24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mzee Kwanza kuboresha huduma kwa wazee

pichaNa Ramadhan Libenanga, Morogoro

TANZANIA inakadiriwa kuwa na wazee 2,507,568 ambao ni sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania wote kwa mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2012.

Kundi hili la wazee limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha huku wengi wakiwa ni wastaafu baada ya kulitumikia Taifa katika nyanja mbalimbali.

Ni wazi kuwa yapo mafanikio mengi nchini ambayo kwa kiasi kikubwa yameletwa na wazee wakati wakilitumikia Taifa katika sekta mbalimbali.

Takwimu zinaonesha kuwa pamoja na kwamba wazee wengi wana umri kati ya miaka 60 na 70 lakini pia kuna wazee takribani 474,053 wenye umri wa miaka 80.

Aidha tathmini zinaonesha kundi la wazee wenye umri kati ya miaka 60-64 ni asilimia 31 wakati wenye miaka 60-69 ni asilimia 20 na wenye miaka 70-74 ni asilimia 19.

Wazee wenye miaka 70-79 ni asilimia12 wakati wazee wenye miaka zaidi ya 80 ni asilimia 19.

Hata hivyo tathimini ya kimkoa inaonesha kuwa mikoa inayoongoza kuwa na wazee wengi ni Kilimanjaro asilimia 6.4, Mbeya asilimia 6.1, Dar es Salaam asilimia 6.1, Morogoro asilimia 5.6, Tanga asilimia 5.6, Dodoma asilimia 5.6, Kagera asilimia 5 na Mwanza asilimia 4.9.

Ni wazi jamii inafahamu kwamba umri unavyozidi kuongezeka ndivyo changamoto kwa wazee zinavyozidi kuongezeka kutokana na kutokuwa na nguvu za kufanya kazi.

Hivyo wengi hujikuta wakikabiliwa na changamoto ya kipato, ongezeko la mahitaji ya huduma za afya na nyingine.

Kipindi hiki ndiyo magonjwa mengi hujitokeza kutokana na mwili kuchoka.

Mbali na afya wazee wanahitaji malazi, chakula na huduma mbalimbali za kijamii ambazo kimsingi zote zinahitaji fedha ili kupata huduma bora na salama.

Kundi kubwa la wazee limekuwa likilalamikia kutokuwepo kwa haki na ustawi wa wazee wakati wa kupata mahitaji mbalimbali katika jamii.

Athuman Ramadhan (70) mkazi wa Manispaa ya Morogoro Kata ya Sultan, anasema changamoto za wazee ni nyingi hali inayosababisha wengine kukata tamaa.

“Kauli ya serikali ya kusema wazee wanatibiwa bure si kweli ni uongo tu wa kwenye majukwaa ya kisiasa, tuna shida sana kiasi cha kuona kama uzee ni  kilema wakati kila mtu utamfika,” anasema Ramadhan kwa masikitiko.

Anasema changamoto nyingine ni lugha chafu kwa watoa huduma hasa sekta ya afya na wanapokwenda kulipia ankara mbalimbali.

“Tumekuwa hatuthaminiwi kama sera inavyoeleza na matokeo yake jamii imejenga dhana ya kudharau wazee kwa kuona muda wao umekwisha na badala yake kusubiri kufa tu,” anasema.

Aidha anasema katika hospitali, zahanati na vituo vya afya wazee wamekuwa wakisaidiwa daftari tu lakini huduma  nyingine zote wamekuwa wakilipia hali ambayo bado ni tatizo kwao.

Hata hivyo wazee hao wameiomba serikali kuweka daktari maalumu katika kila kituo kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya wazee wanapofika katka maeneo hayo.

Kwa kutambua changamoto hizo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeanzisha kampeni maalumu ijukanayo kama ‘Mzee Kwanza’ ambayo inalenga kuhakikisha wazee wanapata huduma stahiki hasa za matibabu.

Akizindua kampeni hiyo hivi karibuni mkoani hapa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema serikali imeandaa muswada wa sheria ya wazee ambapo utapelekwa bungeni ili upitishwe kuwa sheria itakayosimamia upatikanaji wa haki na ustawi wa wazee nchini.

Anasema sheria hiyo itatoa ahueni kubwa kwa wazee na kuboresha sana maisha yao ambapo amesema kuwa mwezi wa tisa wamepanga kuufikisha rasmi bungeni kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Waziri huyo anasema takwimu zinaonyesha jumla ya wazee wanaopata huduma ya pensheni na NHIF ni sawa na asilimia 4 tu ya wazee wote nchini huku bima ya afya ikihudumia wazee 52,000 tu.

“Hatua kubwa ambayo serikali imeshachukua mpaka sasa ni kuagiza kila halmashauri nchini kubaini wazee walio katika maeneo yao na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi kutoka kwenye mapato yao ya ndani,” anasema Ummy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles