26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maximo ampa wiki mbili kiungo Yanga

Marcio Maximo
Kocha wa Yanga, Marcio Maximo

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

KOCHA wa Yanga Mbrazil, Marcio Maximo, amempa wiki mbili za kufanya mazoezi kiungo Hamis Thabit, aliyetemwa wiki chache zilizopita kwenye kikosi hicho na baada ya hapo itajulikana kama anamrejesha kundini au la.

Thabit ameanza kujifua na Yanga jana akiwa na wachezaji wengine wa timu hiyo, wiki mbili zilizopita Yanga ilitangaza majina ya wachezaji 11 iliyowatema likiwemo jina la kiungo huyo.

Maximo alisikia taarifa za kutemwa kiungo huyo, ambapo baadaye alitoa maagizo kwa uongozi wa Yanga kumrejesha afanye mazoezi na wenzake kabla ya kuamua hatima yake ndani ya timu hiyo.

Kwenye mazoezi ya jana eneo la ulinzi, Maximo aliwapa mbinu mabeki wake jinsi ya kuokoa mipira mirefu ya juu, walionekana kuchemka katika zoezi la kuokoa mipira hiyo ya juu kwa kutumia kichwa.

Maximo ametimiza wiki moja na siku mbili toka aanze programu yake ya kuinoa timu hiyo, inayojiandaa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabeki waliokuwa wakinolewa kwenye eneo hilo ni Rajab Zahir, Saleh Abdallah waliokuwa mabeki wa kati, huku Mbuyu Twite na Juma Abdul wakiwa upande wa pembeni, walichemka baada ya kupiga vichwa vingi vilivyokuwa havina nguvu na mipira kudondokea karibu ya lango.

Kukosea kwa mabeki hao kulimlazimu Maximo kuanza kuwakazania kurudia mara kadhaa zoezi hilo ili wabadilike, jambo ambalo liliwafanya wachezaji hao kuanza kufanya vyema na baadaye kocha huyo kuendelea kuwapa mbinu nyingine za kuokoa mipira ya kasi inayopigwa kwenye usawa wa chini.

Kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo Mbrazil, Andrey Coutinho, kwa mara nyingine ameendelea kung’ara mazoezini  baada ya kufunga bonge la bao kwa kumpiga chenga ya maudhi kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ aliyekuwa akitaka kuudaka mpira uliookolewa vibaya na mabeki wake.

Aidha, kipa mwingine wa Yanga, Juma Kaseja, naye ameonekana kung’ara baada ya kuokoa michomo takribani mitano ya hatari iliyokuwa ikipigwa na viungo na washambuliaji wa timu hiyo, huku akiokoa michomo mingine ya kawaida.

Hivi karibuni wakati Maximo akitambulishwa kuinoa timu hiyo, alisema anataka kutengeneza kikosi kitakachotisha anga za kimataifa na kufikia kule walipo TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

“Nimekuja Yanga kuijenga si tu ndani ya uwanja kwa kushinda bali hata nje ya uwanja, nataka kuifanya iwe na ubora kama wa TP Mazembe, ambayo inasifika kimataifa, kikubwa naomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles