23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

MGOGORO WA ASKOFU MOKIWA, WENZAKE WAFIKA PABAYA

 Dk. Valentino Mokiwa
Dk. Valentino Mokiwa

Na FREDY AZZAH – Dar es Salaam

MGOGORO wa Kanisa la Anglikana nchini umefika pabaya.

Hali hiyo inatokana na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, aliyevuliwa wadhifa huo na Askofu Mkuu wa kanisa hilo Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya, kumtaja kwa jina Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi, kuwa ndiye kinara wa mgogoro huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk. Mokiwa ambaye alitaja viongozi watano wa kanisa hilo, akiwamo Askofu Dk. Chimeledya kuwa ndio chanzo cha migogoro ndani ya kanisa hilo, alisema wakati wote Profesa Kabudi amekuwa akiichochea migogoro hiyo huku akiwa amejificha nyuma ya taratibu za kanisa hilo.

“Kwa kawaida Askofu Mkuu wa Kanisa ana timu yake ya maofisa ambayo inamsaidia kutekeleza majukumu yake, lakini katika suala la kuniondoa madarakani, imemshauri vibaya.

“Kwenye jambo hili, wamemshauri vibaya na pia yote yaliyonukuliwa kwenye barua ya kuniondoa uaskofu yamekosewa.

“Kila taasisi kama ulivyo mwili una taasisi yake, kila taasisi ina sehemu ya kurekebisha mapungufu haya. Kwa hiyo, Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro kwa sababu Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam ndiye ninayezungumza hapa.

“Lakini mgogoro unaoitwa mgogoro, ni mgogoro wa kutengenezwa. Kama ninavyosema, pengine katika timu yake kuna watu wenye ‘interest’ (malengo) maalumu, maana wanao washauri waliobobea katika sheria.

“Lakini, ndio hao wanaompotosha akiwamo Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ndiye mshauri wa askofu wetu mkuu.

“Yule ni mwanasheria anayeitwa amebobea, lakini analiingiza kanisa kwenye mpasuko wakati kanisa letu limewahi kuandikwa na Serikali, kwamba linaongoza kwa migogoro.

“Nimesema anashauriwa na mtu tunayetaka kumheshimu na mtu tunayeamini kabisa anaheshimiwa na wengi.

“Pengine anaheshimiwa huko, lakini huku ndani ya kanisa anavuruga, ni mwanasheria aliyezalisha wanasheria wengi katika nchi hii, lakini asiyelitendea kanisa lake sawasawa.

“Kwa kuwa halisaidii kanisa kusimama sawasawa, kuliokoa kanisa na mivurugiko, anakuwa nyuma na haonekani mara zote kwa sababu anakuwa amejificha nyuma ya taratibu.

“Kwa ujumla migogoro mingi katika kanisa letu ni ya kutengeneza, na huu wa Dayosisi ya Dar es Salaam unatengenezwa pia ili kusiwe na maelewano baina ya waumini na askofu.

“Lengo lao ni kuona hapatawaliwi ili waweze kuingia na kushika hatamu za uongozi na hilo tunalijua, kwamba haliko Dar es Salaam tu bali pia katika dayosisi nyingine.

“Kuna viongozi wako Kanisa la Magomeni, wanakuza mgogoro huu kwa sababu mwanzo walikuwa viongozi kwenye Jimbo la Dar es Salaam na baadaye wakavuliwa madaraka kwa sababu ya utovu wa nidhamu, ikiwamo mambo ya fedha,” alisema Askofu Mokiwa.

Akizungumzia mkutano uliotumika kumvua madaraka, alisema haukufuata taratibu na hatatekeleza maagizo ya mkutano huo.

Akijibu swali juu ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye mkataba wa kanisa hilo na Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam (DCB), Askofu Mokiwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu linahusu taasisi nyeti.

 PROFESA KABUDI

Akizungumza na MTANZANIA juu ya tuhuma hizo, Profesa Kabudi alimshangaa Askofu Mokiwa kwa kumtaja kwenye mkutano ambao yeye hakuwapo.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Kabudi alisema anasubiri kuona kitakachoripotiwa na vyombo vya habari ili ajue hatua ya kuchukua.

“Kwanza kabisa mimi ni Msajili wa Kanisa la Angilikana Tanzania na ni msajili ambaye Katiba ya Kanisa na kanuni zake, zinatamka kazi za msajili ni kumshauri askofu mkuu mambo yote yanayohusu sheria.

“Sasa basi, mshauri ni mshauri, mimi ni msajili ila Askofu Chimeledya ni askofu wangu wa tatu. Yaani nimekuwa msajili wakati wa Askofu Mkuu Donald Mtetemela, nimekuwa mshauri, msajili wakati wa Askofu Mkuu, Valentino Mokiwa na sasa ni Mshauri wa Askofu Mkuu, Jacob Chimeledya.

“Kwa hiyo, Askofu Mokiwa asihamishe hoja kwa sababu yeye amekuwa askofu mkuu niliyekuwa nikimshauri na nilikuwa nikihudhuria vikao vya sinodi, Baraza la Halmashauri Kuu ya Kudumu ya Kanisa na nyumba ya maaskofu kama ikihitajiwa.

“Lakini pia askofu mkuu ni kuhani mkuu na moja ya sifa ya kuhani mkuu ni kutotoa siri za kikuhani nje. Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana hata yeye Mokiwa kuna mambo mengi ya kisheria nilikuwa nikimshauri. Yapo aliyoyakubali na yapo aliyoyakataa kwa sababu mengine yalihusu mchakato wa aina hii hii kama ulioko sasa.

“Kama ndivyo hivyo, iweje leo yeye kuhani amtuhumu msajili mwaminifu hadharani?

“Hapo amevunja kiapo cha ukuhani na amemkashifu Mkristo asiyekuwa na nafasi ya kujitetea mbele za watu wengine. Kwa hiyo, muulizeni katika hizo tuhuma 10 zinazomkabili, msajili anaingia wapi?

“Mimi siwezi kutoa siri za ushauri gani nampa askofu mkuu na maaskofu kama ambavyo sikutoa hizo siri wakati wa Askofu Mkuu Mtetemela na kwake yeye, na sitatoa nje ushauri ninaompa Askofu Chimeledya na mwingine atakayekuja.

“Hivyo basi, siwezi kuzungumzia nilimshauri nini alipokuwa askofu mkuu, yapi yalikuwa mabaya, yapi yalikuwa mazuri, yaliyokuwa mabaya aliyafanyaje na mazuri aliyafanyaje,” alisema Profesa Kabudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles