25.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi Simiyu ajeruhiwa na fisi akielekea shule

Na Derick Milton, Simiyu

Mwanafunzi wa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi Somanda “A” iliyoko Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Hollo Malugu (14) amejeruhiwa kichwani baada ya kung’atwa na fisi wakati akielekea shuleni.

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi Machi 10, saa 1 Asubuhi wakati mtoto huyo akielekea shuleni, ambapo akiwa barabarani ghafla fisi huyo alitokea katika Milima iliyoko kwenye maeneo hayo na kuanza kumshambulia.

Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Dk. Judith Ringia akiongea na Waandishi wa Habari amedhibitisha kupokelewa kwa mtoto huyo katika hospitali ya halmashauri kwa ajili ya matibabu.

Dk. Ringia amesema kuwa mtoto huyo amejeruhiwa vibaya maeneo ya kichwani ambapo fisi alimng’ata na kunyofoa nyama huku akibainisha madaktari na wahudumu walifanya jitihada za haraka kumpatia huduma ya kwanza.

“Ni kweli mtoto aliletwa hapa na hali mbaya na ameng’atwa kichwani na kunyofolewa baadhi ya nyama, alipofikishwa hapa hospitali tulimpatia huduma ya kwanza, lakini imeonekana hali yake kuwa mbaya tumempatia rufaa na atapelekwe Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema Dk. Ringia.

Mama Mazazi wa mtoto huyo amesema kuwa katika mtaa wao kumekuwepo na fisi wengi ambao wanaotokea kwenye pori la Magereza la mjini Bariadi, nakwamba mtoto wake alivamiwa wakati akielekea shuleni.

“Wakati anaenda shule, njiani ndipo akavamiwa na akaanza kupiga kelele, ndipo wananchi ambao nao walikuwa njiani wakajitokea na kumuokoa, lakini tayari alikuwa amemjeruhi sana kichwani, ndipo nami nikamkuta akiwa na hali mbaya damu zikimwagika,” amesema Mwasi Sumbuka.

Upande wake mwananchi aliyemuokoa mtoto huyo, Mahega Mpango aliyemwokoa Mwanafunzi huyo amesema kuwa bila yeye mtoto huyo angelipoteza maisha kwani fisi alikuwa amemkandamiza chini huku mtoto huyo akipiga kelele.

“Baada ya kusikia kelele nikakimbia kumuokoa mtoto, ndipo nikakuta fisi akiwa amemkandamiza mtoto chini huku akimg’ata kichwani, nikachukua mawe na kuanza kumpiga ndipo akakimbia,” amesema Mpango.

Baada ya tukio hilo, wananchi wa mtaa huo walichukua uamuzi wa kuanza kumfukuza fisi huyo, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda kutokana na mnyama huyo kuwakimbia na kutokomea katika msitu wa Magereza.

Aidha, wananchi hao wameitaka Serikali kupitia mamlaka ya wanyamapori chini, kuwasaidia kwa kufanya msako mkali wa kuwafukuza fisi hao, kwani mtaa wao kutokana na kuwa na milima mingi kuna fisi wengi.

“Tunaomba msaada wa serikali, mtaa wetu una fisi wengi sana, ikifika saa kumi na mbili wanaanza kuja kwenye maeneo yetu wanatoka milimani au asubuhi ni hatari hasa kwa watoto wetu maana wanakuwa wanakwenda kwenye milima,” amesema Emmanuel Magige.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles