24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Mtuhumiwa: Lukuvi alinikaba, kuninyang’anya fedha

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Mohammed Kiluwa amedai anazitaka fedha zake Dola za Marekani 40,000.

Amedai  hakumpa rushwa yoyote Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi fedha hizo  ila alimkaba na kumnyang’anya  akiwa ofisini kwake .

Amedai hawezi kumpa fedha waziri  kwa  sababu viwanja vyote alivipata kwa halali isipokuwa anadai  Waziri Lukuvi anatumikana baadhi ya wafanyabiashara kumsingizia amempa rushwa, kumchafua  ili wafanyabiashara hao wachukue nafasi yake.

Kiluwa alidai hayo jana katikaMahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu Mkazi Samweli Obasi  alipokuwa akitoa utetezi katika kesi inayomkabili ya kutoa rushwa ya Dola za Marekani 40,000 kwa Waziri Lukuvi,akiongozwa na wakili wake, Imani Madega.

Alidai  tukio hilo lilitokea alipokuwa ofisini kwa waziri huyo ambaye alimtaka apeleke hati za viwanja vilivyoko Kibaha Mlandizi ambavyo alivipata kwa halali na kufuata utaratibu wote kwa gharama ya Shbilioni moja.

Alidai taarifa za kutakiwa kufikakwa waziri huyo alizipata kutoka kwa mwanaye Shabani Selemani ambako usiku huo huo Julai 14 mwaka huu aliamua kumpigia simu Waziri Lukuvi ambaye alimsisitiza azipeleke Jumatatu.

“Nilimweleza Waziri nasafiri Jumapili kuelekea Mtwara lakini alinitaka niende ofisini kwake  Jumatatu saa tano kasorobo nilipokuwa nanunua vitu mbalimbali yakiwamo mapazia, jenereta vya mahitaji ya ofisi, waziri alinipigia simu.

“Baada ya kuniambia niende sikwenda nikaendelea na ununuzi, saa sita akapiga tena simu anasema nifanye haraka ana kikao na watu wa Benki ya Dunia ninamchelewesha nifanye haraka.

“Nilitoka nilipokuwa nikaelekea ofisini kwa waziri, nikiwa naegesha gari akanipigia tena mara ya tatu.

“Nilipofika mapokezi tu nilimkuta kamishna wa ardhi aitwaye Mathew nilimuuliza ninachoitiwa alijibu hajui, nilienda mpaka juu kwa katibu mhutasi wa waziri ambaye alinijibu nisubiri kidogo baada ya muda akaniruhusu niingie.

“Nilipoingia ndani nilimkuta waziri amekaa katika meza ndefu yenye viti vingi akiwa peke yake ofisini, akanionyesha kiti cha kukaa, nikakaa.

“Baada ya kukaa akaniuliza hati zipo wapi, nikamjibu hazipo kwa sababu mwenzangu anayeziweka kasafiri. Akajibu Duhh…..akaniomba vipeperushi na kwa sababu natembea navyo muda wote nikampatia,” alidai.

Kiluwa  alidai Waziri hakumwambia hati hizo anazitaka kwa ajili ya nini.

Alidai Waziri  alimuuliza katika mkoba wake alikuwa amebeba nini na akamjibu fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji ya ofisi yake ambayo walikuwa wakiifanyia ukarabati.

“Waziri aliinuka akaniambia basi nipe, mimi nikawa namuangalia tu, ilifika steji akanishika akaniinua wakati huo ndani tupo wawili tu.

“… akanikaba akaninyang’anya begi langu akafungua zipu akatoa fedha ndani ya begi akaweka mezani. Kutokana na kunikaba, nikawa napiga kelele nisaidieni, nisaidieni, nisaidieni,” alidai.

Alidai baada ya muda kidogo mlango ulifunguliwa aliingia mtu mmoja akamwambia yupo chini ya ulinzi na baadaye akaingia mwingine akasema yupo chini ya ulinzi na kuanza kuuliza na shahidi atakuwa nani.

Licha ya hali hiyo pia alidai waliulizana mmoja akajibu mwenzake akamuulize waziri, alisema shahidi awe katibu muhtasi wake.

Alisema ndipo walipoamua kwenda kumuita katibu muhtasi wa waziri ambaye alifika na kuanza kusoma namba moja mojazilizopo katika dola hizo.

Kiluwa alidai hakutoa fedha wala kumshawishi waziri huyo, bali waziri ndiye aliyempokonya mkoba akafungua zipu na kutoa fedha na kuweka kwenye meza na kwamba ndani walikuwa wawili tu.

Alidai  hakuna mchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wala Kamishna wa Ardhi aliyeona hayo.

Alidai kitendo alichokifanyaWaziri Lukuvi ni kumsingizia na kudanganya kwamba alitoa rushwa wakati  katika ushahidi wake na wala mashahidi wa upande wa Jamhuri   wameshindwa kuthibitisha tuhuma hizo.

Pia  alidai Waziri Lukuvi anatumika na baadhi ya wafanyabiashara kwa lengo la kutaka kumchafua na kumharibia biashara yake iliwachukue nafasi yake.

Kwa sababu hiyo  aliiomba mahakama kumuona hana hatia nakurejeshewa kwa hati zake 16 ambazo alikuwa hajapewa na kurudishwa katika daftari la usajili kwa hati zake 57 alizokuwa amepatiwa.

Vilevile  aliomba arudishiwe fedha zake Dola za Marekani 40,000 ambazo zinashikiliwa na kudai kwamba eneo hilo angewekeza vijana 40,000 wangepata ajira na mapato yangepatikana.

“Waziri Lukuvi anamkwamisha Rais John Magufuli katika azima yake ya kuiingiza Tanzania katika uchumi wa viwanda,” alidai.

Awali, Kiluwa alidai shughulizake ni mfanyabiashara ambazo alianza mwaka 1986 akianza na kazi ya ukandarasi wa barabara na nyumba, duka la vifaa vya ujenzi, duka la spea za magari,kiwanda kidogo cha sabuni Mtwara ambako kwa sasa ana kiwanda cha chuma na eneola uwekezaji ambalo anatarajia kuwa na viwanda takriban 70.

Alidai ardhi anayoimiliki kwa halali ina viwanja 73, nyumba za makazi ambazo zina hati zilizosajiliwa kwa jina lake na mashamba.

Alidai   alifuata taratibu zote zikiwamo za kulipiaSh bilioni moja na kodi ya serikali Sh milioni 190 na alivipata baada ya Rais Dk. John Magufuli kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kiwanda chake cha chumacha Kiluwa ambako alimhoji juu ya eneo alilonalo na kumweleza kuwa hekta 50.

Rais Magufuli alimtaka amalize hilo eneo kwanza ndipo awasiliane na mkuu wa mkoa ili ampatie eneo la uwekezaji.

Kiluwa anadai katika eneo la hekta 50 amekeza viwanda vitano vya kuzalisha betri za gari na pikipiki, nguzo za umeme, kiwanda cha makasha  makubwa, bomba za plastiki na kiwanda cha zege.

Kiluwa alidai aliwasilisha maombi ya kupatiwa hekta 3000, lakini akaambiwa atapatiwa hekta 1000 ambazo hekta 500 za mwanzo alilipa Sh  milioni 500 katika halmashauri  na 500 nyingine zilikuwa zikihitaji kibali cha waziri ambacho kilipatikana baada ya mwezi na alilipia tena Sh milioni 500.

Kiluwa alikuwa na shahidi mmoja, Jurijsmar Tinovs ambaye ni mmiliki na mwanahisa katika Kampuni ya Kiluwa.   Ana hisa asilimia 65 na alidai alikuwa na hati zilizotakiwa kwa waziri na siku hiyo hakuwapo nchini, alikuwa Urusi.

Hukumu ya kesi hiyo imepangwakutolewa Desemba 24, mwaka huu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles