21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Ndugai kuwachongea mawaziri watoro

Job Ndugai
Job Ndugai

NA RACHEL MRISHO, DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema atapeleka kwa Rais Dk. John Magufuli majina ya mawaziri watoro wasiohudhuria vikao vya Kamati za Bunge.

Kauli hiyo aliitoa bungeni jana muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuahirisha Bunge hadi Novemba mosi, mwaka huu.

“Waheshimiwa wabunge, kuna jambo moja ambalo nataka niwaambie na linahusu mahudhurio ya wabunge na mawaziri katika vikao vya kamati ambayo si mazuri.

“Kuna orodha nimeiandaa ya watoro katika kamati lakini kwa leo sitawataja hapa kwa sababu nimeona tuendelee kuwafuatilia katika vikao vijavyo. Kama hawatabadilika nitawaambia waajiri wao, yaani wabunge watoro nitawasema kwa wananchi wao na kwa viongozi wa vyama vyao na kwa mawaziri watoro, nitamwambia namba moja, kwamba mawaziri hawa hawawajibiki ipasavyo.

“Kwa hiyo nawaomba mbadilike kwani tumeamua kutangaza mapema ratiba ya vikao vya kamati kwamba vitaanza Oktoba 17 hadi 30 mwaka huu, ili muweze kupanga ratiba zenu vizuri,” alisema Ndugai.

Katika hatua nyingine, alieleza suala la Tanzania kusaini ama kutosaini Makubaliano ya Mafungamano ya Kiuchumi (EPA) kuwa litawasilishwa bungeni na kujadiliwa kabla Serikali haijatoa uamuzi.

“Ni matumaini ya Bunge hili kupitia kwako waziri mkuu kwamba Serikali italisimamia kikamilifu suala hili na kwa wakati mwafaka litaletwa bungeni ikiwezekana katika mkutano wa Bunge lijalo ili tuweze kujadili na kuishauri Serikali ipasavyo.

“Naamini waziri mkuu utalichukulia suala hili kwa uzito unaostahili ili wabunge waweze kulijadili na kuishauri Serikali vizuri endapo tusonge mbele na jambo hilo kama nchi au vinginevyo kabla Serikali haijafanya maamuzi,” alisema Ndugai.

Pia alieleza sababu za kuahirisha kutia saini makubaliano ya mkataba huo hadi Januari, mwakani kuwa ni kutoa nafasi kwa kamati ya wataalamu kuyafanyia kazi maeneo yenye uhitaji wa kupitiwa upya kwa masilahi mapana ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles