22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Utaratibu mpya wa matibabu utakavyowaathiri wagonjwa wa siko seli

1*Wadau wadai utakwamisha vita dhidi ya ugonjwa huo nchini

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

KITENGO cha wagonjwa wa selimundu (Sickle cell) kilichopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kimekuwa kikihudumia takribani wagonjwa 6,000 kwa mwaka tangu kilipoanzishwa mwaka 2004.

Kwa kipindi chote cha takribani miaka 10 sasa kitengo hicho kimekuwa kikitoa huduma ya matibabu bure kwa wagonjwa hao, hata hivyo huduma hiyo hivi sasa imesitishwa.

April 21, mwaka huu MTANZANIA ilitembelea katika kitengo hicho na kukuta wazazi wapatao 50 waliokuwa wameambatana na watoto wao kwa ajili ya kufanyiwa vipimo hospitali hapo.

Ilishuhudia wazazi hao wakiwa wamepanga foleni ya kwenda kulipia Sh 4,500 waliyoelekezwa na wauguzi kuwa ni kwa ajili ya kupata kipimo cha damu.

Hata hivyo katika eneo hili wanaonekana pia wazazi wengine wakiwa wamekaa pembezoni, wakiwa wanatafakari jambo huku wakiwa na nyuso zilizokata tamaa.

Wengine wanaonekana wakiwa katika mjadala wakijadili juu ya uamuzi huo wa Muhimbili, naamua kuwasogelea na kusikiliza kwa karibu majadiliano yao.

Wazazi  

“Mimi naona bora tu niende na mwanangu nitakuja Alhamisi ijayo nikiwa nimejiandaa na fedha ya kulipia kipimo cha damu,” anasema Mwamvua Ally.

Wazazi hawa wanalalamika juu ya mabadiliko ya ghafla katika kitengo hicho, kwamba wameweka utaratibu wa kulipia huduma bila ya kuwajulisha jambo hilo.

Grace Kabera, mkazi wa Makongo, Dar es Salaam anasema alipewa taarifa hizo mara baada ya kufika hospitalini hapo hali ambayo imemshtua.

“Jamani hali hii imeanza lini? mbona hawakutuambia? Namba zetu za simu walizichukua za nini? Hawajatuma japo ujumbe mfupi wa maandishi kutujulisha mabadiliko haya. Tunatakiwa kulipia huduma na bado dawa ni ghali, hali ya maisha ni ngumu, sijui kama tutaweza kumudu gharama hizi.

“Unajua mtoto anayeugua ugonjwa huu anahitaji ungalizi wa karibu maana mara nyingi huwa ni rahisi kuugua sasa hata kliniki tunatakiwa kulipia na bado dawa zake ni ghali, jinsi hali ya maisha ya sasa ilivyo ngumu unadhani tutaweza kumudu gharama hizo,” anahoji Grace.

Paskalia Semfukwe naye ni mmoja wa wazazi anasema mabadiliko hayo yamemkatisha tamaa mtoto wake kuendelea na matibabu.

Mkami Kitigwa, mkazi wa Temeke anasema “Niliambiwa niende Amana lakini kila nikienda mwanangu anapewa dawa za kutuliza maumivu pekee, hivyo nikawa nakuja huku kwa ajili ya kliniki lakini leo (jana) naambiwa huduma ya bure imesitishwa tunatakiwa kulipia.

Getruda Thadeus mkazi wa Tabora, anasema tangu mwaka 2001 mtoto wake amekuwa akipata huduma hiyo na kwamba alifunga safari kuja klikini na kukuta mabadiliko hayo.

“Nimetoka Tabora, mwanangu ana umri wa miaka 13, tangu 2001 amekuwa akitibiwa bure sikujiandaa kwa fedha za matibabu. Nimefika hapa naambiwa natakiwa kulipia huduma, sina jinsi itabidi nirudi nyumbani nikajipange upya.

Mzazi mwingine anasema mwanawe baada ya kufanyiwa vipimo madaktari walibaini kuwa alikuwa ameishiwa damu na kulazwa hospitalini hapo siku tatu ambapo alitozwa Sh  Sh 70,000.

Daktari

Mmoja wa madaktari wa kitengo hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji, anasema gharama ya kutibu mtoto mmoja ni wastani wa Sh 50,000.

“Wameambiwa walipie kipimo cha damu hiyo Sh 4,500 bado wakitoka huko lazima wamuonea daktari na utaratibu huwa ni Sh 11,000, hivyo ili mtoto atibiwe mzazi atahitaji kuwa na angalau kuanzia Sh 50,000 na kuendelea,” anasema.

Mkuu wa kitengo

Profesa Julia Makani ndiye Mkuu wa Kitengo hicho cha sickle cell katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, anasema utaratibu wa kuwatibu bure wagonjwa hao umebadilika kwa kuwa mradi uliokuwa ukiwapatia ufadhili umekwisha muda wake tangu Machi 31, mwaka huu.

“Wagonjwa wa sickcell walikuwa wakipatiwa matibabu bure baada ya MUHAS kupata ufadhili mwaka 2004 kupitia shirika lijulikanalo Welcome Trust la Uingereza ambalo lenyewe huwa linafadhili masuala ya utafiti.

“Tuliandika dokezo letu lililokuwa na mambo manne ambapo tulisema tunahitaji kufanya utafiti, kutoa huduma, mafunzo kwa madaktari, watafiti na wagonjwa pamoja na kuhamasisha jamii kwa ujumla juu ya ugonjwa huu,” anasema Profesa Makani.

Anasema kitengo hicho kimefanya kazi ya kutoa huduma bure chini ya ufadhili huo kwa miaka 10 hadi Machi 31, mwaka huu ambapo mradi huo ulifikia tamati.

Anasema katika miaka yote 10 wamekuwa wakitoa matibabu bure kwa wagonjwa, kuwalipa madaktari waliokuwa wakiwatibu wagonjwa hao pamoja na kulipia jengo wanalotumia kupitia fedha za mradi huo.

“Lakini nilipoona mradi unakwisha, Novemba mwaka jana niliwaandikia barua Muhimbili kuwajulisha na kuwaeleza kuwa sasa inabidi wachukue hatua ya kuwahudumia wagonjwa hawa ambao hadi sasa wamefikia 6,000,” anasema.

Profesa Makani ambaye pia ni mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), anasema wakati wakiwa wanaendelea na mazungumzo na Muhimbili juu ya namna watakavyoanza kuwahudumia wagonjwa hao hatimaye muda wa mradi huo ulikwisha rasmi.

“Mradi umekwisha huku hospitali ikiwa bado haijajiandaa kuzipokea na kuzisimamia huduma ambazo mradi ulikuwa unazigharamia ikiwamo kulipia vipimo vya wagonjwa na mishahara ya madaktari,” anasema.

Anasema pamoja na changamoto hiyo, pia wazazi wa wagonjwa hao ambao wamepata taarifa ya mabadiliko hayo wapo ambao wameacha kufika kwenye kliniki hiyo wakijua hakuna huduma kabisa jambo ambalo si kweli.

“Baadhi ya wazazi waliposikia kwamba mradi umekwisha walijua huduma zimekwisha, hii si kweli huduma zinaendelea isipokuwa sasa wanatakiwa kulipia gharama,” anasema.

Anasema hivi sasa wanaandaa utaratibu wa kuwajulisha waanze kujiandaa kuwapokea wagonjwa hao kwenye hospitali zao na kwamba mkakati huo utafanyika haraka kabla ya Juni, mwaka huu.

“Bado nina imani na serikali watalifuatilia suala hili na kulitafutia ufumbuzi, najua wanaweza ‘kuli-handle’ kama ilivyo kwa magonjwa mengine hivyo watatafuta ufumbuzi wa haraka,” anasema Profesa Makani.

Hali ya ugonjwa nchini

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka jana, Tanzania inashika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa sickle cell.

Inakadiriwa kwamba takriban watoto 10,000 hadi 12,000 huzaliwa wakiwa na ugonjwa huo kila mwaka nchini wakati kidunia watoto 300,000 huzaliwa na ugonjwa huo.

Mwanaharakati

Yasmini Razak ni mwanaharakati wa ugonjwa huo ambaye anaishi Uingereza, anasema ni vyema serikali ikafumbua macho na kulitazama suala hilo kwa jicho la tatu.

“Nina mtoto mwenye sickle cell, nafahamu jinsi watoto hawa wanavyohitaji uangalizi maalumu, nimesikitishwa na hatua ya Muhimbili kusitisha huduma ya bure ya matibabu haya,” anasema Yasmini.

Anaishauri serikali isitishe kuwapa rufaa wagonjwa hao kwenda kwenye hospitali za pembezoni hadi itakapoimarisha kliniki zake.

“Lakini najiuliza kwanini watoto hawa walipie gharama ikiwa wagonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na mengine wanatibiwa bure na serikali, hawa walazimika kutumia dawa siku zote za maisha yao,” anasema.

Muhimbili

Kaimu Mkurugenzi wa (MNH), Profesa Lawrence Museru, anasema hospitali imelazimika kuwaingiza wagonjwa hao katika mfumo wa kawaida wa malipo baada ya mradi huo kuisha.

“Si kweli kwamba hospitali imesitisha huduma hii bali mradi uliokuwa ukiwahudumia umekwisha, kwa hiyo tumewaingiza wagonjwa waliokuwa wakitibiwa bure katika mfumo wa malipo na hii ni kwa mujibu wa taratibu za hospitali,” anasema Profesa Museru.

Museru anakiri kwamba walikosea kuwataarifu mapema wazazi hao na kusisitizwa kuwa ingawa wanawahamisha wagonjwa katika hospitali nyingine bado wataendelea kuwahudumia watakaokuwa na mahitaji ya huduma za ziada.

“Kwa mfano wale watakaohitaji kuongezewa damu, wenye ugonjwa wa kiharusi na ambao wanahitaji dawa maalumu hawa tutabaki nao. Na ikiwa mtu anashindwa kulipia gharama za matibabu atalazimika kwenda kuonana na maofisa ustawi wa jamii… watamsikiliza na kumpa barua maalumu kwa ajili ya kutibiwa.

Jamii inapaswa kufahamu kuwa zipo baadhi ya huduma hapa Muhimbili ambazo ni lazima walipie ili kuchangia uendeshaji kama vipimo vya MRI kwa sababu ni ghali,” alisema.

Akifafanua sababu za muhimbili kutoza Dola 2,000 za Marekani kwa jengo walilokuwa wakilitumia wakati mradi huo uliendeshwa kwa msaada wa wafadhili, anasema waliwalipisha kwa kuwa nafasi hiyo ilikuwa ni maalumu kwa idara ya damu hospitalini hapo.

“Kwa kawaida ukiandika mradi unataja ‘cost’ zote ambazo utagharamia ndio maana wale watafiti walilipwa, kwa hiyo huwezi kusema kwanini walilipa jengo ni kwa sababu baadhi ya huduma zilisimama,” anasema.

Mganga Mkuu wa Mkoa

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Grace Maghembe, anasema hospitali zote za mkoa huo zina wataalamu wa kutosha wa kuwahudumia watoto hao.

“Tumewapokea kama wagonjwa wa rufaa wa kawaida na tuna wataalamu wa kutosha kuwahudumia isipokuwa wale watakaokuwa na matatizo tutalazimika kuwarudisha Muhimbili kwa matibabu zaidi,” anasema Dk. Maghembe.

Wizara

Gazeti hili pia lilitaka kupata ufafanuzi kuhusu watoto walio na umri wa miaka mitano nao kulipishwa gharama huku sera ikisema wanatakiwa kulipiwa na serikali.

Mkurugenzi Msadizi wa Huduma za Hospitali katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, anasema mwongozo uliopo wizarani unaelekeza kuwa wagonjwa wenye matatizo sugu wanapaswa kulipia wakiwamo wa sickle cell.

“Watu wamezoea kwamba watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wazee kuanzia miaka 60 hawagharamii matibabu, lakini wizara ina mwongozo ambao unayataja makundi ya magonjwa sugu ambayo yanapaswa kulipiwa ikiwamo ugonjwa wa sickle cell,” anasema Dk. Gwajima.

Anasema mradi huo ulilenga kujua Tanzania kuna wagonjwa wangapi wa sickle cell hivyo wanasubiri matokeo ya utafiti huo ili waweze kutunga sera na miongozo ya matibabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles