24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Miaka mitatu ya urais wa JPM, Uchumi wakua kwa asilimia 7.5 

                                     Bethsheba Wambura, Dar es Salaam

Ikiwa imepita miaka mitatu tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amefanya mambo kadhaa ili kuhakikisha nchi inafikia malengo yake ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 5, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alipokuwa akitoa taarifa ya mambo muhimu yaliyotekelezwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli tangu alipoanza kutawala hadi sasa.

Akisoma taarifa hiyo iliyotengwa katika maeneo 10, amesema ipo miradi mingi iliyotekelezwa na Serikali ndani ya miaka mitatu ya Rais Magufuli.

Amesema katika miaka yake mitatu ya kuwa madarakani Rais Magufuli amesimamia misingi ya uchumi pamoja na changamoto kadhaa zinanazoikumba uchumi wa dunia na hata ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Katika mwaka 2017/18 uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 7.1 na kuifanya kuwa ya kwanza kwa Afrika Mashariki lakini katika takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB) ni ya Tisa kati ya nchi 10 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi.

“Huwezi kuongelea kukua kwa uchumi bila ya kuangalia moja ya vijenzi muhimu vya kuashiria ukuaji wa uchumi, katika mambo ambayo Rais amefanya ni kuhhakikisha mapato ya Serikali yanakua, ameziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza ukusanyaji wa kodi ya Serikali kutoka wastani wa Sh Billioni 850 hadi Sh Trilioni 1.3 kwa mwezi,” amesema.

Akiyataja mashirika ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na kuonekana kuwa ni mzigo kwa maendeleo ya Taifa lakini ndani ya miaka mitatu ya ufuatiliaji wake Rais Magufuli ameweza kuyafufua ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Reli (TRC), Mamlaka ya maji safi na maji taka Dar es Salaam (DAWASA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).

“Rais Magufuli alipoingia katika madaraka alisema atahakikisha adhma ya tangu wakati wa baba wa taifa ya kujenga nchi ya viwanda ambapo ndani ya miaka mitatu jumla ya viwanda 3306 vimeandikishwa, vinaendelea kujengwa na baadhi vimekamilika na vinatoa bidhaa mbalimbali, kati ya hivyo 251 ni vikubwa na 173 ni vya kati.

“Mchango wa sekta ya viwanda pekee katika pato la Taifa umekua kutoka asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi asilimia 5.5 mwaka 2017 na ukuaji wake ulikua kutoka asilimia 6.5 mwaka 20115 hadi asilimia 7.1 mwaka 2017/18,”  amesema Dk Abbasi.

Msemaji huyo amesema katika kuhakikisha anapambana na rushwa na ufisadi kwa pamoja Rais Magufuli alijenga mahakama ya mafisadi (makosa ya uhujumu uchumi) ambayo ilianza kazi rasmi Julai 2017 na mpaka sasa kesi 41 zilifunguliwa na kuna maombi ya dhamana 346 yamewasilishwa katika mahakama hii kati ya 2017 na 2018.

Amesema Rais Magufuli pia ametekeleza na anajiandaa kutekeleza mingine miradi mikubwa ambayo inatajiwa kuleta mageuzi ya ajira na maendeleo ya nchi ambapo baada ya kuleta ndege nne pia serikali ina mpango wa kuleta ndege zingine mbili aina ya airbus zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 130 ifikapo Desemba mwaka huu na Oktoba 2019 italeta Dream Liner nyingine.

Dk Abbasi ameitaja miradi mingine iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ni kukamilika kwa daraja la juu la kwanza nchini (Fly Overs), Reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, mradi mkubwa wa umeme wa maji (Stiglers’ Gorge) na kuondoa kero ya usafiri wa majini kwa kununua meli mpya mbili za mizigo katika ziwa Nyasa za Mv Ruvuma pamoja na Mv Njombe.

Amesema pamoja na hayo lakini Rais Magufuli amewekeza katika miradi mingine ambayo imewekeza moja kwa moja katika maisha ya watu ambayo ni Afya, Elimu na Nishati.

“Katika nishati tumepunguza kero za umeme kwa kuwekeza katika uzalishaji wa umeme wa gesi Miradi ya Kinyerezi 1 (megawati 185) na Kinyerezi 2 (megawati 240) inaendelea kukamilika. Katika afya tumejenga vituo vya afya, kuleta mashine za kisasa za kupimia kama CT-Scan, MRI na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati.

“Serikali pia inaendeleza jitihada za kuhakikisha maji yanapatikana katika miji na vijiji vyote nchini na katika sekta ya elimu tumehakikisha Watanzania wana uwezo wa kupata elimu ya msingi hadi sekondari bure na kumaliza migomo katika vyuo vikuu kwa kutoa mikopo kwa wakati,” amesema.

Amesema kuna wakati Rais alifanya maamuzi maagumu yaliyobezwa na watu wengi lakini yameleta manufaa kwa taifa kwa mfano wakati alipoamua kujenga ukuta katika mgodi wa Tanzanite Mirerani. Serikali imekusanya Sh. Milioni 788.5 ambayo ni sawa na asilimia 52 ya lengo la kukusanya Sh Billioni 1.5 kwa mwaka kutoka kwa wachimbaji wadogo.

“Rais asingeweza kufanya yote haya bila kuwepo kwa amani hivyo amejitahidi kudumisha amani pamoja na na matukio ya hapa na pale kama tukio la Kibiti lakini amehakikisha nchi inasimama katika amani na utulivu,

“Lakini pia anaenzi misingi ya Taifa kwa sababu nchi ilipopata uhuru toka kwa mkoloni ndio maana leo Watanzania tupo huru kuamua mambo yetu na hata miradi aliyoanzisha kwa kutumia fedha za ndani nini utekelezaji wa adhma hiyo,” amesema.

Aidha Dk Abbasi amewaasa Watanzania kuendeleza utamaduni wa kulipa kodi ili fedha hizo zikatumike kukamilisha miradi ya maendeleo muhimu kwa taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles