24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

MIKAKATI KUFIKIA WATALII  MILIONI TANO YAANZA

Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeanza utekelezaji wa agizo la Rais, Dk.John Magufuli la kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2020.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Japhet Hasunga, alipokuwa akifungua jukwaa la wawekezaji katika sekta ya utalii lililofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), mjini hapa jana.

Akizungumza na wawekezaji kutoka kampuni za mawakala wa utalii, wamiliki wa mahoteli, kambi za kitalii na wadau wengine wa sekta hiyo Hasunga alisema, watatumia jukwaa hilo kufikia malengo.

“Ilani ya CCM, imeelekeza hadi kufikia mwaka 2020 tuwe tumefanikiwa kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni 2,” alisema na kuongeza:

“Lakini lengo hilo limesharekebishwa na Rais Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi uzinduzi wa ujenzi wa rada nne, ambapo alitamka na kuagiza ifikapo mwaka 2020 tuwe tumefikia watalii milioni 5,” alisema.

Alisema kuandaliwa kwa jukwaa hilo na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuna toa fursa pana ya kuwasikiliza wawekezaji hao kutoka sekta ya utalii ikiwamo kufanya kazi nao kwa pamoja.

“Lengo la Jukwaa hili ni kuwaleta pamoja wawekezaji hawa ili tujadiliane nao na kuzungumzia maendeleo ya sekta hii ya utalii ikiwamo kuona vivutio katika eneo letu la Ngorongoro.”

“Tumewaita ili kuona ni uwekezaji wa aina gani unatakiwa kuwapo kwenye eneo hilo kwani tayari tumeshawatembeza kwenye baadhi ya maeneo,” alisema Hasunga.

Kwa upande wake Naibu Mhifadhi anayeshughulikia uhifadhi, Maendeleo ya Jamii na Utalii Dk. Maurus Msuha alisema, jukwaa hilo limefanyika kwa lengo la kuongeza uekezaji kutokana na kuwa na vivutio vingi.

“Tumekuja kuwaeleza wawekezaji fursa zilizopo pia namna gani tunaweza kushirikiana nao kutumia fursa hii ya upekee wa bonde la  Ngorongoro duniani ili kupata mapato yatakayotuletea faida.

“Unaweza kujiuliza kwanini Ngorongoro, ukweli ni kwamba hakuna Ngorongoro nyingine duniani kilichopo pale huwezi kukipata katika maeneo mengine duniani,” alisema Dk. Msuha.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka akizungumza kwenye jukwaa hilo aliwahakikishia wawekezaji hao usalama wa kutosha katika shughuli zao za utalii zinazoleta manufaa kwa taifa.

“Ushiriki wa wananchi ni mdogo katika masuala ya utalii, tuwaombe wawekezaji waliopo na watakaokuja wajihadii kurudisha faida kidogo wanayopata kuipeleka kwenye miradi ya maendeleo,” alisema DC Taka.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Tarafa ya Ngorongoro Edward Maura akizungumza niaba ya wananchi alishauri maeneo yenye vivutio vipya kuhakikisha yanaanza kutangazwa kwa nguvu ili kuvutia watalii zaidi.

“Tuna maeneo kama Mlima Loormalisin uliopo Kijiji cha Nainokanoka huu ni watatu kwa urefu hapa nchini, lakini bado haujatangazwa ili kuwavutia zaidi watalii,” alisema Maura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles