28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wagombea urais wapigana vikumbo kwa Komba

kombaNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
KIFO cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kepteni John Komba (CCM), kimewafanya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotajwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kupigana vikumbo huku kila mmoja akizungumzia umuhimu wa kiongozi huyo.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria msiba nyumbani kwa marehemu, Mbezi kwa Komba jijini Dar es Salaam ni pamoja Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wengine ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa.
LOWASSA
Akizungumzia msiba huo, Lowassa alisema ni pigo kwa taifa, CCM na kwake binafsi.
Alisema kuwa, Komba alikuwa mhamasishaji na mpiganaji aliyetaka CCM iendelee kushika dola.
“Kuondoka kwa Komba ni pigo kwa taifa, chama na kwangu binafsi. Taarifa za kifo hiki nilizipata nikiwa njiani natoka Monduli, nilisikitika sana. Kifo hiki kinatupa funzo, kwamba Mungu akitaka, utake usitake, lazima uondoke,” alisema Lowassa.
NGELEJA
Kwa upande wake, Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema (CCM), alisema wamepoteza mtu wa kazi na aliyesimamia mambo aliyokuwa akiyaamini.
Alisema kwamba, Komba alikuwa kiongozi wa kujitolea kwa wananchi na kufundisha uzalendo wa kupenda nchi kwa kupitia nyimbo zake.
“Watanzania tumemkosa mzalendo na tumekosa masomo yake kupitia sanaa. Lakini, natoa rai kwa Serikali kuendelea kuwaenzi na kuwaendeleza wasanii,” alisema Ngeleja.
Alisema funzo aliloliacha Kepteni Komba ni kuwajali wanyonge na kuwatumikia wananchi Watanzania.
MEMBE
Naye akizungumzia kifo hicho, alisema msiba huo umegusa ukanda mzima wa Afrika Mashariki kutokana na umaarufu wa marehemu aliokuwa nao katika sanaa enzi za uhai wake.
“Alipata umaarufu tangu akiwa Chuo cha Ualimu Marangu kule Moshi na baadaye alipokuwa jeshini ambako Mosses Nnaye aligundua sauti yake na kumshawishi kuingia CCM,” alisema.
Membe alimwelezea marehemu Komba kama alikuwa ishara ya upendo, ushirikiano na mshikamano.
“Kifo chake ni kama mshumaa uliozima ghafla, kwani kwa chama alikuwa na nguvu ya kukipa ushindi, hivyo tunamuomba Mungu atupe mshumaa mwingine wa kuendeleza alipoachia Komba.
“Taifa limempoteza mbunge mkweli asiye mnafiki, kitaifa alihusika kuwa shahidi wa kuonyesha mipaka ya Ziwa Nyasa kuwa sehemu ya Tanzania kwa kuonyesha makaburi ya babu zake yaliyopembeni mwa ziwa hilo,” alisema.
MWIGULU
Kutokana na kifo hicho, Mwigulu alisema Kepteni Komba alikuwa ni mtu aliyetengeneza nembo ya CCM na pia ameondoka katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ambacho alikuwa akihitajika zaidi.
Alisema kwamba, alizungumza na marehemu Jumapili iliyopita ambako alimgusia kuhusu maendeleo ya jimbo lake la Mbinga Magharibi.
“Nilimtania kwamba katika nyimbo zako usiache kutaja jina langu, akanitania kwamba jina lako linaimbika. Jambo ambalo sitasahau ni nyimbo zake kuzitumia katika magari ya matangazo zilizosaidia kujaza watu katika mikutano,” alisema.
Dk. Asha-Rose Migiro
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema kifo cha mwanasiasa huyo ni pigo kwa CCM na wabunge wengine pia.
“Nakumbuka siku mbili kabla ya kifo chake, nilikutana naye na akanihakikishia kwamba atapita kwa kishindo Oktoba jimboni mwake.
“Huyu alikuwa kiunganishi cha taifa katika matukio, kwa mfano lile la kifo cha Mwalimu Nyerere kwa kupitia nyimbo zake,” alisema Dk. Migiro.
DK SLAA
Wakati hao wakisema hayo, Dk. Slaa alisema kila mtu atakuwa ameguswa na kifo cha Kepteni Komba kwa kuwa alikuwa akijulikana zaidi na wakati mwingine kuwazidi baadhi ya viongozi wa kitaifa.
“Kifo hicho ni pigo, hasa kwa chama chake cha CCM ambacho alikuwa mhamamishaji wake na pia ni pigo kwetu kwa kuwa inatukumbusha kuwa kila mtu ataondoka na imani yangu ni kwamba, atakuwa ameondoka salama kama tulivyoelezwa na wasemaji wengi hapa,” alisema Dk. Slaa.
Pamoja na hayo, alitoa wito kwa Watanzania kuungana kumuombea marehemu ili afike salama na kuelekea mahali pema na salama.
PROFESA LIPUMBA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kifo cha Kapteni Komba ni pigo kwa CCM na hata kwa Watanzania kwa kuwa alikuwa na mchango mkubwa.
“Kwanza natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi wa Mbinga Magharibi na CCM kwa kuondokewa na mtu muhimu. Kapteni Komba alikuwa mwanasiasa, mwanasanaa na alitoa mchango mkubwa.
“Alihamasisha wananchi kukipigia kura CCM kutokana na nyimbo zake. Kwa kipindi hiki sisi wapinzani tunaungana na wenzetu wa CCM kwa sababu kifo kinamkuta mtu yeyote.
“Nyimbo zake zimependwa si tu na wanachama wa CCM, lakini pia na Watanzania kwa ujumla,” alisema Profesa Lipumba.
MAKINDA
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitoa siri kwamba ndiye aliyemshauri Komba kugombea ubunge mwaka 2005 katika Jimbo la Mbinga Magharibi.
“Nilipokutana naye katika awamu ya pili ya uongozi wa Rais Mkapa, aliniambia nia yake ya kugombea ubunge mwaka 2010, nikamkatalia na kumshauri agombee 2005 na akafanikiwa kupata ubunge,” alisema.
NAPE
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema amempoteza mtu muhimu kwake ambaye alikuwa baba na mhamasishaji wa chama.
“Komba kwangu ni baba kwa sababu baba yangu, Moses Nnauye ndiye alishiriki kumshawishi kutoka Jeshi la Wananchi na kujiunga na CCM,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, Nape alisema anaamini TOT itakuwa imara kwa kuwa Kateni Komba alikuwa amewajenga vijana wadogo.
“Msiba huu umeahirisha ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana mkoani Dodoma na sasa inatarajiwa kuendelea keshokutwa,” alisema.
Khadija Kopa
Naye mwimbaji wa muda mrefu wa Bendi ya TOT aliyokuwa akiiongoza Kapteni Komba, Khadija Kopa, alimuelezea marehemu huyo kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu waliompatia ujasiri alionao hivi sasa.
“Bila ya kunichukua kwa ushawishi wa Moses Nnauye kutoka Zanzibar ambako nilikuwa nikifanya kazi katika Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), leo nisingepata umaarufu huu,” alisema Kopa.
Msemaji awa mbogo
Wakati huo huo, taarifa zilizokuwa zimeenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha mwanasiasa huyo, zilimfanya Katibu wa Bendi ya TOT, Gasper Tumaini, kuwa mbogo na kushangazwa na hoja zinazoibuliwa kuhusu mali za marehemu na kifo chake.
Alisema taarifa za kupigwa mnada kwa nyumba za marehemu si sahihi, kwani siku kadhaa chache zilizopita, Kapteni Komba alikuwa akiugua ugonjwa wa shinikizo la damu pamoja na kisukari.
“Habari hizo zimekuwepo kwa muda mrefu na wala hazikuwa na ukweli wowote zaidi ya kwamba amefariki kutokana na maradhi ya shinikizo la damu na kisukari,” alisema.
Alisema kwamba, marehemu Komba alifariki akiwa katika mipango ya kustaafu muziki, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Jumapili iliyopita alikuwa akifanya mazoezi ya wimbo wake mpya ambao alitarajia kuutoa hivi karibuni, baada ya kutoa wimbo ulioanza kutamba unaoitwa CCM ni ile ile’,” alisema.
Andrew Komba
Mtoto mkubwa wa marehemu Komba, Andrew Komba, alisema kama familia wamepata pigo kubwa kwa kuwa ndiye alikuwa akiunganisha familia na alijenga misingi ya kupendana na kusaidiana.
Ratiba ya mazishi
Akitoa ratiba ya mazishi, Msemaji wa Familia hiyo, Dominic Mwakangale, alisema itakuwa imegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni chama na Bunge.
Alisema kuwa, jana mwili wa marehemu ulitolewa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam saa 10 jioni na kupelekwa kanisani kwa ajili ya maombezi. Leo saa nne asubuhi, mwili huo utaagwa katika Viwanja vya Karimjee.
Baada ya kumalizika kwa shughuli hiyo, alisema mwili wa marehemu utachukuliwa na kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea Songea kwa ajili ya mazishi.
KIFO
Kapteni Komba alifariki juzi jioni ambapo taarifa iliyotolewa na Hospitali ta TMJ alikokuwa akipatiwa matibabu, zilieleza kuwa alifariki dunia kwa ugonjwa wa shinikizo la damu na kisukari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles