29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mgombea Frelimo asaka mbinu za ushindi CCM

Philipe Jacinto Nyusi
Mgombea urais wa chama cha Frelimo cha Msumbiji, Philipe Jacinto Nyusi

Na Arodia Peter, Dar es Salaam

MGOMBEA urais wa chama cha Frelimo cha Msumbiji, Philipe Jacinto Nyusi, amesema ziara anayoifanya Tanzania ni maalumu kwa ajili ya kupata mawaidha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kilisaidia kuleta ukombozi wa taifa hilo kutoka kwa wakoloni wa Ureno.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Jijini Dar es Salaam juzi, Nyusi alisema safari ya ukombozi wa taifa la Msumbiji ilianzia Tanzania, hivyo Frelimo hakina budi kuendelea kupata ushauri mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Tanzania na CCM kwa ujumla wake.

Alisema ziara yake itakisaidia chama chake kupata mawazo na ushauri ili kikiingia madarakani kiweze kukabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwemo za miundombinu ya maji, barabara, afya na kilimo.

“Tumekuja Tanzania kutoa heshima kwa CCM, mwanzilishi wa taifa, viongozi wa serikali, hatuwezi kusahau kwamba safari ya ukombozi wa Mozambique (Msumbiji) ilianzia hapa.

“Mozambique inakabiliwa na changamoto za barabara, kilimo, afya, elimu na barabara, ziara hii itatusaidia kupata maarifa kutoka kwa wenzetu Tanzania,” alisema Nyusi.

Frelimo ni kati ya vyama sita vilivyopigania uhuru katika nchi zao ambavyo hadi sasa vipo madarakani.

Mbali na Msumbiji, vingine ni Tanzania (CCM), Afrika Kusini (ANC), Angola (MPLA), Zimbabwe (ZANU PF) na Angola (SWAPO).

Katika ziara hiyo ya siku tatu, mgombea huyo wa Frelimo jana alikutana na Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam na baadaye alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Viongozi wengine ambao walitarajia kukutana naye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

Mbali na hao, pia Nyusi atakwenda Zanzibar kukutana na Rais, Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na viongozi wengine wa chama na serikali.

Uchaguzi nchini Msumbiji unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, raia wanaoishi nje ya nchi wanaruhusiwa kupiga kura ya kuchagua rais. Vyama vilivyo katika ushindani na chama tawala cha Frelimo ni Renamo na MDM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles