22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Naibu Waziri atoa maagizo kwa wenye viwanda kulinda mazingira nchini

Na Clara Matimo, Mwanza

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis amesema amebaini bado kuna watu wanakiuka maagizo ya Serikali kwa kutengeneza mifuko ya plastiki isiyokidhi vigezo, ambapo ametoa maagizo manne mazito ili kuhakikisha jitihada za utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini zinafanikiwa.

Khamis ametoa maagizo hayo leo Jumatano Februari 22, 2023 baada ya kutembelea dampo la kisasa la Buhongwa jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa na kubaini uwepo wa taka nyingi za plastiki ambazo zinatolewa mitaani.

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis Akisikiliza maelezo jinsi mradi wa dampo la kisasa lililopo Kata ya Buhongwa Wilaya ya Nyamgana linavyofanya kazi kutoka kwa Afisa Mazingira halmashauri ya jiji la Mwanza, Desderius Polle(mwenye kofia) alipotembelea mradi huo Februari 22, 2023.

Hivyo, ameziagiza kamati zote zinazohusika na uhifadhi, utunzaji wa mazingira kusimamia mianya yote inayopenyeza taka za plastiki ambazo ni hatarishi kwa misha ya wananchi kwani Serikali iliishapiga marufuku mifuko hiyo kuingia, kutengenezwa na kutumiwa nchini, ambapo watakaobainika kujishughulisha, kuiingiza au kuitengeneza wachukuliwe hatua za kisheria.

Vilevile, ameagiza magari yote yanayobeba takataka kutoka mitaani kupeleka dampo yafunikwe ili kuepusha taka hizo kudondoka barabarani na kuleta athari kwa wananchi kwani amebaini taka hizo zimekuwa zikidondoka na kumwagika njiani na kuachwa bila kuzolewa.

“Tatu, tumepokea malalamiko ya wananchi kwamba wanalipa ushuru ili kuzolewa taka lakini hazichukuliwi kwa wakati hivyo naagiza ziwe zinachukuliwa kwa wakati ili zisilete madhara zaidi. Vilevile, naagiza maeneo yote ya dampo yapandwe miti inayoweza kuhimili mazingira husika ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Khamis na kuongeza

“Kuna baadhi ya watu wanatupa taka kwenye vyanzo vya maji wakati kwenye taka hizo zipo zenye sumu, ngumu, nyepesi, majimaji, plastiki na za kila aina na sumu hiyo inaleta athari kubwa kwa viumbe vinavyoishi ndani ya maji, hivyo tukasimamie utupaji mzuri wa taka atakayetupa karibu na chanzo cha maji achukuliwe hatua za kisheria, tutunzeni vyanzo vya maji, tupande miti sana, tupunguze athari,”.

Aidha Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis ameviagiza viwanda vyote nchini kutenga fungu maalumu kwa ajili ya kusaidia shughuli zote za mazingira katika maeneo husika ikiwemo usafi, upandaji miti na kutoa elimu inayohusu mazingira.

Naye, Meneja wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, Jarome Kayombo amesema baraza hilo limeyapokea maagizo ya serikali na litasimamia viwanda vyote vitekeleze majukumu yao kwa kufuata vigezo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema ofisi yake itasimamia sheria zote za utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili mkoa huo uweze kuvutia watalii ambapo amewataka wanaojihusisha na biashara ya mifuko ya plastiki kuacha mara moja kwa kuwa watawasaka hadi kuwamata ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira halmashauri ya jiji la Mwanza, Desderius Polle amesema jiji hilo huzalisha tani 357 kwa siku kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikwamo majumbani, maeneo ya biashara, viwandani, taasisi za umma na binafsi huku likiwa na uwezo wa kuhudumia tani 265 kwa siku ambazo kabla ya kusafirishwa kwenda dampo hutunzwa na kuhifadhiwa kwenye vyombo maalum (skip buckets).

“Manufaa ya mradi wa dampo la kisasa la Buhongwa tumefanikiwa kuzuia uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na utupaji hovyo taka ngumu, kuzuia harufu mbaya inayotokana na kuoza kwa taka ngumu, kutengeneza mazingira ambako urejeshaji taka ngumu unafanyika kwa usimamizi wa kitaalam na kuongeza kipato kwa halmashauri ya jiji,” amebainisha Polle.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, Katibu Tawala halmashauri ya Jiji la Mwanza, Alfred Yonas amesema wameunda kamati maalum yenye wataalamu mbalimbali wakiwemo wa mazingira na afya ambao watashauri maeneo ya kupanda maua, miti na kuweka vyungu ili kulipendezesha jiji hilo na tayari wamepanda miti 9,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles