Mugabe aondoka mkutanoni Swaziland akidaiwa kuugua

RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

HARARE, ZIMBABWE

RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe aliondoka katika mkutano wa kikanda mjini Mbabane, Swaziland juzi kabla haujamalizika kuelekea Dubai, ikidaiwa ameenda kutibiwa.

Mkutano huo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ulitarajia kumalizika jana.

Aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Harare saa 1:44 jioni na ilipofika saa nne usiku akaelekea Dubai.

Gazeti binafsi la NewsDay lilikariri chanzo cha habari serikalini kikisema Rais Mugabe alikuwa akienda Dubai kuangaliwa afya yake.

Vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na Serikali, ambavyo Jumatatu viliripoti kuondoka kwa Mugabe kuelekea Mbabane, havikusema lolote jana kuhusu ziara ya Dubai.

Rais Mugabe mara kwa mara husafiri kwenda Singapore kwa matibabu.

Huko nyuma, alikana ripoti kuwa anaugua kansa ya tezi dume, akisema anaenda Mashariki ya Mbali kwa matibabu ya jicho.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Zimbabwe, Sydney Sekeremayi, jana alisema vyombo vya usalama vinadhibiti hali baada ya mlolongo wa maandamano ya kuupinga utawala wa Mugabe.

Waandamanaji walipambana na polisi Jumatano na Ijumaa wiki iliyopita baada ya wanausalama kuvunja kwa nguvu maandamano yaliyofanyika mji mkuu wa Harare.

Vyama vya upinzani vinashinikiza mageuzi ya uchaguzi, kukomesha rushwa, mgogoro wa uchumi pamoja na kujiuzulu kwa Mugabe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here