25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

JAHAZI LAZAMA, LAUA 12 LIKIELEKEA PEMBA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba

AMINA OMARI Na OSCAR ASSENGA – TANGA

ZAIDI ya watu 12 wamekufa maji na wengine 27 kujeruhiwa baada ya jahazi walilokuwa wakisafiria kuzama kwenye Kisiwa cha Jambe kilichopo Pwani ya Bahari ya Hindi jijini Tanga.

Jahazi hilo linalofanya safari zake kati ya Pemba na Tanga, lilizama baada ya kukumbwa na upepo mkali wakati likielekea kisiwani Pemba.

Akithibitisha tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alisema lilitokea saa 12:30 asubuhi katika eneo la Sahare Kasera, Kata ya Mnyanjani, Tarafa ya Ngamiani Kaskazini, likihusisha jahazi la MV Burudani lenye namba MV Z5512 maarufu kama Sayari.

Kamanda Wakulyamba alisema jahazi hilo lilikuwa likiendeshwa na nahodha aliyejulikana kwa jina la Badru Saidi ambaye pia alifariki dunia kwenye ajali hiyo.

Hadi sasa miili iliyopatikana ni ya wanaume watano na wanawake saba.

Kamanda Wakulyamba alisema mashuhuda wa ajali hiyo walisema chombo hicho kilikuwa kimebeba kati ya watu 30 na 40.

Hata hivyo, alisema wanawasiliana na Mamlaka ya Usimamizi wa Vyombo vya Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) ili kubaini idadi halisi ya abiria waliokuwa katika boti hiyo.

Aidha kamanda huyo alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya majini kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya uokoaji, ikiwamo mawasiliano ya uhakika kama rada ili kuwa na njia rahisi za mawasiliano wanapokumbana na dhoruba baharini.

“Lakini pia wananchi wanaosafiri majini watumie taasisi za uokoaji wanapokumbana na matukio ya kuzama baharini, kwani hiyo itakuwa ni njia rahisi kuweza kujiokoa,” alisema.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Dk. Goodluck Mbwilo alithibitisha kupokea maiti 12 na majeruhi 25.

Dk. Mbwilo alisema kati ya maiti hizo, sita ni watu wazima na sita ni watoto wadogo ambao bado hawajatambuliwa na wamehifadhiwa hospitalini hapo.

“Bado miili yote haijatambuliwa, tutaendelea kuihifadhi kwa utambuzi,” alisema Dk. Mbwilo.

Kuhusu majeruhi, alisema wapo 18 ambao ni watu wazima na watoto saba.

Naye Muuguzi wa zamu katika wodi ya wanawake, Judith Mzia, alisema kuwa wamepokea majeruhi wanawake 17 na watoto watatu, kati yao wawili wana hali mbaya.

“Majeruhi wote wanaendelea vizuri na matibabu na hadi kesho pengine wanaweza kuruhusiwa kurudi majumbani, isipokuwa watoto wawili ambao wapo chini ya ungalizi maalumu baada ya kuonekana hali zao si nzuri na kulazimika kuwawekea oksijeni,” alisema Mzia.

Baadhi ya majeruhi katika ajali hiyo ambao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo, walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali uliosababisha dhoruba na baadaye kuzama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles