25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ndege ya JWTZ yaanguka Mwanza

Na Mwandishi Wetu,

NDEGE ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) imeanguka jana katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Mwanza wakati ikifanya mazoezi.
Akitoa taarifa za kuanguka kwa ndege hiyo katika Makao Makuu ya jeshi hilo yaliyopo Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ, Joseph Masanja, alisema ndege za kivita za JWTZ zilikuwa katika mazoezi ya kawaida na wakati rubani wake, Meja Peter Lyamunda, akijiandaa kuruka, ndipo ndege mnyama akaingia katika moja ya injini na kusababisha kuwaka moto.
Alisema rubani huyo alipoona ndege yake inawaka moto alifanikiwa kuruka nje ya ndege hiyo kwa kutumia vifaa maalumu na kufanikiwa kuokoa maisha yake, ingawa amepata majeraha katika mguu wakati akijiokoa.
“Kwa sasa hali yake ni nzuri na anaendelea na matibabu kama kawaida, wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa hii ni ajali ya kawaida, waendelee na shughuli zao na sehemu ilipoanguka ndege hiyo haikuleta madhara yoyote kwa binadamu, nyumba wala miundombinu,” alisema Masanja.
Katika hatua nyingine, mashuhuda wa ajali hiyo waliliambia MTANZANIA Jumamosi jana kuwa walisikia kishindo kikubwa baada ya ndege hiyo kuanguka na kuwaka moto, huku mabaki ya ndege hiyo yakitapakaa eneo la tukio.
Mbali ya ndege hiyo kuungua, pia nyasi eneo la tukio ziliungua kabla ya kuzimwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.
WANDISHI WAZUIWA, WAKAMATWA
Baadhi ya waandishi wa habari waliofika uwanjani hapo walizuiliwa kupiga picha na baadhi yao kupekuliwa.
Mbali ya kuzuiliwa na askari wa JWTZ, walinyang’anywa vifaa vyao, zikiwamo kamera na simu za mkononi.
“Hamruhusiwi kupiga picha hapa, tunaombeni muangalie kwa macho tu, yaani kula kwa macho tu, ingieni muangalie kisha twendeni eneo la chanzo cha ajali lakini ole wenu atakayeandika taarifa hii, kuweni na subira hadi tutakapowaita.
“Tunawataka taarifa za hapa ziacheni hapa hapa,” alisema askari mmoja aliyekuwa akiwalinda waandishi kuhakikisha hawapigi picha wala kuandika chochote.

Pia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Valentino Mlowola, wote walikuwapo eneo la tukio, lakini walikataa kuzungumza na kudai JWTZ itatoa ufafanuzi wa ajali hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles