24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

TANESCO YADAIWA BIL. 860/- ZA UMEME

Na PATRICIA KIMELEMETA – dar es salaam


SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), linadaiwa zaidi ya Sh bilioni 863.48, zikiwa ni malimbikizo ya madeni kutoka kwa kampuni mbalimbali zinazozalisha umeme na kuwauzia.

Hayo yalisemwa jana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Nje wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Johanes Kisiri.

Mkaguzi huyo alisema taarifa hizo zinatokana na taarifa ya ofisi ya CAG ya mwaka 2015/16.

Kisiri alisema deni hilo limesababishwa na Tanesco kununua umeme kwa bei kubwa kutoka kwa wazalishaji umeme binafsi, huku likiuuza kwa gharama ndogo kwa wateja wake.

Alisema Tanesco inanunua umeme kwa Sh 544.65 kwa kila uniti na kuuzia wateja wake uniti moja kwa wastani wa Sh 265.30 hali iliyosababisha kujiendesha kwa hasara.

“Ripoti yetu inaonyesha kuwa Tanesco wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 863 zilizotokana na malimbikizo ya deni kutoka kwa makampuni ya wazalishaji huru wa umeme na wale wazalishaji wa dharura, hali iliyosababisha deni kuongezeka,” alisema Kisiri.

Aliongeza kutokana na hali hiyo, ofisi ya CAG imeishauri Serikali kumalizia mradi wa maji ya korongo la Stiegler ambao ulikuwa unasimamiwa na Mamlaka ya Bonde la Rufiji (Rubada).

Alisema mrafi huo unajengwa kwa gharama ya Dola za Marekani  bilioni 2.4  na ukikamilika utaweza kuzalisha megawati za umeme 2,100.

“Mradi huu ulipangwa kutekelezwa katika vipindi vya awamu tatu, ambapo awamu ya kwaza ungezalisha megawati 300, ya pili 600 na awamu ya mwisho ni megawati 300 ambayo ingekamilika mwaka 2028,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, CAG alishauri Serikali kuwa miradi mikubwa ya kuzalisha umeme kama hiyo ingepewa taasisi zenye fedha ili iweze kukamilika kwa wakati, hali ambayo ingesaidia kupunguza gharama ambazo Tanesco wanatumia kulipa makampuni yanayowauzia umeme.

“Lakini pia Serikali iziwezeshe taasisi husika kupata fedha za kuendeleza mradi huo, ambao utatoa nishati ya gharama nafuu ikilinganishwa na umeme unaozalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta,” alisema.

 

FEDHA INAZODAI TANESCO KWA WATEJA WAKE

Wakati Tanesco ikidaiwa fedha hizo na kampuni mbalimbali, zikiwamo Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Symbion Power na Aggreko, Machi 9, mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk. Tito Mwinuka, alisema wanawadai wateja wao nchi nzima Sh bilioni 275.38.

Alisema wizara na taasisi za Serikali zinadaiwa zaidi ya Sh bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), linadaiwa zaidi ya Sh  bilioni 127.87 na makampuni binafsi na wateja wadogo wadogo zaidi ya Sh bilioni 94.97.

Tanesco ilitoa taarifa (notice) kwa wadaiwa wote kulipa madeni yao ndani ya kipindi cha siku 14, baada ya hapo hatua ya kusitisha huduma kwa wateja watakaoshindwa kuanza kulipa madeni yao pamoja na hatua zingine za kisheria zitachukuluiwa.

Mara kadhaa tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, Tanesco imekuwa ikitangaza kukusanya kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwenye taasisi mbalimbali zikiwamo za Serikali na Serikali ya Zanzibar.

 

TANZANITE INAVYOPIGWA

Jana Kisiri akizungumzia ukaguzi wa madini, alisema Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) iliingia ubia na Kampuni ya Tanzanite One Tanzania Limited (TML) kuchimba madini ya tanzanite yaliyopo Mirerani mkoani Manyara.

Alisema hata hivyo, TML imekuwa ikiiuzia madini hayo Kampuni ya Sky Associates bila ya kuishirikisha Stamico.

“Kampuni ya TML na Sky Associate ni ndugu, lakini wamekuwa wakiuziana madini ya tanzanite bila ya kuishirikisha Stamico, hali iliyosababisha kujitokeza kwa walakini,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, CAG aliishauri Serikali mauzo ya madini hayo kufanyika kwa uwazi kupitia minada ya hadhara, ambayo itaondoa mianya ya kuuzwa kwa bei isiyo halali ya ushindani sokoni.

“Ukienda kwenye masoko ya kimataifa, bei ya madini hayo ipo juu, lakini kitendo cha kuuziana wenyewe kwa wenyewe kinasababisha kujitokeza kwa ujanja ujanja,” alisema.

 

MAMLAKA YA BANDARI

Kisiri alisema Serikali iliagiza kufanyika kwa ukaguzi maalumu katika Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam (TPA) ambako walibaini kuwa zaidi ya Sh bilioni 15.02 za ushuru wa bandari (wharfage) hazijakusanywa.

Alisema kitendo hicho kimefanywa na baadhi ya watendaji wasio waadilifu ambao wamekuwa wakishirikiana na kampuni zinazotoa mizigo bandarini na wafanyakazi wa benki ili kufanikisha mpango huo.

Kisiri alisema kutokana na hali hiyo, waliishauri Serikali kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na benki husika ili waweze kurudisha fedha hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles