25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

‘NASA IMEPANGA KITUO CHA KUHESABU KURA TANZANIA’

NAIROBI, KENYA

KIONGOZI wa wengi katika Bunge la Taifa la Kenya, Aden Duale amedai muungano wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), unapanga kuanzisha kituo sambamba cha kujumuisha kura nchini Tanzania.

Akihutubia kongamano la taifa la wajumbe wa Chama tawala cha Jubilee (JP) kwenye Ukumbi wa Bomas, mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema NASA imepanga kuiba kura kwa kudukua mitambo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikiwamo kupitia nchi jirani.

"Tunajua wale wapinzani wetu wanapanga kuanzisha kituo cha kujumuisha kura nchini Tanzania na kudukua mitambo ya IEBC kufanikisha njama yao ya kuiba kura. Hii ndio maana juzi mliwasikia wakisema watapata kura milioni 10," alisema Mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Hata hivyo, Duale hakutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yake, ambayo huenda yakaathiri uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kenya na Tanzania.

Pamoja na kutokuwapo ushahidi wa jambo hilo, kitendo cha Duala kuihusisha Tanzania pengine kinatokana na uwapo uhusiano ulioshiba baina ya mgombea urais wa NASA, Raila Odinga na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Mbunge huyo alitoa wito kwa wafuasi wa Jubilee kuhakikisha wanalinda kura za Rais Uhuru Kenyatta ili zisiibwe na watu wa NASA, ambao alidai wameweka mbele masilahi yao badala ya wananchi wa kawaida".

Itakumbukwa mapema mwaka huu, Duale aliihusisha NASA na kisa ambapo wahuni walikamatwa kwa tuhuma za kudukua mitandao ya benki kadhaa nchini kuiba fedha.

Wakati Duale akitoa madai hayo, Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto walikuwa wakiidhinishwa rasmi na wajumbe wa Jubilee kutetea nyadhifa zao katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na zaidi ya wajumbe 4,000 kutoka pembe zote nchini.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,227FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles