24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Nabii Bushiri, mkewe wakamatwa kwa udanganyifu, utakatishaji Sh bilioni

RUSTENBURG, Afrika Kusini

NABII aliyejizolea umaarufu ndani na nje ya Bara la Afrika wa Kanisa la Enlightened Christian Gathering (ECG), Shepherd Bushiri na mkewe, Mary, wamekamatwa na kikosi cha Hawks mjini Rustenburg kwa makosa ya udanganyifu na kutakatisha fedha zinazofikia Randi milioni 15 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 2.6.

Kikosi cha Hawks kilithibitisha kuwakamata Bushiri na mkewe Ijumaa wiki hii na wakati huo huo kanisa lake likithibitisha wanandoa hao kuwekwa ndani.

Kikosi cha Hawks kinajihusisha na uchunguzi wa makosa ya jinai kama rushwa, uhujumu uchumi na mengine yanayohusiana nayo.

Msemaji wa kikosi cha Hawks, Brigedia Hangwani Mulaudzi, alisema Bushiri na mkewe walikamatwa katika hoteli ya kifahari Rustenburg.

Brigedia Mulaudzi alisema kesi dhidi ya watuhumiwa hao inahusiana na makosa ya jinai ya udanganyifu na kutakatisha fedha pamoja na kuvunja sheria ya makosa ya jinai ambayo walitenda mwaka 2015.

Makosa hayo yanahusiana na sheria ya kubadilisha fedha za kigeni ambacho ni kiasi cha dola 1,147,200 sawa na Randi milioni 15.

Aliongeza kuwa Nabii huyo na mkewe ambao wanaendesha biashara mbalimbali nchini Afrika Kusini na nje ya nchi hiyo, wanatarajiwa kupanda kizimbani kesho katika Mahakama ya Kibiashara mjini Pretoria nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wa Nabii huyo katika mtandao wa Facebook, imesema tukio la kukamatwa kwake lilitokea saa 07:00 wakati akiwa katika Hoteli ya Sparkling Waters mjini Rustenburg.

“Walimchukua Nabii Bushiri na mama yetu Mary Bushiri na kuwafunga pingu kuwapeleka Pretoria. Wamemshtaki baba yetu kwa makosa ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Tukio la kukamatwa kwake limekuja katika siku ambayo Tume ya CRL ilisafisha jina lake kuhusika na vifo vya watu watatu waliofariki kanisani hapo na kusisitiza kwamba kanisa la Pretoria analoliongoza linaendeshwa kwa taratibu na sheria za wazi.

Mwezi Aprili mwaka jana, gazeti la Sunday World liliripoti kuwa Nabii Bushiri anaingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia kanisa lake nchini Afrika Kusini na kwamba alikuwa na uwezo wa kutuma Randi milioni 15 kwa mwezi kwenda nchini mwake Malawi.

Mulaudzi amewahi kulithibitishia gazeti hilo kipindi hicho kwamba Kikosi cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai cha Hawks, kilikuwa kinamchunguza Nabii huyo, lakini alikataa kuzungumzia undani wa uchunguzi huo kwa madai ni mapema sana na suala lenyewe lilikuwa katika hatua za awali hivyo hakukuwa na nyaraka za uthibitisho.

Nabii huyo mtata alikiambia kituo cha televisheni cha SABC News kuwa hakuwa na taarifa kama Jeshi la Polisi lilikuwa linamchunguza na kwamba alisikia uchunguzi huo kupitia vyombo vya habari.

Hivi karibuni Bushiri alikanusha madai ya kanisa lake kuwataka waumini kulipia huduma ya kuonana naye katika maombi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles