NA OSCAR ASSENGA, TANGA.
KATIBU wa Chama cha Watu Wenye Albino Mkoa wa Tanga (TAS), Mahamudu Salehe, amesema ukosefu wa losheni za kuzuia mionzi ya jua kwa jamii hiyo kumesababisha vifo vya watu watano vinavyotokana na kansa ya ngozi.
Alisema vifo hivyo vimetokea kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita mkoani hapa jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua stahiki kukabiliana nalo kwa vitendo ili kuiwezesha jamii hiyo kuweza kutimiza malengo yao.
Salehe aliyasema hayo jana wakati akipokea msaada wa mabati na misumari kwa ajili ya ukarabati wa ofisi yao kutoka kwa Katibu wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba Asilia mkoani hapa (UWAWATA), Jumaa Lukuwa.
“Lakini pia kukosekana kwa matibabu ya kudumu kwenye wilaya mbalimbali mkoani Tanga ndiyo chanzo cha vifo vya jamii hiyo kwani wakati wa uhitaji wake unapochelewa wanaweza kupoteza maisha, hivyo tunaiomba jamii na Serikali kuangalia namna ya kutusaidia ili vipatikane,” alisema.
Akizungumzia msaada waliotoa, Lukuwa alisema ni kwa ajili ya kuiwezesha jamii ya albino kuondokana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili, lakini pia kutoa fursa ya kuweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Alisema licha ya hivyo, lakini pia wamefanya hivyo kuisaidia jamii hiyo kuweza kutekeleza vema majukumu yao ya kuwaelimisha wananchi juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wakunga ili hali hiyo iweze kutokomezwa kwenye jamii.
“Lakini pia tutashirikiana na chama hicho kutoa elimu juu ya dhana potofu ya ramli kwa kuhakikisha tunaipiga marufuku kwani ndiyo chanzo pia cha mauaji kwa jamii hiyo,” alisema.