30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TUTAWAKUMBUKA DAIMA

Na Waandishi Wetu-ARUSHA

TUTAWAKUMBUKA daima. Hayo ndiyo maneno ya mwisho ya waombelezaji waliokuwa wakiyatoa wakati wa kuaga miili ya wanafunzi 33 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya jijini Arusha.

Miili ya wanafunzo hao, walimu wao wawili pamoja na dereva wa gari hilo iliagwa jana katika ibada maalumu iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambapo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliongoza maelfu ya waombolezaji.

Mbali na Makamu wa Rais viongozi mbalimbali walihudhudhuria mazishi hayo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, mawaziri, wabunge na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani.

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya wanafunzi hao, Makamu wa Rais ambaye alihudhuria msiba huo kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, alisema taifa linahuzunika kutokana na kuondokewa na nguvu kazi.

Alisema taifa zima linaomboleza huku akiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na uwezo wa gari wa kubeba abiria.

“Tukio hili linatukumbusha wajibu wetu, ninapaza sauti kwa madereva wetu wawe makini wanapoendesha magari, wazingatie alama za barabarani lakini pia wasiendeshe magari wakiwa wametumia kilevi chochote. Ndiyo maana tunapiga vita matumizi ya dawa za kulevya maana pia ni chanzo cha matukio kama haya.

“Msiba huu si wenu peke yenu, taifa zima linaomboleza pamoja nanyi kwa kuondokewa na nguvu kazi ya taifa hili, tulikuwa na malengo makubwa na wapendwa wetu hawa.

“Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye amenituma niwafikishie salamu za pole nyingi sana na rambirambi zetu kwa wazazi ndugu, jamaa na marafiki mliofiwa na wapendwa wenu,” alisema Samia.

Alisema ni jambo lisilopendeza katika nchi kusikia kila siku matukio ya ajali  ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya watu.

Kutokana na hali hiyo alisema kuanzia sasa Serikali itaweka alama zinazoonekana katika barabara zote ili madereva waweze kuchukua hadhari.

“Haipendezi kila siku kusikia ajali, taasisi zote zinazohusika, wizara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani hakikisheni mnaweka alama za barabarani lakini pia magari ya abiria yakaguliwe na yabebe abiria kadiri ya uwezo wake na si vinginevyo,” alisema.

Makamu wa Rais, alitumia fursa hiyo kuwashukuru watalii raia wa Marekani ambao ni madaktari waliotoa huduma ya kwanza kwa majeruhi katika eneo la ajali wakati wakiwa njiani kuelekea katika hifadhi na mbunga za wanyama.

Mbali hilo Samia aliishukuru Serikali ya Kenya kwa kutuma mwakilishi ambaye ni Waziri wa Elimu, Dk. Fred Matiagi katika msiba huo.

“Wakati ajali inatokea kulikuwa na watalii walikuwa wanakwenda kutembelea hifadhi kwa bahati nzuri walikuwa madaktari kutoka Marekani walipofika eneo la ajali walijitolea kutoa huduma tangu wakati huo mpaka sasa na walikatisha safari na wanaendelea kushirikiana na madaktari wetu na wanatamani kuwachukua majeruhi kuwapeleka nje ya nchi tunawashukuru sana.

 “Pia tunamshukuru kipekee Rais Uhuru Kenyatta pamoja na jirani zetu Wakenya kwa faraja mliyotupatia, kama vile haitoshi Rais Kenyatta amemtuma Waziri wa Elimu,  Dk. Matiagi,  tunawashukuru sana jirani zetu na ndugu zetu katikaJumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema

Waziri wa Elimu Kenya

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Uhuru Kenyatta, Dk. Matiagi alisema msiba huo ni wa wananchi wote wa EAC.

“Nimetumwa na Rais Uhuru, tunahuzunika wote pamoja na ninyi wananchi wa Tanzania. Ajali hii imetulazimisha kujitafakari kwa siku mbili hizi, tumefikiri kuhusu usalama wa watoto wetu kuhusu usafiri wa watoto wetu ambao ni wanafunzi .

“…Taifa la Kenya linaungana na wazazi ndugu na wananchi wote kuomboleza na kutoa pole, tunasema huu msiba unatuhusu wote,”alisema WDk. Matiagi

Waziri Aboud

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Poli wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mohamed Aboud, alisema wamepokea taarifa za vifo vya watoto na walimu wao kwa huzuni na kwamba SMZ inashirikiana na familia za marehemu na Watanzania wote kuomboleza msiba huo.

“Kwa niaba ya Rais Shein (Rais wa Zanzibar),  tunatoa salamu za pole kwa wananchi wa Arusha, wazazi wa watoto na ndugu wote, taarifa hizi tulizipokea kwa mshituko mkubwa ni jambo la kuhuzunisha sana Serikali ya Zanzibar inashirikiana nanyi kwa hali zote katika msiba huu,” alisema

Mbowe

Naye Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, alisema taifa limepewa muda mwingine wa kutafakari amani, mshikamano na umoja uliopo.

“Tumepewa siku nyingine ya kutafakari umoja wetu wa kitaifa, amani yetu na mshikamano wetu wa kitaifa kwa niaba ya wabunge wa vyama vyote vya upinzani tunatoa pole kwa msiba huu ambao umesababisha mshtuko mkubwa kwetu sote. Sote tupo bega kwa bega na Serikali kwa jambo lolote linalohitajika,” alisema Mbowe.

Gambo na kauli tata

Wakati akiwatambulisha viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya kuaga miili hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema iwapo asingewatambulisha baadhi ya viongozi waliofika pengine asingebaki salama.

Baada ya kutoa maelezo hayo ndipo alipomtambulisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hali iliyowafanya waombolezaji waliofika uwanjani hapo kuanza kushangilia.

Pamoja na kumtambulisha Lowassa, Gambo hakumtambulisha hasimu wake wa kisiasa mkoani humo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema pamoja na Meya wa jiji hilo, Calist Lazaro wote wa Chadema na hivyo kuzua minong’ono ya chinichini.

Kinana aibukia msibani

Licha ya kuripotiwa kwa taarifa ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwamba amepewa likizo ya mapumziko na chama chake kutokana na matibabu aliyokuwa akipata nje ya nchi, kiongozi huyo jana aliibuka katika msiba huo.

Kinana ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Arusha miaka ya 1990, alilazimika kukatisha mapumziko yake ambapo alikiwakilisha chama chake na kutoa salamu.

“Nasimama nanyi hapa kuomboleza, natoa pole nyingi na salamu za rambirambi kwa wafiwa, wazazi , ndugu na jamaa mliopoteza wapendwa wenu. Vifo vya wapendwa hawa vimetuunganisha poleni sana,” alisema.

Ateta na Lowassa

Wakati wa kuelekea kutoa heshima za mwisho kwa marehemu hao, Kinana alionekana kuteta jambo na rafiki yake wa zamani Edward Lowassa kwa muda usiozidi dakika tatu.

Wakiwa katika eneo hilo viongozi hao walionekana wakiwa katika mazungumzo hayo ya muda mfupi na kisha baada ya hapo kila mmoja alielekea katika gari yake.

Profesa Ndalichako

Akizungumza katika msiba huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako,  alisema vifo vya wanafunzi hao na walimu wao viwe chachu kwa Watanzania kuwekeza katika elimu.

“Watoto hawa walifariki wakiwa katika harakati za kujiandaa na mitihani, maana yake wazazi na walimu wa watoto wetu hawa walikuwa wamewekeza kwenye elimu tuwaenzi kwa kufanya bidii na kuwekeza kwenye elimu,” alisema Prof.  Ndalichako.

Waziri Ummy Mwalimu

Kwa upande wake Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema vifo vya watoto hao vimetokea wakati wazazi tayari walikuwa wakitimiza wajibu wao wa kutoa haki ya msingi ya kuwapatia eleimu lakini ajali imekatisha ndoto yao.

 “Wizara yangu inahusika pia na watoto ,tunatoa salamu nyingi za pole kwa ndugu na jamaa wote. Vifo hivi vilitokea wakati wazazi wakitimiza wajibu wao wa kuwapa watoto haki yao ya msingi ya elimu, sote tunaenzi watoto hawa,”  alisema Ummy

Simbachawene azua jambo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  George Simbachawene,  alipingana na wote waliotoa salamu za pole wakihusisha ajali hiyo na mpango wa Mungu.

“Tamisemi pia inahusika na elimu, tunatoa pole nyingi kwa wafiwa na wananchi wote. Lakini mimi napingana na dhana hii kwamba vifo vya aina hii ni mpango wa Mungu, huu ni mpango wa shetani.

“Najua jinsi ilivyo ngumu kubeba uzito wa msiba huu hasa kwa wale walioguswa moja kwa moja lakini viongozi wa dini wako hapa mtanisaidia, mimi siamini kama kila kifo ni mpango wa Mungu,” alisema Simbachawene.

Viongozi wa dini

Nao viongozi wa dini ambao walikuwa akizungumza kwenye ibada hiyo, wakiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu, Askofu Solomon Masangwa wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Askofu Dk. Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikan na Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaban Juma.

Katika ujumbe wa viongozi hao wa dini kila mmoja walisisitiza umuhimu wa binadamu kujiandaa kwa maisha ya hapa duniani.

Lema alalama

Katika hatua nyingine Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alimtupia lawama Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa kile alichodai  kunyimwa kutoa salamu za pole wakati wa kuaga miili ya wanafunzi hao.

 “Mimi kama mbunge mwenyeji niliyefiwa jimboni kwangu pamoja na meya tulipata taarifa juzi jioni kwamba katika maombolezo haya leo (jana) viongozi wa Chadema hawapaswi kuzungumza.

“Nilimpigia simu Mbunge wa Ngorongoro, William Ole Nasha, nikamweleza ubaguzi mchafu unavyopangwa katika jambo hili muhimu la kuaga watoto wetu, alinihakikishia kuwa Makamu wa Rais asingeweza kukubaliana na ujinga huo.

“Baada ya kuingia uwanjani, jina langu lilikuwepo kwenye ratiba kwa ajili ya salamu za rambirambi, lakini baada ya Mkuu wa Mkoa kukabidhiwa itifaki, mambo yalibadilika na ilionekana dhahiri kuwa sitakiwi kabisa kutoa pole kwa watu wa jimbo langu waliofikwa na msiba huu.

“Mwenyekiti Mbowe (Freeman) aliandika meseji kwenda kwa Makamu wa Rais kukumbusha umuhimu wa wenyeji kutoa salamu, Makamu wa Rais baada ya kupokea meseji hiyo, alimwita Mkuu wa Mkoa, ndipo ilionekana kama kuna ushindani unatokea kati yao, lakini hatukuweza kabisa kupata nafasi ya kutoa salamu kwa wapendwa wetu.

“Wabunge wa CCM waliokuwepo ambao ni mawaziri wote waliweza kutoa pole, huu ni ubaguzi uliojaa ujinga na chuki mbaya kisiasa, nitaeleza madhara yake kwenye hotuba yangu leo,” alisema Lema.

Bunge lachangia mil. 100/-

Jana Bunge lilitangaza kutoa rambirambi ya Sh milioni 100 kwa ajili ya wanafunzi 32 waliofariki dunia katika ajali hiyo.

Rambirambi hizo pia zitahusisha dereva mmoja na walimu wawili waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Spika wa Bunge, Job Ndugai aliliambia Bunge, kwamba fedha hizo zilipatikana baada ya wabunge hao kukubali kukatwa posho zao za siku moja.

“Waheshimiwa wabunge, kama mtakumbuka asubuhi niliwaambia kwamba, nimepata ushauri kutoka kambi zote mbili hapa bungeni kuhusu ajali iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa basi la Shule ya Luck Vicent ya Arusha.

“Baada ya kuwaeleza kuhusu ushauri huo uliohusu kukatwa posho zenu za siku moja ili fedha zitakazopatikana zipelekwe kwa wafiwa kwa kiwango sawa, sasa nataka niwape taarifa ya fedha zilizopatikana.

“Kupitia michango yenu wabunge, zimepatikana shilingi milioni 86 na ofisi ya Bunge itatoa shilingi milioni 14.

“Kwa maana hiyo, jumla tumepata shilingi milioni 100 ambazo tutazipeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ili zikagawiwe kwa familia za wafiwa kwa viwango sawa,” alisema Spika Ndugai.

MCT yaionyooshea kidole TBC

Baraza la Habari Tanzania (MCT), limelishutumu Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na vyombo vingine vya kielektoniki kwa kushindwa kulipa uzito mapema tukio la ajali hiyo.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema vyombo hivyo vimeonesha udhaifu mkubwa kwa kuendelea na program nyingine za vipindi wakati nchi iko kwenye majonzi makubwa.

“Imefika wakati sasa TBC kujiimarisha kuwa ni chombo cha umma na wajiwekeze katika kuripoti masuala ya wananchi kwa kuwa kinaendeshwa kwa kodi zao.

“Ni jambo la fedheha kwa chombo cha umma  kuendelea na vipindi vya kawaida wakati Taifa lipo kwenye majonzi makubwa,”alisema Kajubi.

 Mbali na hilo, Kajubi alisema baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti tukio hilo vilikiuka kanuni za maadili ya uandishi wa habari.

Alitaja baadhi ya ukiukwaji huo wa kanuni kuwa ni pamoja na kutumia picha za maiti ya ajali hiyo iliyotikisa nchi.

 “Lipo gazeti kongwe na linaloheshimika la kila Jumapili lililochapisha picha hizo katika ukurasa wake wa mbele, hii inasikitisha sana,” alisema Kajubi.

Habari hii imeandaliwa na ABRAHAM GWANDU, ELIYA MBONEA , JANETH MUSHI (Arusha), MAREGESI PAUL (DODOMA) na MANENO SELANYIKA (DAR).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles