na pale penye malalamiko chama husika kitapaswa kuwasiliana na msimamizi wa uchaguzi ili aviarifu vyama vingine,” alisema.

Pia alisema vyama vya siasa 13 vinatarajiwa kuchuana kugombea nafasi za udiwani katika kata hizo 20, huku vingine 11 vikichuana kugombea ubunge wa Dimani.

Alisema jumla ya wagombea wote ni 83, huku 11 wakiwa ni wa ubunge na wagombea wa nafasi ya udiwani wakiwa ni 72 na kati yao, watano ni wanawake.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 37(1) b cha sheria ya Uchaguzi, sura ya 343 na kifungu cha 41(1) vya sheria ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sura ya 292 Tume imefanya uteuzi kwa wagombea wa ubunge na udiwani kwa kata mbalimbali. Jumla ya vyama 11 vimesimamisha wagombea wa ubunge katika Jimbo la Dimani, kwa upande wa udiwani katika Halmashauri 20 ni 13. Hivyo jumla ya wagombea wa nafasi ya udiwani ni 72,” alisema.

Jaji Kaijage alisema hadi sasa pingamizi zilizokatwa ni sita na tano zimekatwa katika Kata ya Ihumwa, Manispaa ya Dodoma na moja katika Kata ya Isagehe- Kahama.

Katika hatua nyingine, Jaji Kaijage alisema atafanya kazi yake ya kuiongoza NEC kwa kuzingatia weledi na kiapo chake alichoapa pamoja na sheria na kanuni.

Uchaguzi huo wa marudio unafanyika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo vifo, huku ule wa Dimani unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wake, Hafidh Ali Tahir (CCM), kilichotokea Novemba 11, mwaka huu mkoani Dodoma, alikokuwa akihudhuria Mkutano wa Bunge baada ya kuugua ghafla.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles