25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

MZOZO WA ARDHI WAWAKUTANISHA DC MURO, BATILDA

Na JANETH MUSHI-ARUMERU             |              


MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, juzi amekuwa mbogo wakati wa utatuzi wa mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Kijiji cha Engutukoit na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Buriani.

Katika mgogoro huo, Dk. Batilda anadaiwa kumiliki shamba lenye ekari 2,144 lililosajiliwa kwa hati namba 101178 na L.O no 13254 lililoko katika kijiji hicho na kwa sasa wananchi hao wamevamia na kulitumia kama eneo la malisho huku wakidai ni eneo lao la kijiji na hawamtambui.

Kutokana na mgogoro huo, Muro akiambatana na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, walifika kijijini hapo katika mkutano wa hadhara uliokusudia kujadiliana na kufikia mwafaka.

Hata hivyo, majadiliano baina ya wananchi na Muro yaliibua mvutano mkali uliodumu kwa zaidi ya saa nne wakati walipoeleweshwa juu ya utaratibu wa umiliki wa ardhi.

Muro alikuwa mkali kuhusu mgogoro huo baada ya wananchi hao kukataa maelekezo yake kuwa wataalamu wa upimaji watafika katika eneo hilo kwa upimaji na kuhakiki mipaka ili eneo la kijiji liainishwe na eneo la Dk. Batilda lianishwe kumaliza mgogoro huo na alimwagiza Mwenyekiti wa kijiji hicho, Samuel Saruni, kusimamia mchakato huo.

“Tumebaini kukosekana kwa elimu ya kutosha kwa masuala yanayohusu ardhi, jambo la kwanza tutakalofanya kuanzia wiki ijayo ni kuleta wapimaji ili wapime na kuainisha maeneo, eneo lipi ni la Serikali ya Kijiji na lipi ni eneo la mwekezaji na tukishapima kila mmoja ataishi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu bila kuingiliana.

“Hata kama hutaki, Serikali inafanya kazi kwa kufuata sheria, hivyo mkubali kufuata sheria, mwenyekiti nakuagiza kuanzia sasa wiki ijayo uwapokee wataalamu watakaokuja kupima ardhi ila anza kutoa elimu kwa wananchi, asitokee mtu atakayezuia mchakato huu, kama wana mambo mengine ya msingi waje ofisini tuzungumze, watu hatugomi, tunazungumza na migogoro inakwisha kwa watu kufuata taratibu,” alisema.

Muro aliwaeleza wananachi hao kuwa Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya vijiji, uhifadhi na kuwataka wakubaliane kuwa hayawezi kutolewa maeneo yote kwa malisho na kama suala hilo ni tatizo kuna taratibu za kufuatwa ili wapatiwe maeneo hayo badala ya kuvamia maeneo yasiyokuwa yao.

“Maelekezo yangu kwenu, naomba tutambue Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya Serikali ya Kijiji na yako chini ya kijiji na kijiji kikiamua kuyauza au kuyatoa wanafuata utaratibu, yamo ya uhifadhi hayako katika Serikali ya Kijiji,” alisema na kuongeza:

“Mnapogoma maeneo yasionyeshwe mnakwenda kinyume na sheria, mtakapotoa alama za mipaka zilizowekwa kwa ajili ya upimaji mnavunja sheria na mimi niko hapa kusimamia sheria, tusipimane, msinipime ubavu kugomea amri halali ya Serikali.

“Kama hamtaki kupokea maelekezo ya Serikali, mkatafute Serikali nyingine au maeneo mengine ambayo Serikali haitoi maelekezo, mnajua Serikali ipo na ikitoa maelekezo mnagomea wakati tunaongozwa na kanuni, taratibu na sheria. Lengo la mkutano huu ni kupatikana kwa haki kwa pande zote mbili.”

 

BATILDA

Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Batilda, alisema eneo hilo alilinunua mwaka 2012 kutoka kwa wamiliki wa awali kwa lengo la kuwekeza kwa ajili ya uhifadhi.

Alisema alichukua mkopo benki kununua eneo hilo huku akiweka nyumba yake rehani na anashindwa kulipa deni kutokana na wananchi hao kumzuia kuwekeza.

“Nimenunua hii ardhi mwaka 2012, nimechukua mkopo benki, nimeweka nyumba yangu ili niweze kununua hili eneo na kuliendeleza kwa maana ya uhifadhi na kuhakikisha kunakuwa na ‘tented camps’ na kuleta watalii kijijini, halmashari ipate mapato, kijiji mpate mapato na nyie mnufaike.

“Tusemeni ukweli, tumwogope Mungu, chuki yote hii ni mfumo dume kwa sababu Wamasai mwanamke hamiliki ardhi, nimeona kila mahali kwa wajomba zangu, mamangu huyu hapa amerushwa ardhi ya babake. Sasa mimi nimetoa fedha zangu, nyumba yangu inataka kupigwa mnada kwa sababu ya eneo hili mnalotaka kuninyang’anya kwa kutumia mabavu, nimeleta wawekezaji wenzagu ambao tutashirikiana, kila wanapokuja wanafukuzwa.

“Serikali inanidai kwanini hufanyi uwekezaji, nashindwa kufanya uwekezaji kwa sababu kila tunapokuja hapa vijana wanahamasishwa kufanya vurugu na kufukuza watu, kumewekwa bikoni vijana wamezing’oa, sasa maendeleo hayawezi kwenda kwa sababu ya kufanya mabavu, kwa sababu leo hii hati ipo, ama mnapenda au hampendi hati hii hapa ipo, Serikali inatambua kuna ardhi yenye hati,” alisema.

 

MWENYEKITI

Awali Saruni alisema licha ya kuwa kiongozi wa kijiji hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 2014, lakini hajui ukubwa wa eneo lake bali anatambua mipaka ya wilaya inayokizunguka.

Alisema walidhani eneo lote lililopo kijijini hapo ni mali ya kijiji, hivyo hawakujua kuna eneo la mwekezaji ambalo halipo chini ya Serikali ya Kijiji na kumwomba Muro kushirikiana na wataalamu wengine ili kutoa elimu zaidi kwa wananchi hao.

Saruni alisema mwaka jana baada ya Dk. Batilda kutaka kuanza kuwekeza katika eneo hilo, ndipo mgogoro kati yake na wananchi ulipoanza na baada ya jitihada za kujaribu kuutatua kushindikana, alilazimika kuandika barua kwa Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini kuomba wasaidiwe.

“Nimefurahi kuona Serikali imekuja tena kujadiliana na wananchi ili kumaliza mgogoro, barua iliyotuelekeza tufanye uchaguzi wa kijiji haikutueleza kuna eneo la mwekezaji, tulikuwa tunajua ardhi yote ni ya kijiji chetu, sasa ndiyo tunajua kuna sehemu sio ya kwetu, sasa ni jukumu la Serikali kuwaelewesha watu vizuri ili waelewe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles