28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

MIAKA 25 BAADA YA BEIJING Bado kuna vikwazo usawa wa kijinsia

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

USAWA wa kijinsia umekuwa wimbo unaoimbwa karibu duniani kote, shinikizo kubwa likiwa ni juu ya upatikanaji sawa wa rasilimali na fursa bila kujali jinsia.

Hii ni kutokana na kundi kubwa la wanawake kuwa nyuma katika masuala mbalimbali kulikosababishwa na mila, desturi na tamaduni ambazo zilimbagua kwa kumuona hastahili kupata fursa husika.

Jitihada kubwa zimefanyika kubadili mtazamo wa jamii juu ya kundi hilo (wanawake) kuliwezesha liweze kunufaika katika kila jambo kama ambavyo inafanyika kwa wanaume.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995, ni mojawapo ya jitihada zilizofanyika kufikisha ujumbe duniani kote juu ya masuala mbalimbali ya haki za wanawake hasa la usawa wa kijinsia.

Miaka 25 sasa baada ya kufanyika kwa mkutano huo, yapo mambo ambayo mataifa mbalimbali yanaweza kusimama kifua mbele na kujipongeza kwamba yametekeleza maadhimio yaliyotolewa katika mkutano huo.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio yaliyopatikana suala la usawa wa kijinsia limeendelea kukabiliwa na changamoto na kusababisha utekelezaji wa azimio hilo kukumbwa na mikwamo hali inayozidi kuwaweka wanawake katika wakati mgumu.

Ndiyo maana kwa miaka kadhaa sasa Kaulimbiu za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zimekuwa zikishabihiana na suala zima la usawa wa kijinsia kama hatua ya kuzidi kupaza sauti ili dunia itekeleze kwa vitendo dhana hiyo.

Tanzania ambayo inaungana na mataifa mengine katika kumbukumbu hiyo, mwaka huu inaadhimisha Siku ya Wanawake kwa kaulimbiu isemayo: ‘Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye.’

Kwamba, inaendelea kuhimiza dhana ya usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha wanawake wanatambuliwa, kuheshimiwa, kulindwa na kunufaika na fursa mbalimbali bila kubaguliwa.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, Tanzania inatafakari miaka 25 ya mkutano wa Beijing na kujipima wapi iliko na nini kimesababisha isifike pale ilipotaka.

UTEKELEZAJI MAAZIMIO

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu, anasema mambo mengi yamefanyika yakiwamo kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia mifuko ya uwezeshwaji kiuchumi.

Dk. Jingu anasema kwa kipindi cha miaka minne, zaidi ya Sh bilioni 39 zimetolewa kwa wanawake zaidi ya 800,000 kupitia asilimia 10 ya fedha za ndani za halmashauri na Sh bilioni 2 zimetolewa kwa zaidi ya wanawake 3,000 kupitia dirisha la wanawake la Benki ya Posta Tanzania Agosti 2018 hadi Machi 2019.

“Umiliki wa ardhi umeongezeka kwa wanawake kutoka asilimia sita mwaka 2014 hadi 16 mwaka 2017, pamoja na ushiriki wa wanawake katika maonyesho ya biashara ya kimataifa kutoka 1,183 mwaka 2017 hadi 13,016 Machi mwaka 2019,” anasema Dk. Jingu.

Suala lingine linalotekelezwa ni maboresho ya Sera ya Wanawake na Jinsia ambayo inafanyiwa mapitio hivi sasa kuwezesha iendane na wakati.

Hivi sasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea na mchakato wa kukusanya maoni kwa wadau kutoka Kanda saba za Tanzania Bara ili kuwezesha maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000.

Hatua hiyo inatoa fursa kwa wadau kuibua changamoto, upungufu uliopo na kuimarisha uzingatiaji wa mahitaji ya wanawake na wanaume ili kutoa fursa sawa ya upatikanaji haki na usawa kwa watu wote.

Mshauri Mwelekezi wa Mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia, Profesa Linda Mhando, anasema sera iliyopo ilikuwa na mapendekezo 20 lakini katika mchakato unaoendelea hivi sasa tayari kuna maeneo 24 yaliyopendekezwa.

Anayataja maeneo hayo kuwa ni jinsia na maendeleo vijini/mjini, jinsia na haki za kumiliki ardhi, jinsia na matumizi ya maji na mazingira, haki za mtoto wa kike, jinsia na ulemavu, ukatili wa kijinsia, jinsia na elimu na mafunzo na jinsia, sayansi, teknolojia na uvumbuzi.

Mshauri Mwelekezi wa Mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia, Profesa Linda Mhando, akizungumza katika kikao kazi cha kutoa maoni na tathimini ya sera hiyo.

Maeneo mengine ni jinsia na hifadhi ya jamii, jinsia, afya ya uzazi na Ukimwi, jinsia, uongozi na maamuzi, jinsia, ajira na kazi, jinsia, sheria na haki za binadamu, jinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi, jinsia na ujumuishwaji wa kifedha, jinsia, mazingira na mabadiliko tabianchi na jinsia na matumizi ya nishati.

Pia yamo jinsia na miundombinu, takwimu za jinsia, jinsia na sekta ya madini, jinsia, vyombo vya habari na mawasiliano, jinsia, mila/desturi potofu, jinsia na ufugaji na jinsia na ufadhili wa kifedha.

“Sera ina takribani miaka 20 lakini kuna changamoto, Tanzania inakwenda kwenye uchumi wa kati lazima mwanamke ashiriki kikamilifu kuleta Pato la Taifa na apewe stahiki zote anazopaswa,” anasema Profesa Linda.

Profesa Linda anasema uelewa kuhusu dhana ya jinsia bado ni changamoto hasa katika maeneo ya vijijini hivyo, juhudi kubwa zinahitajika kuhakikisha inaeleweka miongoni mwa jamii.

“Katika karne ya 21 lazima tuzungumzie dhana ya jinsia, kwanini tunasema ‘gender’, kwanini si wanawake…wanaume wakihusishwa kwenye gurudumu la maendeleo itarahisisha kuliko kuwaacha nyuma,” anasema Profesa Linda.

MKWAMO

Licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto katika maeneo mbalimbali zinazorudisha nyuma juhudi za maendeleo ya wanawake.

Wanawake wengi wanakumbwa na ubaguzi na ukatili, pamoja na idadi ya wanawake katika ngazi mbalimbali kuongezeka kwa kasi kubwa, bado hawapandi au kushika vyeo vya kutoa uamuzi.

Kuna mtazamo kuwa wanawake wanatumia muda mwingi ikilinganishwa na wanaume katika kutunza familia.

Pia baadhi ya waajiri wanadhani kuwa kazi nyingine haziwezi kufanywa na wanawake hivyo kuwapa kazi nyepesi.

Ripoti ya mwaka 2018 ya Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO), kuhusu mtazamo wa wanawake kweye sekta ya ajira inaonyesha pengo la usawa wa kijinsia halijapungua kwa miaka 20.

Kulingana na ripoti hiyo, katika kipindi cha miaka 27 pengo la usawa wa kijinsia limepungua kwa asilimia mbili tu huku idadi ya wanawake na wanaume walioajiriwa ikipungua duniani kote. 

Ripoti hiyo imeainisha changamoto zinazoathiri usawa wa kijinsia kuwa ni pamoja na malipo duni na utofauti wa malipo kwa misingi ya jinsia, ukatili na unyanyasaji katika maeneo ya kazi, teknolojia ambazo zinatokana na mabadiliko ya kidijitali zinazoathiri fursa na viwango vya kazi wanazozifanya wanawake na uwakishi duni wa wanawake katika vyama vya wafanyakazi.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Espinosa, anasema hakuna taifa lolote duniani ambalo limefikia usawa kamilifu wa kijinsia na bado wanawake wanaendelea kukabiliwa na ubaguzi kwenye kanda zote duniani.

“Bado wanawake wako nyuma katika malengo 17 ya maendeleo endelevu (SDGs), ni asilimia 42 ya nchi zote duniani ambako wanawake wana haki sawa ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa wanaume ilhali ni asilimia 60 ya nchi zinazowapatia wanawake fursa sawa na wanaume kwenye suala la huduma za kifedha,” anasema Maria.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, anasema ingawa mazingira yamebadilika tangu wakati huo, lakini kumekuwapo wimbi kubwa linaloshambulia haki msingi za wanawake katika medani mbalimbali za maisha.

“Haki msingi za wanawake zilizovaliwa njuga miaka 25 iliyopita zinaendelea kudorora; usawa wa kijinsia bado unayo safari ndefu kutokana na ubaguzi na mfumo dume unaoendelea kutawala sehemu mbalimbali za dunia,” anasema Michelle. 

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, anasema wanawake nchini ni zaidi ya asilimia 51 ya wananchi wote hivyo kundi hilo lina uwezo wa kufikia maamuzi yenye tija.

“Hatuwezi kusema tuna usawa wa kijinsia wakati bado hatujaweza kuchaguliwa na watu, kama isingekuwa kipengele cha viti maalumu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lingekuwa na wanawake asilimia sita tu, idadi ambayo ni ndogo.

“Asilimia 30 ya wabunge wa viti maalumu na wale wa kuteuliwa haina mantiki katika kuelekea usawa wa kijinsia hivyo, nawahimiza wanawake mjitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” anasema Anne.

SERIKALI

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema Serikali imetoa kipaumbele katika masuala ya kukuza usawa wa kijinsia kwa kuyaweka kuwa ni miongoni mwa ajenda muhimu za maendeleo za kitaifa na utekelezaji wake unagusa nyanja mbalimbali.

Hata hivyo, anasema taifa bado linakabiliwa na changamoto ya vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto huku vingi vikifanywa na ndugu na jamaa wa karibu.

Kwa mujibu wa Ummy, katika kipindi cha 2016 hadi 2018 wahanga wa ukatili wa kijinsia 116,899 walitambuliwa kupitia madawati 420 ya jinsia na watoto yaliyopo katika vituo mbalimbali vya polisi nchini na kati yao 78,400 ni watu wazima na 38,499 ni watoto.

“Inakuwaje mtoto analawitiwa mara ya kwanza, ya pili, ya tatu…mama na baba mko nyumbani je, tunakosea wapi? Napata kesi nyingi mtu anakuja mtoto ameshaharibiwa.

“Wengine walipendekeza kule bungeni tuwaasi wanaume wanaofanya vitendo hivi, kuasiwa haitatusaidia, miaka 30 jela bado ni adhabu kubwa lakini watu hawaachi. Ni jukumu letu kwa pamoja kuzuia vitendo vya ulawiti na ubakaji hivyo kila mmoja atimize wajibu wake,” anasema Ummy.

Waziri Ummy anasema pia madawati ya jinsia yameongeza mwamko wa wananchi katika kujiamini na kutoa taarifa za ukatili pale unapotokea kwenye maeneo yao.

Anasema vituo vya mkono kwa mkono vya kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia vimeongezeka kutoka 10 mwaka 2017 na kufikia 13 mwaka 2019.

“Vituo hivi vinawezesha utoaji huduma rafiki na za haraka kwa waathirika wa vitendo vya ukatili na vinahusisha wataalamu mbalimbali wakiwamo Jeshi la Polisi, ustawi wa jamii, wanasheria na madaktari,” anasema.

Anasema pia watoto 6,927 wametambuliwa kupitia huduma ya simu bila malipo yaani namba 116 kwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles