25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MGOMO WA MABASI USIO NA KIKOMO WATANGAZWA

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Yaendayo Mikoani (Taboa), kimetangaza mgomo usio na kikomo kuanzia kesho, huku kikiwataka mawakala wanaotoa huduma za kukatisha tiketi kutofanya hivyo kuanzia leo.

Mgomo huo unalenga kupinga sheria  zilizotungwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ambazo zinatajwa kuwa na vifungu kandamizi vinavyoweza kutishia ustawi wa biashara ya mabasi nchini.

Pamoja na hatua hiyo, wamiliki hao pia wamewataka wabunge kutopitisha sheria hizo hatari katika Bunge linaloanza keshokutwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, katika Mkutano  Mkuu Maalumu wa chama hicho, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alisema  mgomo huo unalenga kuisisitiza Serikali na wabunge kwa ujumla kuhakikisha wanafuta baadhi ya vifungu vya sheria  ambazo zitawaumiza wamiliki na wasafiri.

 “Tunawaagiza mawakala kuacha kukatisha tiketi kuanzia kesho (leo), tunaomba radhi kwa wateja wetu, lakini jambo hili haliepukiki,” alisema Mrutu.

Alisema sheria zinazolalamikiwa ni pamoja na  Sheria ya Leseni na Usafirishaji sura ya  317 namba  11 (6), ambayo ina kipengele cha adhabu ya kutaifisha  magari kwa makosa ya binadamu .

 “Mfano hii sheria inayotoa adhabu ya kutaifisha gari (forfeiture of a motor vehicle) ifutwe, kwa sababu katika hali ya kawaida adhabu hiyo ni kubwa sana  ukilinganisha na thamani ya gari na makosa ambayo mengi katika sheria yanatajwa ni ya kibinadamu,” alisema Mrutu.

Alisema adhabu ya kutaifisha magari haitawajenga wafanyabiashara hao, bali itawarudisha nyuma kimaendeleo, kwakuwa wengi wao wanaiendesha kwa mikopo.

Alisema mapendekezo yaliyotolewa katika kifungu namba 35(1) yana lengo la kuongeza adhabu ya faini kutoka Sh 10,000 hadi kufikia Sh 2,00,000, huku kosa la mara ya pili likitozwa kutoka kiwango cha juu cha Sh 20,000  hadi Sh 5,00,000.

“Taboa tunaona mapendekezo haya yanalenga kutukomoa, kwa sababu adhabu hii ni kubwa sana, haina uwiano kutoka adhabu ya sasa na mpya inayopendekezwa,” alisema Mrutu.

Alibainisha kuwa, kwa hali halisi ya kipato katika biashara ya usafirishaji, adhabu hiyo haitatekelezeka, bali itawaingiza katika mgogoro na mamlaka husika kwa ujumla.

Aliongeza wasafirishaji wana tozo nyingi ambazo wanalipa kwa kila siku gari linapokuwa barabarani,   hivyo wahusika waone kuwa, wafanyabiashara hao wanaichangia Serikali vya kutosha na wasilazimishwe kuichangia kwa adhabu.

Alisema chama kinaona adhabu ya faini ibaki kama inavyosomeka katika sheria iliyopo, yaani kima cha chini kiwe Sh 10,000 na kiwango cha juu (kwa kosa la kujirudia) iwe Sh 20,000.

Aliongeza kuwa, eneo jingine ni marekebisho  ya kifungu cha 41 ambayo  yamelenga kupandisha faini kutoka Sh 20,000 na kufanya adhabu ya kifungo isiwe chini ya miaka miwili, ambayo wanaona ni kubwa.

“Tunaona marekebisho yasifanyike katika kifungu hiki kwa sababu adhabu ni kubwa sana na ni ngumu kutekelezeka, hiyo adhabu ibaki kama inavyosomeka katika sheria,” alisema Mrutu.

Akizungumzia Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini sura ya 413, Mrutu alisema katika marekebisho yatakayofanywa yataongeza vifungu vidogo vine, ambapo katika kifungu namba 40A(1), marekebisho yaliyopendekezwa yanaipa mamlaka haki ya kuamuru  mmiliki wa gari kulipa nusu ya fedha  kabla ya kumfikisha mahakamani.

“Kifungu kinaelekeza endapo mtuhumiwa atakuwa amekiri kosa kwa maandishi, kwamba mtu akisemekana ametenda kosa na kukamatwa na Sumatra mtu huyo akikiri kwa maandishi, basi Sumatra wanayo mamlaka ya kumwamuru alipe nusu ya fedha ambayo angeilipa kama angeshitakiwa na kutiwa hatiani,” alisema Mrutu.

Alisema Taboa hawaoni sababu ya mtu kukiri kosa kwa maandishi na kuamriwa kulipa nusu ya faini na baadaye afikishwe mahakamani.

“Maoni yetu katika hili, tunaona mtu akikiri kosa anapaswa aandikiwe kulipa faini ndani ya muda maalumu bila kumpa usumbufu zaidi,” alisema Mrutu.

Pamoja na hayo, Mrutu alisema msimamo wa chama hicho ni kwamba, wanaona mapendekezo ya sheria hizo yamelenga kuepuka amri ya Mahakama Kuu katika Rufaa Namba 14 ya mwaka 2014, iliyompa ushindi Nayaz Hassan Kan, mmiliki wa mabasi ya Super Najmunisa, ambapo Sumatra waliamuriwa wasitoze faini zaidi ya iliyoelekezwa katika sheria.

Akizungumzia mgomo huo, Mkurugenzi wa Sumatra, Johansen Kahatano, alisema hana taarifa, hivyo hawezi kutoa majibu mpaka atakapofuatilia na kupata ukweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles