23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa kachero aliyeuawa akamatwa

4NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

SALOME Lukumay ambaye ni mke wa aliyekuwa kachero mkuu wa kitengo cha intelijensia cha Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), marehemu Emily Kisamo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa ajili ya mahojiano.

Mbali na Salome, taarifa zinasema jeshi hilo linawashikilia watu wengine wawili kwa ajili ya mahojiano juu ya kifo cha Kisamo.

Vyanzo mbalimbali vya habari jijini hapa wakiwamo baadhi ya marafiki wa marehemu Kisamo, waliiambia MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, kwamba Salome na watu hao wawili wanashikiliwa kwa kuwa kuna dalili za wao kuwa na mawasiliano na kachero huyo kabla hajauawa kwa kuchinjwa.

Kisamo anadaiwa kuuawa Desemba 18, mwaka huu kwa kuchinjwa na kichwa kutenganishwa na kiwiliwili kisha mwili wake kuwekwa ndani ya buti ya gari yake iliyotelekezwa eneo la Kikwarukwaru, lililopo Kata ya Lemara jijini hapa.

Taarifa za mke huyo wa marehemu zilionekana kuwa za kweli baada ya  MTANZANIA kufika nyumbani kwa marehemu jana na kukuta waombolezaji wakiwa peke yao bila yeye kuwapo.

Hata MTANZANIA lilipotaka kuonana na mke huyo wa marehemu, mmoja wa ndugu zake wa karibu alisema hakuwapo nyumbani tangu mumewe alipouawa wiki iliyopita.

“Tangu jana watu wanakuja msibani kutoa pole, mama mwenye nyumba hayupo. Taarifa zilizopo zinadai bado anaendelea kulisaidia Jeshi la Polisi kwenye upelelezi wa mauaji ya muwe wake,” alisema rafiki wa marehemu akiomba asitajwe jina gazetini kwa kile alichosema yeye si msemaji wa familia.

Naye msemaji wa familia ya marehemu Kisamo, Wakili Mwandamizi wa Kujitegemea Colman Ngallo, alisema hana taarifa za mke wa marehemu kukamatwa.

“Hatuna taarifa yoyote mpaka sasa, polisi wanaendelea na uchunguzi wao,” alisema Wakili Ngallo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas, alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo jana, aliwaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo ni la kesi ya mauaji, hivyo analazimika kujiridhisha katika utoaji wa taarifa.

Kisamo aliuawa wiki iliyopita na watu wasiojulikana, na polisi waligundua maiti yake ikiwa ndani ya gari baada ya kuendesha msako mkali wa kumtafuta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles