CHRISTOPHER MSEKENA
HUWEZI kumkwepa Ommy Dimpoz kwa sasa kwani ndiye msanii anayetamba katika chati za muziki kupitia wimbo wake Ni Wewe aliouachia hivi ukaribuni.
Dimpoz, amekuwa gumzo baada ya ngoma hiyo kutoka na mashabiki kunukuu moja ya kauli aliyozowahi kutoa mwigizaji, Steve Nyerere kwamba msanii huyo hatoweza kuimba tena kwani upasuaji umeathiri sauti yake.
ILIKUWAJE STEVE AKASEMA HIVYO?
Mara baada ya kufanya upasuaji wa kwanza Ommy Dimpoz alipoteza sauti. Katika mahojiano aliyofanya na vyombo mbalimbali vya habari, alikuwa anazungumza kwa sauti ndogo inayofanana na mtoto ndiyo maana Steve Nyerere akapata nguvu ya kusema Dimpoz hataimba tena.
STEVE NYERERE AJITETEA
Baada ya kuwa gumzo na kuonekana mtu ambaye hamtakii mema Ommy Dimpoz kipindi anaumwa, Steve Nyerere ameliambnia Swaggaz kuwa:“ Hata kocha kwenye mpira mchezaji anapoteguka mguu huwa anasema mchezaji huyu hatacheza kwa muda fulani lakini akipona atarudi tena uwanjani, mimi sikusema Ommy hataimba milele, nilisema Ommy atachukua muda sana kurudi kwenye kazi yake mpaka apone, mimi siyo msaidizi wa Mungu, tusipende kugombanisha watu.”.
DIMPOZ AMSAMEHE
“Hatujaonana na Steve lakini nashukuru Mungu kama ameweza hata kuposti wimbo wangu kwenye ukurasa wake wa Instagram ni kitu kizuri, ni kaka yangu, kibinadamu pengine hayo yaliyotokea tuyaache maisha yaendelee,” anasema Ommy Dimpoz.
MUUJIZA WA MAJI
Ommy Dimpoz anasema baada ya kupoteza sauti kwa muda kutokana na upasuaji wa kwanza uliofanyika Afrika Kusini, siku moja alishtukia sauti yake imerudi jambo ambalo yeye na bibi yake hawakutarajia.
“Sauti ilianza kurudi kabla sijakwenda kwenye upasuaji mwingine Ujerumani, nimejifunza katika kuumwa imani ni kitu muhimu sana, bibi yangu alinipigia simu akinijulia hali, akawa ananionea huruma ninavyoongea kwa tabu,
“Akaniambia ikifika muda fulani wa jioni kwa imani yangu, kaa mwombe Mungu akuondolee hilo tatizo, chukua hata maji yaombee harafu kunywa, nikamsikiliza nikafanya kama alivyoniambia, nilivyoamka asubuhi, akanipigia simu kunijulia hali, ile nasema haloo, nikakuta sauti imetoka kama kawaida hata mwenyewe najishangaa,” anasema Dimpoz.
YOGO BEATZ ASILIMUA WALIVYO REKODI
Mtayarishaji wa muziki Bongo, Yogo Beats kutoka studio za TNT Productions ambaye amehusika kutengeneza audio ya wimbo Ni Wewe, Ommy Dimpoz, akiwa bado kwenye mapumziko nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mwaka jana.
Akizungumza na Swaggaz Yogo Beats alisema: “Changamoto ilikuwepo kutokana na hali yake ilivyokuwa aliporejea nchini kutoka Afrika Kusini kwenye upasuaji wake wa kwanza, alirudi akiwa na sauti ndogo sasa ilibidi tutafute namna ambavyo ataweza kusikika vizuri,
“Alinipigia simu akiwa bado hayupo sawa, akasema anataka tufanye wimbo, akanitumia aidia, uzuri ni kwamba tayari alikuwa na mashahiri, nikatengeneza biti, tukarekodi mara ya kwanza lakini hatukupata kile ambacho tunakitaka,
“Nikamwambia bora niwe namfuata nyumbani kwake, nafunga studio yangu sebuleni kwake kufanya wimbo, ilituchukua mwezi mzima kukamilisha ngoma nzima kwa sababu kuna muda tulikuwa tunarekodi mstari mmoja mmoja, siku nyingine tunaahirisha kurekodi mpaka tukapata ile tunayoitaka,” anasema Yogo.
Kwa upande wa Christina Bella ambaye naye amesikika katika wimbo Ni Wewe, Yogo anasema hakuamini aliposikia Ommy Dimpoz anataka kuimba.
“Bella mwenyewe alicheka aliposikia Ommy anataka kuimba, lakini alikuja nyumbani akakuta tumesharekodi vesi mbili, aliposikiliza akasisimka sana, akapata mzuka wa kuingiza sauti ile ambayo inasikika, aliimba mara moja tu mzigo ukaisha,” anasema.
Aidha Yogo Beats anasema katika kipindi chote wanarekodi wimbo huo mara kadhaa Dimpoz alikuwa anashindwa kuimba katika kiwango chake cha awali jambo ambalo lilikuwa linamuumiza na kumtoa machozi.
“Tulifurahi sana tulipokamilisha kurekodi, tulipiga stori nyingi tukausikiliza mara nyingi kwa sababu siku iliyofuata ndiyo alikuwa anarudi tena Afrika kusini kufanyiwa upasuaji wa pili,” anasema Yogo.
ASHIKA NAMBA MBILI YOUTUBE
Katika mtandao wa YouTube hapa Tanzania imeendelea kushika namba mbili kwa kutazamwa zaidi huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Rayvanny kupitia wimbo wake Tetema aliomshirikisha Diamond Platnumz. Video ya Ni Wewe imefanyika siku 14 zilizopita katika pwani ya Mombasa Kenya na kuongozwa na Kelvin Bosco Jnr.