28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Mhagama akemea vitendo vya kukamata wawekezaji kabla ya uchunguzi wa kina

Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama, amekemea vitendo vya kukamata wawekezaji na kuwaweka ndani bila kufanyika uchunguzi wa kina akisema vinarudisha nyuma juhudi za kuwaleta nchini ama za kukuza wale wa ndani.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akifungua semina ya wakuu wa  vyombo  vya ulinzi na usalama,  iliyowashirikisha, makamanda wa polisi mikoa, wakuu wa upelelezi mikoa na watendaji wa  taasisi na wizara ya madini lengo likiwa kujadili mbinu za kulinda rasilimali za madini.

Alivitaja baadhi ya vitendo vinavyoweza kurudisha nyuma ukuaji wa sekta ya madini kwamba ni pamoja na kuwakamata wawekezaji wa ndani na wa nje na kuwafungulia mashtaka kabla ya uchunguzi kukamilika au kufanya maamuzi ya kusimamisha shughuli za madini.

“Ukamataji holela na kusimamisha shughuli za uwekezaji, husababisha kuzorotesha juhudi iliyofanyika ya kuwaleta au kuwakuza wawekezaji, shughuli za uwekezaji kwenye madini zinahitaji uwekezaji mkubwa na muda wa kutosha kujiridhisha kuona kama mradi husika unaweza kuwa na tija kwa pande zote.

“Nitoe rai, mnapofanya maamuzi yanayohusu ulinzi na usalama kwenye shughuli za madini muwe mmejiridhisha vya kutosha na vyanzo vya habari, pia kupata taarifa au ufafanuzi kutoka kwa mamlaka zinazohusika kabla ya kuchukua hatua,” alisisitiza.

ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuangalia kama kuna tija kwa baadhi ya migodi kulindwa na kampuni za ulinzi kutoka nje ya nchi.

Jenista alisema ulinzi na usalama ni nyenzo muhimu katika kuwezesha sekta ya madini inuwanufaishe Watanzania.

“Sekta ya madini imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo utoroshwaji wa madini kwenda nchi za nje, ukwepaji wa kodi na mambo ambayo ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu zilizopo,” alisema.

Alisema uthubutu uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli, kuleta mageuzi katika sekta ya madini kwa kuangaliwa upya Sheria ya Madini ya mwaka 2010, umewezesha Watanzania na wawekezaji kunufaika kwa usawa.

Naye, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, alisema mwelekeo na malengo ya wizara hiyo ni kuhakikisha sekta ya madini inaongeza mchango wake kwenye uchumi wa nchi.

Alisema wanatarajia ifikapo mwaka 2025, sekta ya madini ichangie zaidi ya asilimia 10 kwenye pato la taifa.

Biteko alisema baada ya marekebisho yaliyofanyika mwaka juzi kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini, mwaka wa fedha 2018/19 mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa (GDP) ulikua kwa asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 4.8 kwa Mwaka 2017/18.

Pia, alisema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana kasi ya ukuaji wa sekta ya madini ilikuwa kwa asilimia 13.7 ambapo ilishika nafasi ya pili kiukuwaji ikitanguliwa na sekta ya ujenzi.

“Katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara imeweza kukusanya Sh. bilioni 242 sawa na asilimia 103 ya lengo la nusu mwaka la kukusanya sh. bilioni 237.5,”alisema  Waziri Biteko.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya vyombo vya ulinzi na usalama, Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, Benedict Wakuryamba, alisema bila ulinzi na usalama kuimarika, hakuna jambo litakaloweza kufanyika kwa manufaa ya Watanzania.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles