25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

MIMBA UTOTONI: TATIZO HUANZIA KWENYE USIRI WA WAZAZI

Na VERONICA ROMWALD –DAR ES SALAAM

NDOA na mimba za utotoni zinatajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa mtoto wa kike kuweza kufikia ndoto zake kama ilivyo kwa mtoto wa kiume.

Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, takwimu zinaonesha tatizo hilo linazidi kuongezeka.

Hali hiyo inatajwa kuchangiwa zaidi na mila potofu na desturi za baadhi ya makabila ambazo kwa namna moja au nyingine zinakandamiza haki za mtoto wa kike.

Kwa mfano, yapo baadhi ya makabila ambayo hadi leo yanamuona mtoto wa kike ni sawa na bidhaa inayofaa kuuzwa na kununuliwa hasa pindi tu anapovunja ungo.

Wakati mtoto wa kike akionekana kuwa sawa na bidhaa, mambo ni tofauti kwa mtoto wa kiume ambaye huendelea kupatiwa mahitaji na haki zote za msingi hususan elimu.

Watoto wa kike mara nyingi tunashuhudia katika baadhi ya maeneo wakikatishwa masomo yao na kuozeshwa.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) ya mwaka 2016, inaeleza wasichana wana fursa ndogo ya kumaliza shule ikilinganishwa na wavulana.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Oktoba 20, mwaka jana huko Visiwani Zanzibar, inaeleza wasichana wako katika hatari zaidi ya kukabiliwa na ndoa za utotoni, ajira za watoto, ukeketaji na matendo mengine ya udhalilishaji.

Inataja asilimia 42 ya wasichana barani Afrika, huolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 na kwamba kwa wastani watoto wa kike wawili kati ya watano huolewa kabla ya kufikisha umri huo wa miaka 18 nchini.

Kulingana na ripoti hiyo, ndoa za utotoni, ajira za watoto, ukeketaji na matendo mengine ya udhalilishaji yanayodhoofisha haki na afya ya msichana yanatishia matumaini ya ajenda ya kimaendeleo ya dunia.

Kwamba, matendo hayo yanaathiri wasichana na kuvunja haki zao za kibinadamu kuanzia wakiwa na umri wa miaka 10 na kufanya washindwe kutimiza ndoto zao katika maisha yao hapo baadae.

Inabainisha kuwa zaidi ya nusu ya wasichana 60 milioni walio na umri wa miaka 10 wanaishi katika nchi 48 zenye ukosefu mkubwa wa usawa wa kijinsia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya vijana milioni 125 walio na umri wa miaka 10 hii leo, wasichana ni milioni 60.

 Ripoti ya WHO

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na matokeo kuchapishwa Januari, 2016; Tanzania inatajwa kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni.
Ripoti hiyo inaeleza matukio ya ndoa na mimba za utotoni nchini yapo kwa kiwango cha asilimia 28.

 Ripoti ya NBS

Matokeo ya utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania (TDHS,
2010) uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini (NBS) nayo yanaonesha asilimia 37 ya watoto wa kike Tanzania huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.
Kwa mujibu wa utafiti huo, Mkoa wa Shinyanga unaoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ukifuatiwa na Mkoa wa Tabora wenye asilimia 58, Mara asilimia 55, Dodoma asilimia 51, Lindi asilimia 48, Mbeya asilimia 45, Morogoro asilimia 42, Singida asilimia 42, Rukwa asilimia 40 na Ruvuma wenye asilimia 39.
Ripoti hiyo inataja mikoa mingine yenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni kuwa ni Mwanza asilimia 37, Kagera asilimia 36, Mtwara asilimia 35, Manyara asilimia 34, Pwani asilimia 33, Tanga asilimia 29, Arusha asilimia 27, Kilimanjaro asilimia 27, Kigoma asilimia 29, Dar es Salaam asilimia 19 na Iringa ambao una asilimia nane.
Meneja wa Afya ya Uzazi na Ujinsia na Afya ya Mama na Mtoto wa UNFPA-Tanzania, Felister Bwana anasema hali hiyo inachangiwa zaidi na ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana.

Anasema jamii nyingi hasa zilizopo barani Afrika zinachukulia suala la afya ya uzazi na ujinsia, uhusiano na kujamiiana kwa ujumla ni masuala ambayo hayapaswi kuzungumzwa.

“Wanaamini ni mwiko kuzungumzia masuala hayo na kamwe huwezi kukuta wazazi wakizungumza na watoto wao kuwaeleza ukweli juu ya mambo hayo au baba anaona ni jukumu la mama kuwaeleza watoto wake, hali hiyo inafanya vijana kutafuta taarifa wenyewe shida inatokea pale wanapopewa taarifa ambazo si sahihi,” anasema.

 Mkakati wa kuwakomboa

Felister anasema kutokana na hali hiyo, UNFPA Kanda ya Afrika iliamua kuanzisha mradi wa Amua Accelerator kwa lengo la kutafuta mbinu bunifu kukabiliana na tatizo la ndoa na mimba za utotoni nchini.

Anasema ili kufanikisha mradi huo, UNFPA imeshirikiana kwa ukaribu na serikali pamoja na mashirika likiwamo lisilo la Kiserikali la Sahara Sparks na Mulika Tanzania.

“Mradi huu unatekelezwa katika nchi nne ikiwamo Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, tunawakusanya vijana na wao wanatakiwa kubuni mbinu ambazo zitatumika kufikisha ujumbe sahihi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana wenzao,” anasema.

Anasema pamoja na kwamba lengo ni kufikisha ujumbe sahihi, kingine ni kuwatengeneza fursa ya ajira vijana kupitia ubunifu wao.

“Tuliona kwa kuwa tatizo la ndoa na mimba za utotoni linawakabili vijana, tuliamini kwamba wanafahamu tatizo lipo wapi ingawa vijana wengi bado hawana elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi na ujinsia.

“Pia hawajafikiwa na huduma za afya ya uzazi na ujinsia, tumebaini pia hata wale waliofikiwa na huduma, wahudumu wengi si rafiki kwa vijana wanaokwenda kufuata huduma hizo hii imesababisha wengi kuwa waoga na kushindwa kujiamini kufika kwenye vituo vya kutolea huduma hizi.

“Vile vile vijana wengi waishio maeneo ya vijijini hawapati taarifa sahihi kuliko hawa waishio mjini. Kuna suala la mila na desturi pia, ambapo katika jamii nyingi inaonekana ni mwiko kutamka masuala ya afya ya uzazi na ujinsia.

“Yaani masuala ya uhusiano na kujamiiana kwa ujumla huwezi kukuta mzazi anamweleza kijana wake au baba anaona ni jukumu la mama kuwaeleza watoto wake, hali hiyo inafanya vijana kutafuta taarifa wenyewe shida inatokea pale wanapopewa taarifa ambazo si sahihi,” anasema na kuongeza: “Hivyo, kupitia mradi huu wa Amua Acceleration tuliona wakati umefika sasa kuwaita vijana wenyewe na kuwashirikisha ili wabuni mbinu zitakazosaidia kuwafikishia ujumbe sahihi vijana wenzao.

Anasema kwa kiwango kikubwa vijana waliofanikiwa kufikia mwisho wa mchakato huo wamefanikiwa kubuni mbinu za kisasa ambazo anaamini zitatumika kufikisha ujumbe sahihi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana wenzao na hivyo kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.

Mchakato ulivyokuwa

Meneja Mradi wa Sahara Sparks, Adam Mbyallu anasema waliwakutanisha wadau wa sekta ya afya na vijana wenyewe ambao walijadiliana na kuainisha changamoto zinazowakabili vijana kuhusu suala zima la afya ya uzazi na ujinsia.

“Wadau hao waliainisha matatizo manne ambayo ni ndoa za utotoni, mimba za utotoni, afya ya hedhi, maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Wadau walikubalina suala la ndoa za utotoni liwe ajenda kuu la mradi,” anasema.

Anasema tulienda mbali zaidi na kuwauliza wadau iwapo wanadhani tatizo hilo linachangiwa na nini hasa na wakatueleza ni kutokana na ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi na ujinsia.

“Vijana walisisitiza kwamba hakuna upatikanaji wa huduma rafiki za afya ya uzazi na ujinsia, vituo vingi vimewekwa kwenye kliniki za uzazi na watoa huduma si rafiki,” anasema.

Anasema wadau hao walieleza pia jambo jingine linalochangia ongezeko la ndoa na mimba za utotoni ni ushiriki mdogo wa wanamume katika kutatua changamoto za uzazi salama na ujinsia.

Anasema wadau pia walisema kuna mkanganyiko wa sheria ya ndoa ya 1971 ambayo inaruhusu mtoto kuolewa akiwa na umri wa miaka 14/15 kwa ruhusa ya wazazi wake.

Anasema uwapo wa ndoa na mimba za utotoni kumechangia ongezeko la idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi.

“Kwa hiyo tulipokea mawazo 373 ambayo yalitoka kwa vijana wenyewe na baada ya kuyachambua tulipata vikundi sita ambavyo vine kati yake vimeibuka na ushindi na kujinyakulia Dola 6,000 sawa na Sh. Milioni 14 kila kimoja,” anasema.

Kauli za washindi

Mwakilishi wa kikundi cha Harakati za lucy Gwamaka Mwabuka anasema wametengeneza katuni ambayo wataitumia kufikisha ujumbe wao kupitia mtandao wa youtube.

“Tumekusudia pia baadae kuingia mkataba na chaneli mbalimbali nchini ambazo zitarusha katuni hizi zitakazotengenezwa katika ‘episods’ tofauti tofauti, Lucy anawakilisha wasichana wengi,” anasema.

 E-Shangazi

Mwakilishi wa kikundi hiki, Debora Peter anasema E- Shangazi ni shangazi wa mtandao ambaye atakuwa akitoa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa njia ya facebook.

“Katika jamii nyingi za Kiafrika shangazi ni mtu muhimu ambaye vijana humshirikisha mambo mengi, kwa hiyo kupitia shangazi huyu wa mtandao kijana, mzazi au mlezi ataweza kumuuliza swali lolote shangazi huyu naye atampa majibu sahihi kupitia akaunti ya ‘facebook messenger’,” anasema.

 Mkwawa Art Space

Kundi hili ambalo makazi yake yapo kule mkoani Iringa lenyewe limejipanga kutumia sanaa kufikisha ujumbe kwa vijana, wazazi na walezi.

 Maisha Package

Mwakilishi wa kundi hili, anasema wao wamebuni kuuza taulo za kike, kondomu za kiume na kwamba wataweka kipeperushi chenye taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi na ujinsia.

“Kwa kuzingatia umri, tumetengeneza vitita viwili, kuna ambacho hakitakuwa na kondomu za kiume ndani yake (Maisha Package Plain) ambazo mzazi anaweza kumnunulia mtoto wake pia na akapata kipeperushi chenye taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi na ujinsia,” anasema.

Mwakilishi wa UN

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi hao, Mwakilishi Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini (UN -TANZANIA), Alvaro Rodriguez anasema kupitia mradi huo ambao una malengo sawa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), UN wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana.

“Mradi huu ni sehemu ya mpango wetu wa kuhakikisha vijana wanafikia malengo yao, nawashukuru UNFPA kwa kuendesha mradi huu kwa ajili ya vijana Tanzania.

“Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea uchumi wa kati, kunahitajika kuwa na sera na mipango ambayo itaiwezesha nchi kuwa na uwiano wa umri na kutasaidia kuwapo kwa nguvu kazi na hasa vijana ambayo itafanya kazi na kusaidia uchumi kukua,” anasema Rodriguez.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles