29.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU: ALICHOFANYIWA LISSU KINAUDHI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema kitendo alichofanyiwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kinaudhi na watawasaka wahusika kwa nguvu zote.

Hii ni kauli ya kwanza ya Mwigulu tangu kushambuliwa kwa Lissu Septemba 7, mwaka huu akiwa anatokea kwenye kikao cha asubuhi cha Bunge mjini Dodoma.

Mwigulu alitoa kauli hiyo jana, alipoulizwa na MTANZANIA sababu ya Serikali kutokubali kuruhusu vyombo vya uchunguzi kutoka nje vije kuchunguza shambulio hilo la Lissu kama ambavyo Chadema na familia ya mbunge huyo wameomba.

“Kazi ya uchunguzi inaendelea ikihusisha tukio hilo na matukio mengine, mtaendelea kujulishwa punde pakiwepo na hatua ya kuwajulisha.

“Nikuhakikishie tu kuwa jambo hilo ni la kuudhi sana, hivyo vyombo vinafanya kazi kwa nguvu zote kupata undani na kuwatafuta wahusika,” alisema Mwigulu.

Gazeti hili lilizungumza na Mwigulu, baada ya mkutano wake aliofanya juzi katika Kata ya Kinampanda Wilaya ya Iramba mkoani Singida, ambako pamoja na mambo mengine, aligusia uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa Lissu.

 

UCHUNGUZI KUFANYWA NA WATANZANIA

Akizungumza na wananchi katika mkutano huo, Mwigulu alisema uchunguzi wa tukio hilo utafanywa na vyombo vya dola vya hapa nchini.

“Nchi hii ni huru, inajitegemea, wanaofanya uhalifu Tanzania, upelelezi utafanywa na vyombo vyetu na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria vya hapa hapa.

“Tunatakiwa tuamini vyombo vyetu, hata ukimtoa mtu mbali, bado atatakiwa aulize watu wa hapa, niwahakikishie tutashughulika nao kweli na tumeshaanza.

“Uchunguzi huwa hauna ukomo kwa sababu unaisha tu pale ukishawapata wote waliofanya uhalifu. Marekani ilimtafuta Osama kwa muda mrefu sana, si kwamba hatufanyi uchunguzi,” alisema Mwigulu.

Aliwataka Watanzania kuviamini vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoendelea kuchunguza tukio hilo na mengine yanayofanywa na watu wasiojulikana.

Pia aliwatahadharisha wale wanaojiandaa kusababisha matatizo kwa watu, kuwa wamechagua vita ambayo wameshindwa kabla hawajaanza.

“Kasumba ya kushambulia watu na kubeba jina la watu wasiojulikana, wamemshambulia Lissu, mwanajeshi mstaafu, hakimu pale Lindi, sasa wanaofanya uhalifu wa aina hiyo dakika zao zinahesabika,” alisema.

Mwigulu alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kufika katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, mara baada ya tukio la Lissu kupigwa risasi.

Kutokana na kile kinachoelezwa ni mshtuko wa tukio hilo, waziri huyo mwenye dhamana ya ulinzi wa raia na mali zao, alifika hospitalini hapo kwa teksi, huku akiacha gari lake bungeni.

Mwigulu ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi mkoani Singida, akiwa na wabunge wengine na viongozi wa Bunge, alikaa uwanja wa ndege wa Dodoma hadi ndege iliyombeba Lissu kumpeleka Nairobi nchini Kenya ilipoondoka.

 

MAALIM SEIF, DUNI WAMJULIA HALI LISSU

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji, wamekwenda katika Hospitali ya Nairobi kumjulia hali Lissu.

Mkuu wa Idara ya Uenezi Chadema aliyeko katika hospitali hiyo, Hemed Ali, alisema viongozi hao waliwasili hospitalini hapo jana.

Mbali na viongozi hao wa CUF na wabunge wa Chadema, baadhi ya wanasiasa waliofika kwenye Hospitali ya Nairobi kumjulia hali Lissu, ni pamoja na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa.

 

LISSU ALIVYOSHAMBULIWA

Lissu alipigwa risasi Septemba 7, mwaka huu, alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge.

Baada ya shambulio hilo, alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi anakoendelea kutibiwa.

Viongozi wa Chadema waliamua kumpeleka Nairobi kwa kile walichoeleza kuwa usalama wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles