26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Mganga Mkuu Pwani atahadharisha kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko

Na Gustafu Haule, Pwani

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk.Gunini Kamba, ametoa tahadhari kwa wananchi waliopo mkoani humu juu hatari ya kuwepo kwa magonjwa ya milipuko.

Aidha, kutokana na hali hiyo amewataka wananchi hao kuepukana na visababishi vya magonjwa ya milipuko hususan kipindupindu, kuhara na ugonjwa wa matumbo kwa kuzingatia kanuni za afya.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dk. Gunini Kamba akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kuhusu magonjwa ya milipuko. Picha na Gustafu Haule.

Dk. Kamba ametoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu namna ambavyo ofisi yake inavyopambana na magonjwa hayo.

Amesema kipindi hiki ni kibaya kwa kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la maembe na kwamba kama wananchi hawatakuwa makini ni wazi kuwa watakaribisha magonjwa hayo.

Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa ya kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafi wa afya na usafi wa mazingira wanayoishi kwa kuhakikisha kila wanachokula kinasafishwa na maji safi na salama.

Aidha, Dk. Kamba amesema ugonjwa wa kipindupindu unatokana na uchafu hivyo ni vyema wanapotaka kula maembe wahakikishe yanasafishwa vizuri ili kuondoa wadudu waenezao magonjwa hayo.

“Tupo kwenye msimu wa ongezeko la matunda hasa maembe na kipindi hiki ndicho ambacho watu wanakumbwa sana na magonjwa ya milipuko hivyo natoa tahadhari ya watu kuwa makini pale wanapotaka kula matunda,” anasema Dk.Kamba.

Amesema ofisi yake inaendelea na mikakati ya kupambana na magonjwa hayo na moja ya mikakati hiyo ni kutoa elimu kwa wananchi, wanafunzi na hata maeneo ya soko kazi ambayo inafanywa na maafisa afya.

Ameongeza kuwa kipindi cha ugonjwa wa corona wananchi walihamasika kutumia kanuni zote za usafi zilizoagizwa na serikali lakini baada ya corona kumalizika wananchi wamesahau kuendelea na kanuni hizo.

“Wananchi walipokuwa wanatumia kanuni za kunawa mikono mara kwa mara, kutumia vitakasa mikono ni njia ambazo zilikuwa zinasaidia kuzuia magonjwa mengine ya mlipuko ndio maana magonjwa hayo hayakuwepo,” amesema Dk. Kamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles