25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Nani kutangulia robo fainali Uefa wiki hii?

 BADI MCHOMOLLO 

MICHEZO ya mwisho ya 16 bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajiwa kuanza wiki hii na kufikia mwisho wiki ijayo.

Wiki hii tunatarajia kuziona timu nne zikiaga mashindano hayo, huku nne zingine zikisubiri wiki ijayo kufungashiwa virago.

Hii ni moja kati ya hatua ngumu kutokana na michezo hiyo kupigwa nyumbani na ugenini, hivyo timu ambayo itaweza kutumia vizuri nafasi inaweza kusonga hatua inayofuata.

Timu zenye nafasi kubwa ya kufanya vizuri ni zile ambazo zilianza vizuri kwenye michezo ya kwanza hatua hii, lakini chochote kinaweza kutokea kwa kuwa soka ni mchezo wa makosa.

SPOTIKIKI leo hii imekuanikia timu nne zenye nafasi kubwa ya kusonga mbele hatua ya robo fainali kutokana na kile walichokifanya kwenye mchezo wao wa awali.

RB Leipzig Vs Tottenham

Unaweza kusema ndani ya klabu ya Tottenham kuna mgomo wa wachezaji kutokana na timu hiyo kushindwa kufanya vizuri katika baadhi ya michezo kwa siku za hivi karibuni.

Ndio, kuna baadhi ya wachezaji wanadai hawana furaha chini ya kocha wao Jose Mourinho, hii inaweza kusababisha timu hiyo kushindwa kufanya vizuri.

Katika mchezo wa kwanza ambapo Tottenham walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya wapinzani hao RB Leipzig, walikubali kichapo cha bao 1-0, jambo ambalo linawapa wakati mgumu Tottenham wakiwa ugenini kesho.

Tottenham walitabiriwa kufanya vizuri msimu huu baada ya kuishia fainali msimu uliopita chini ya kocha wao Mauricio Pochettino ambaye alifukuzwa kazi msimu huu kutokana na mwenendo mbaya wa timu hasa kwenye michuano ya Ligi Kuu England.

Katika historia, huu ni mchezo wa pili kwa timu hizi kuwahi kukutana, hivyo Tottenham wataingia mchezoni kwa lengo la kutaka kulipa kiasi na kufuzu hatua inayofuata. RB Leipzig wao wanahitaji sare ya bila kufungana au ushindi, wakati huo Tottenham wakihitaji ushindi jambo ambalo linaweza kuwa ngumu kwao, hivyo mchezo huu utakuwa na ushindani wa hali ya juu.

Valencia Vs Atalanta

Ushindani wa timu hizi utakuwa tofauti kidogo kutokana na ubora wao, lakini kila mmoja katika ligi yake amekuwa akipambana kutafuta nafasi nne za juu.

Kule nchini Italia klabu ya Atalanta FC wanapambana vizuri na wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi, wakati huo nchini Hispania, Valencia wanashika nafasi ya saba.

Timu hizi mbili hazina historia kubwa ya kukutana kwenye michuano yoyote, lakini waliwahi kucheza mchezo wa kirafiki mwaka 2017 na Valencia wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani walikubali kichapo cha mabao 2-1, huku mcheo uliopita Valencia wakikubali kichapo cha mabao 4-1.

Bado Valencia wana kibarua kizito cha kufanya kuhakikisha wanasonga hatua hinayofuata kwa kuwa mchezo huo wa kesho wanatakiwa kushinda jumla ya mabao 3-0, jambo ambalo linaonekana kuwa ngumu hasa kwa ubora wa washambuliaji wa Atalanta kutoka bila ya bao, hivyo safari ya Valencia inaweza ikafikia mwisho kesho, lakini chochote kinaweza kutokea.

PSG Vs Dortmund

Hapa napo kipute kipo, mchezo huu utapigwa kesho kutwa huku wababe hao wa soka nchini Ufaransa wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani na kuwakaribisha wapinzani hao.

Mchezo uliopita Dortmund walikuwa nyumbani na kufanikiwa kushinda mabao 2-1, bado mchezo wa marudiano unaonekana kuwa mgumu kwa kuwa Dortmud watakuwa ugenini huku wakiwa na kazi kubwa ya kumzuia Kylian Mbappe, Neymar, Cavan na wengine wasipate ushindi, lakini PSG wanahitaji ushindi wa bao 1-0 ili kusonga mbele kwa kuwa watakuwa na faida ya bao la ugenini.

Kazi kubwa ya Dortmund ni kulinda ushindi walioupata kwenye mchezo uliopita, lakini lazima watengeneze nafasi za kushambulia ili wawe kupata bao kwa ajili ya kujihakikishia nafasi ya kuendelea hatua ya robo fainali. Mchezo huo utakuwa na ushindani wa aina yake, kila timu itahitaji nafasi, hivyo mwenye kufanya kosa anaweza kuwa kwenye wakati mgumu.

Liverpool Vs Atletico Madrid

Huu utakuwa mchezo wa kibabe, Liverpool ambao ni mabingwa watetezi watakuwa kwenye Uwanja wa nyumbani Anfield kuwakaribisha Atletico Madrid ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliopita.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp mara baada ya kukubali kichapo hicho kwenye mchezo wa kwanza, aliwaambia mashabiki wa Atletico Madrid wajitokeze kwa wingi pale Anfield kuiangalia timu yao inavyoaga michuano hiyo.

Klopp alikuwa na maana kuwa mpinzani ambaye anakuja kwenye uwanja huo hawezi kutoka salama, hivyo Liverpool wanajiamini kwa kiasi kikubwa kuweza kushinda mchezo huo na kusonga mbele hatua ya robo fainali.

Hata kwa upande wa kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone, anaamini safari hii kikosi chake kitakuwa bora zaidi ya mchezo wa kwanza kwa kuwa wakati ule aliwatumia baadhi ya wachezaji huku wakiwa majeruhi kama vile Diego Costa na Alvaro Morata, huku wengine ambao walikuwa majeruhi ni pamoja na Jose Gimenez, Kieran Trippier, Santiago Arias na Hector Herrera, lakini kwa sasa wapo fiti.

Atletico wanahitaji kulinda ushindi wao au sare ya aina yoyote kwenye uwanja wa ugenini, wakati huo Liverpool wakihitaji ushindi kuanzia mabao mawili. Mbali na Liverpool kuwa mabingwa watetezi, lakini wana kazi kubwa ya kufanya.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles