25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi kidato cha nne afariki kwa kukosa hewa akibakisha mtihani mmoja

NYEMO MALECELA-Kagera

MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mwemage, iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Paficitus Tumwesige, amefariki dunia baada ya kukosa hewa kutokana na kufunga milango huku akiwa amewasha jiko la mkaa ndani ya nyumba aliyokuwa amelala.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwemage, Lenard Ndyakoa, alisema kifo cha mwanafunzi huyo kilitokea usiku wa kuamkia Novemba 9, mwaka huu nyumbani kwao.

Mwalimu Ndyakoa alisema baada ya wataalamu wa afya kuupima mwili wa mwanafunzi huyo, ilionekana kifo chake kilitokana na kukosa hewa kwa sababu alifunga milango na madirisha wakati akiwa na jiko la mkaa ndani jambo lililosababisha kukosa hewa.

Alisema mwanafunzi huyo alikutwa amelala pembeni mwa jiko hilo la mkaa.

“Marehemu alikuwa amemaliza mitihani ya masomo saba na alikuwa amebakiza somo moja la bailojia 2 ambalo lingefanyika Novemba 12, mwaka huu.

“Mazishi yake yalifanyika Jumapili baada ya kuthibitishwa kuwa kifo chake hakina utata,” alisema mwalimu Ndyakoa.

Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na mama yake ambaye anafanya kazi katika Kituo cha Afya cha Mwemage kilichopo kwenye halmashauri hiyo na pia wana makazi mengine Kijiji cha Kibena ambako pia wapo watoto wake wengine wadogo.

Siku ya tukio mama huyo alikuwa amemwacha katika nyumba iliyoko karibu na kituo anachofanyia kazi, yeye akaenda kulala kijijini ili kuwaona watoto wake wengine.

“Hivyo wakati mauti yanamkuta mama yake hakuwepo. Aliacha amemwagiza apike chakula chake na usiku aamke asome kujiandaa na mtihani,” alisema.

Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Deo Chacha alisema tukio hilo ni la kusikitisha ukizingatia mwanafunzi huyo alikuwa amebakiza mitihani michache.

“Pia msiba huo ulisababisha mshutuko kwa wanafunzi aliokuwa anasoma nao, lakini kwa kuwa ulitokea maeneo ya nyumbani basi walisikitika sana, lakini waliendelea na mitihani iliyokuwa imebaki,” alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, alisema tukio hilo liliripotiwa kwao na ilithibitishwa kuwa kifo chake kilitokana na kukosa hewa ya oksijeni kutokana na kufunga milango wakati akiwa na jiko la mkaa ndani alilokuwa akilitumia kupikia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles