22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

MAJALIWA AAGIZA WAFUGAJI WAKOROFI WASAKWE

Na Tobias Nsungwe,

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, kupiga kambi katika Kata ya Miono wilayani Bagamoyo ili kuwasaka wafugaji wanaodaiwa kuwapiga wakulima. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana, Majaliwa alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo ambao walisimamisha msafara wake wakati akienda kukagua miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyoko wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Akitoa kero za eneo hilo, Diwani wa Kata ya Miono, Juma Mpwimbwi, alisema kata hiyo inakabiliwa na tatizo la wakulima kupigwa na wafugaji na wakipelekwa kituo cha polisi hawachukuliwi hatua yoyote.

 “Wafugaji wanatupiga lakini wenzetu hawachukuliwi hatua na hata ukienda kushtaki polisi hawakai kwa sababu wanadai wao wana fedha,” alisema diwani huyo.

 Pia alisema mbali ya kero sugu ya maji, waliahidiwa barabara ya lami tangu miaka saba iliyopita lakini hadi sasa hawana hata kipande kidogo tu cha barabara hiyo.

Naye Shabani Mkwimbi ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, alisema kata hiyo ina kituo cha polisi na mahakama lakini utendaji kazi wa viongozi waliopo hapo unatia shaka.

 “Waziri Mkuu tunataka ukimaliza kuongea na sisi, uondoke na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Miono, Maro na msaidizi wake Rashidi pamoja na hakimu wa hapa, kwa sababu hawa watu habari yao ni nyingine. Mkulima akienda polisi au mahakamani hashindi kesi hata siku moja, lakini mfugaji akienda anashinda,” alisema huku akishangiliwa.

 “Hawa watu wanadai wana hela na wanafanya chochote wanachotaka na ndiyo maana hawalali polisi hata kama wameua mtu,” aliongeza.

 Akijibu kero zao, Waziri Mkuu aliwahakikishia wakazi hao kwamba Serikali iliyopo madarakani ni yao na hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko juu ya sheria.

Alisema suala la polisi wa kituo cha Miono litashughulikiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo ambaye alikuwepo katika msafara wake. “Tena Mkuu wa Mkoa yuko hapa na yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huu, atasimamia hilo.”

 Akifafanua kuhusu suala la wafugaji kuwapiga wakulima, Waziri Mkuu alisema msimamo wa Serikali ni kuwaona wakulima wanafanya kazi zao kwa uhuru na wafugaji nao wanafanya kazi zao kwa uhuru. “Hakuna mfugaji anayeruhusiwa kupeleka ng’ombe wake kwenye mashamba yenye chakula. Hili haliruhusiwi hata kidogo,” alisisitiza.

Aliwataka maofisa mifugo wa mkoa huo waende kwa wafugaji na kutambua mifugo waliyonayo na kama kuna maeneo wahakikishe wanapatiwa maeneo rasmi ili waweze kupatiwa matibabu kwa ajili ya mifugo yao.

 Aliwataka wafugaji wanaokata mabomba ya maji ya mradi wa maji wa Chalinze (Chaliwasa) ili kupata maji ya kunywesha mifugo yao, waache tabia hiyo mara moja na akaonya kuwa watakaokamatwa, wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles