26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

MUHINGO KUZIKWA LEO

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MWILI wa mwanahabari mkongwe na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu (59), unatarajiwa kuagwa leo  sehemu mbili tofauti na kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni saa tisa alasiri.

Muhingo ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Myelofibrosis ambao hudhoofisha uwezo wa kinga za mwili kutengeneza damu  kwa  miaka 11, alikutwa na mauti Jumamosi wakati akitibiwa katika  Hospitali ya Agakhan jijini Dar es salaam.

Akizungumza  jana Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda ambaye pia alikuwa rafiki wa marehemu, alisema  ibada ya kuaga mwili wa Muhingo itafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mbezi (Kibanda cha Mkaa).

Alisema baada ya kusaliwa, mwili huo utapelekwa kanisani kwa ajili ya kuagwa na  baadaye utapelekwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo wanahabari, marafiki na jamaa wataungana kwa ajili ya kumuaga.

“Muhingo  kesho (leo) ataagwa sehemu mbili, kuanzia saa 4-6 ataagwa katika Kanisa  la KKKT ambapo alikuwa muumini, saa 6-8  mwili huo utawasili katika Viwanja vya Mnazi Mmoja eneo ambalo linafanyika maonesho ya kijeshi ambapo wanahabari,marafiki na jamaa watajumuika kwa ajili kuaga kabla ya kupelekwa makaburini,’alisema Kibanda.

Alisema  shughuli za mazishi ya Muhingo zitafanyika saa tisa alasiri katika makaburi ya Kinondoni.

Enzi za uhai wake, Muhingo alitambulika vema kama mwalimu mbobezi na kiongozi mahiri katika masuala ya habari kwa waandishi wengi ambao wanaendelea kuitumikia tasnia hiyo. Pia ni mmoja wa waanzilishi wa Gazeti la Mwananchi.

Umahiri wake ndani ya tasnia ya habari ulijitanua na kufahamika vema kuanzia mwaka 1993 alipoanza kuripoti kwenye magazeti ya Mwananchi na The Express.

Mazingira ya kubobea zaidi katika uandishi yalimpandisha hadhi mwaka 1995 na kuwa mwandishi mwandamizi, Mhariri wa Makala, Mhariri na Mkuu wa Kitengo cha Picha katika Gazeti la Mtanzania.

Ndani ya utumishi wake katika ngazi ya uhariri, Muhingo, alitumikia magazeti mbalimbali   nchini na baadaye kuwa  Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

Mbali na ubobezi wake katika tasnia hiyo, pia Muhingo amepata kutumikia nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Makete na Morogoro Mjini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles