28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

MUHIMBILI YALIA UHABA VIFAA VYA UPASUAJI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Profesa Charles Majinge

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema bado ina uhaba wa vifaa vya kufanyia upasuaji bila kufungua tumbo kwa kina mama.

Kauli hiyo imetolewa hospitalini hapo Dar es Salaam jana na madaktari waliokuwa wakifanya mafunzo ya namna ya kufanya upasuaji huo usiokuwa wa kawaida.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Profesa Charles Majinge, alisema ni jukumu la hospitali hiyo na bodi yake kuweza kuongeza vifaa hivyo.

“Vyumba vya hospitali vipo vya kutosha isipokuwa vifaa, ambalo ni jukumu la hospitali na bodi kununua ili kuviongeza. Vipo vya kuanzia, vitahitajika vingi na tutatenga vyumba vingi zaidi,” alisema Profesa Majinge.

Alisema huduma hiyo ni maendeleo ya elimu ya upasuaji ambayo kwa nchi za Ulaya zinaitumia kwa asilimia 90.

Pia alisema jukumu la sasa ni kuiwezesha hospitali hiyo kufanya kazi kama taasisi ambayo ina ubingwa wa hali ya juu na hospitali ya rufaa, ili wasiwepo wagonjwa wa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

“Tunakazania iweze kuleta huduma ambazo zilikuwa zinawapeleka wagongwa nje ya nchi ziweze kufanyika hapa. Warsha hii inazungumzia kutoa uvimbe kwa kina mama, kufanya upasuaji wa kizazi, kutoa kizazi, mirija na wagonjwa wengi wanahitaji,” alisema.

Profesa Majinge alisema upasuaji wa njia hiyo utawafanya kina mama wasipoteze damu nyingi na wasipoteze muda mwingi hospitali.

Aliendelea kusema kuwa upasuaji huo unapunguza muda wa mgonjwa kukaa hospitali na gharama za uendeshaji kwa sababu unaweza kufanyika asubuhi na jioni mgonjwa akaruhusiwa.

Kwa upande wake, bingwa wa magonjwa ya wanawake MNH, Dk. Vicent Tarimo, alisema njia hiyo ya upasuaji inapunguza athari zinazopatikana wakati wa upasuaji wa zamani.

Alisema upasuaji huo unasababisha tundu la sentimita moja na kuendelea na baada ya wiki mbili mgonjwa anaweza kwenda kazini kama kawaida.

Naye daktari wa magonjwa ya wanawake, Dk. Abidan Mganga, alisema pamoja na uhaba wa vifaa, lakini pia wataalamu wa kutoa huduma hiyo ni wachache.

“Wataalamu walizoea michano mikubwa, wataalamu wa kupasua kwa njia hii ya bila kufungua tumbo ni wachache, lakini pia vifaa vya upasuaji wa aina hii vinavyomwezesha mtaalamu kuingiza kamera tumboni na kufanya upasuaji vinahitajika tofauti na ule uliozoeleka,” alisema.

Dk. Mganga alisema pamoja na mafunzo hayo kuwa chachu kwa wataalamu wa kutoa huduma hiyo, lakini pia uongozi wa MNH uone kuwa ni vyema kuwatuma madaktari zaidi kwenda kuongeza ujuzi nje ya nchi.

“Muhimbili na Idara ya Magonjwa ya Kina Mama na Uzazi waliona wachukue hii warsha ili kuleta chachu kwa wataalamu kuchukua mafunzo ya aina hii, lakini pia kwa upande wa utawala waone sasa kuwa hizi huduma tunazotoa zinaendana na kasi ya sayansi na teknolojia ya afya, hii ikiwamo kuwapa wataalamu ujuzi wa kisasa ikiwamo kusoma na vifaa,” alisema. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles