26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

Mkutano wa SADC ulivyorahisisha kutangaza vivutio vilivyopo

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MGENI njoo mwenyeji apone ni kati ya methali zilizozoeleka ambayo humaanisha kwamba mgeni anapomtembelea mwenyeji hufaidika kwa njia moja au nyingine.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Tanzania ambayo ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Agosti 17 na 18 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 1,000 kutoka nchi wanachama zinazounda jumuiya hiyo.

Katika mkutano huo Tanzania ilicheza karata yake vizuri kwani ilijiandaa vyema katika kila eneo na kufanya mkutano huo kuwa na mafanikio makubwa.

Ikiwa nchi iliyojaliwa kuwa na rasilimali nyingi hasa vivutio vya utalii, Tanzania ilitumia vyema mkutano huo kujitangaza kwa sababu wageni wengi ndiyo ilikuwa mara yao ya kwanza kuja nchini hivyo ujio wao ulirahisisha kutangaza vivutio vilivyopo.

Mkutano huo ulitanguliwa na Maonyesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC kisha kufuatiwa na vikao mbalimbali vya kisekta na wakati wote huo tayari kulikuwa na matangazo ya picha za mnato na video yanayoonyesha vivutio tofauti vilivyopo nchini.

Matangazo hayo yaliwekwa kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Barabara ya Nyerere, mitaa mbalimbali ya katikati ya jiji, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) na hoteli walizofikia wageni husika.

Katika eneo la mkutano (JNICC) matangazo yaliwekwa ndani na nje ya ukumbi sambamba na kuwapatia wageni vipeperushi vyenye taarifa za vivutio mbalimbali.

Pia katika chumba kilichotumiwa na wake za marais kwa ajili ya chakula kulikuwa kukionyeshwa video za vivutio mbalimbali vikiwemo vinavyopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo ina aina 350 za maua huku aina zaidi ya 40 zikiwa hazipatikani sehemu nyingine yoyote duniani.

Takwimu zinaonyesha idadi ya watu katika SADC ni milioni 350 lakini urali wa biashara baina ya nchi wanachama bado si mzuri licha ya nchi kadhaa kuwa na rasilimali nyingi kulinganisha na nyingine.

Kutokana na upekee wa mkutano huo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliunganisha nguvu ya pamoja na kutumia fursa hiyo kuongeza mshikamano wa biashara katika ukanda huo.

Wengine walionufaika

Wajasiriamali, wamiliki wa hoteli, wafanyabiashara wa vyakula, usafiri, taasisi za fedha, burudani na wengine walijitokeza na kutumia mkutano huo kujitangaza kwa lengo la kupata kipato na kujenga uhusiano wa kibiashara.

Pia taasisi mbalimbali za umma zilikwenda katika mkutano huo na ushawishi wa miradi, biashara na uwekezaji kwa lengo la kupata washirika na fursa za kiuchumi.

Kwa upande wa taasisi za fedha benki mbalimbali kama vile CRDB, NMB, TBP, NBC na Azania zilikuwa zikitoa huduma wakati wa mkutano huo.

Hoteli nazo zilinufaika hasa zilizoko katikati ya jiji huku nyingine zikiwa ni zile zilizoko Masaki na Mikocheni.

Baadhi ya hoteli zilizofaidika ni Slipway, Double Tree, Amaria (Mikocheni), City Lodge, Doble View, Tropical, Florida, Sea Shells, Southern Sun, Serena, Hyatt, Holday Inn, Amaria (city centre), Tanzania executive suites, Tifany Diamond, Rainbow, Sophia, Peacock, Best Western na Sleep Inn.

Kwa upande wa watoa huduma za usafirishaji nao walipata fursa za kukodisha mabasi ambayo yalikuwa yakiwachukua na kuwarudisha wajumbe kutoka mahali walikofikia na sehemu kunakofanyika mkutano huo.

Mabasi hayo pia yalitumika kusafirisha wajumbe sehemu mbalimbali kama vile kutembelea baadhi ya viwanda vilivyopo nchini na baadhi ya miradi ya kimkakati kama vile Reli ya Kisasa (SGR) na ule wa uzalishaji umeme unaotekelezwa katika maporomoko ya Mto Rufiji.

Kwa upande wa burudani baadhi ya vikundi vya ngoma za asili ikiwemo ya utamaduni wa Kabila la Wamasai, Wagogo na kundi la TOT Plus ni miongoni mwa waliopata fursa ya kutumbuiza.

Pamoja na mambo mengine mkutano huo ulishuhudia Rais Dk. John Magufuli akikabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Katika kipindi ambacho Tanzania itakuwa mwenyekiti kwa mwaka mzima kutakuwa na matukio mengi ya jumuiya hiyo yatakayokuwa yakifanyika hapa nchini kwa hiyo kiuchumi ni fursa kubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema wiki iliyopita kuwa kutakuwa na mikutano ya kisekta takribani 30 ya jumuiya hiyo itakayofanyika hapa nchini.

Biashara ndani ya SADC

Ukanda huo unatajwa kuwa na utajiri mkubwa lakini nchi wanachama bado hawajaweza kuuendeleza na kufikia viwango vya ushindani kwani hata biashara baina yao imekuwa chini kwa asilimia 25.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la SADC, Peter Varndell, ambaye aliwasilisha maazimio ya baraza hilo wakati wa kufunga Maonyesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda, anasema mazingira mazuri ya biashara yatasaidia kukuza biashara na ajira kikanda.

Miongoni mwa maazimio ya baraza hilo ni nchi wanachama kuhimiza ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi, kuainisha sera na sheria zinazosababisha ufanyaji biashara kuwa mgumu, kusimamia sera na kuharakisha maendeleo ya vijana katika jumuiya hiyo.

Mengine ni kuwa na mfuko wa kuendeleza teknolojia na ubunifu, kuwawezesha wanawake na vijana kuhakikisha wanashiriki katika ujenzi wa viwanda na kuwa na mpango kabambe wa kuzalisha gesi ya kutosha ili watu waweze kuanzisha viwanda kwa wingi.

Mwenyekiti wa baraza hilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte, alimuomba Rais Magufuli kusukuma mbele ajenda ya biashara ili waweze kunufaika na eneo huru la biashara Afrika.

Shamte anasema zaidi ya asilimia 90 ya ajira zinatengenezwa na sekta binafsi katika nchi za SADC lakini bado sekyta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi.

Anasema kutokana na vikwazo hivyo gharama za kufanya biashara Afrika ni zaidi ya mara saba kulinganisha na nchi za Asia.

Anasema pia zaidi ya Dola bilioni 30 zimekuwa zikitumika kuagiza chakula nje wakati kuna asilimia 60 ya ardhi inayoweza kutumika kuzalisha.

“Tuachane na ushindai usio na maana tukumbatie zaidi ushirikiano kuhakikisha miradi midogo na mikubwa inafanikiwa. Tunaunga mkono jitihada za serikali kupata suluhisho la matatizo yetu na hatuna sababu ya kuendelea kulalamika,” anasema Shamte.

Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax, alisema ushiriki wa Tanzania bado ni mdogo katika jumuiya hiyo lakini fursa bado zipo nyingi.

“Kuna fursa kubwa ya soko la huduma kwa sababu vikao si chini ya 30 vitafanyika Tanzania hivyo kuna haja ya kujadiliana namna gani fursa hizo zitumiwe,” alisema Dk. Tax.

Mkutano huo ulifanyika chini ya kaulimbiu isemayo ‘Mazingira Wezeshi ya Biashara kwa ajili ya Kuwezesha Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda, Kukuza Biashara na Kuongeza Fursa za Ajira’.

Kaulimbiu hiyo imeweka msisitizo katika kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo kuondoa vikwazo vya mipakani, ukiritimba kwenye maamuzi, rushwa ili kukuza sekta ya viwanda na kustawisha biashara kwenye ukanda huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles