Ndayiragije aanika mkakati wake Stars

0
535

Mohamed Kassara-Dar es salaam

KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, amesema mkakati wake wa kwanza ni kupata ushindi mnono nyumbani ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali za Mataifa Afrika  kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) zitazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Stars itakuwa nyumbani kumenyana na Sudan katika mchezo wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali hizo kwa mara pili, utakaopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ndayiragije alisema baada ya wachezaji wake wote kuwasili kambini, ameanza kuisuka kikamilifu safu ya ushambuliaji ili iwe na makali ya kutosha yatakayowapa ushindi katika mchezo huo.

Ndayiragije aliongeza kuwa, kiujumla ana kazi mbili za kufanya kwenye kikosi chake kabla ya kuikabili Sudan, kwanza ni kupunguza makosa katika idara ya ulinzi ili isiruhusu mabao, lakini pia kuongeza kasi ya washambuliaji kucheka na nyavu ili kumaliza mapema shughuli nyumbani

“Kikosi kipo kamili kwa ajili ya mchezo huo, wachezaji wote tayari wameshawasili kambini. Kwa sasa tunaendelea na programu zetu kulingana na ubora wa mpinzani wetu, kikubwa tunachokifanya ni kuhakikisha tunapata ushindi mnono nyumbani ili kujipunguzia kazi ugenini.

“Mchezo huu tutaanzia nyumbani, hivyo lazima tutumie vema faida hiyo, tunatakiwa kwenda ugenini tukiwa na mtaji mkubwa wa mabao, tulishindwa kufanya hivyo dhidi ya Kenya, tukajipa mzigo mzito ugenini, lakini safari hii tunataka kuanza vizuri kwa ushindi nyumbani,” alisema Ndayiragije.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here