25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 1, 2024

Contact us: [email protected]

Miracolo kuanzisha shule ya uuguzi, famasia

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Uongozi wa Hospitali ya Miracolo iliyopo Segerea Wilaya ya Ilala Dar es Salaam unatarajia kuanzisha shule ya uuguzi na famasia baada ya mafanikio yaliyoonekana katika utoaji huduma.

Akizungumza Juni 30, 2023 wakati wa maadhimisho ya miaka saba tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, Deogratias Kweka, amesema imekuwa ikitoa huduma bora kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya nchi.

Amesema kutokana na mafanikio hayo wamejipanga kupanua huduma ambazo zitahusisha pia kuanzishwa kwa shule hiyo.

Naye Mkurugenzi wa hospitali hiyo ambaye pia ni dakrari bingwa wa watoto, Anna Deogratias, amesema wataendelea kutoa huduma bora na kuongeza huduma za kibingwa ili kuwafikia Watanzania wa maeneo mbalimbali ya nchi.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Maganga, amesema wana kliniki za magonjwa ya watoto, kinamama, moyo, sukari, figo, upasuaji na kwamba wako mbioni kuanzisha kliniki ya macho.

“Tumejipanga kushirikiana na vituo vingine vya afya vinavyotuzunguka ili kurahisisha utoaji huduma kwa sababu tunategemeana, inawezekana mimi nikawa na huduma hii na mwingine hana kwahiyo kwa kushirikiana tutaweza kufanya kazi kwa karibu,” amesema Dk. Maganga ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo, kisukari na figo.

Mlezi wa hospitali hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamisi Kigwangalla, ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo na kuwataka kujitofautisha na watoaji huduma wengine ili kufikia mabadiliko makubwa.

“Wakati mnaendelea kujipanga kwenda hatua nyingine mfikirie kujitofautisha, usiangalie mwenzako ni mkubwa kuliko wewe, mnaweza mkashindana na msiogope kushirikiana na ambaye anakuzidi nguvu,” amesema Dk. Kigwangalla.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Segerea, Jackson Bashange, ameipongeza hospitali hiyo kwa huduma bora wanazotoa kwani imekuwa msaada ndani na nje ya mtaa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles