30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Mfumo mpya wakuomba ajira OATS kuondoa ‘manung’uniko’ nchini

*Ajira kuombwa kwa njia ya mtandao Bara na Zanzibar

*Kuepusha usumbufu, ubobevu kwenye kompyuta watajwa

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imesanifu na kujenga mfumo wa kufanya usaili kwa njia ya kielektroni – “Online Aptitude Test System” (OATS) ambao umekamilika kwa asilimia 98.

Kukamilika kwa mfumo huo kutatoa fursa kwa Watanzania wa pande zote Bara na Visiwani kuomba fursa za ajira huku jambo la msingi likiwa ni mhusika kukumbuka akaunti na neno la siri huku ufanisi katika kompyuta ikiwa ni nyenzo muhimu.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Aprili 15, jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Simbachawene amesema mfumo huo utawezesha wasailiwa kufanya usaili wa kuandika/mchujo kwa njia ya kidijitali katika eneo la karibu na mahali anapoishi, kutumia muda mfupi, kuepuka gharama za usafiri, malazi na changamoto za ajali.

Amesema kwa hatua za mwanzo, usaili huo utafanyika katika vituo maalumu katika taasisi za umma na binafsi.

“Vituo hivi ni pamoja na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), Vyuo Vikuu vya Umma na binafsi, baadhi ya vyuo vya kati vya umma na binafsi, vyuo vya ualimu na baadhi ya sekondari zenye miundombinu ya maabara ya kompyuta zilizounganishwa na huduma ya intaneti,” amesema Waziri Simbachawene.

Amesema ili kuepuka usumbufu watafuta fursa za ajira wote kutoka pande mbili za Muungano wanatakiwa kufahamu akaunti zao, neno la siri (nywila) na kuwa mahiri katika matumizi ya kompyuta.

Aidha, Waziri Simbachawene amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imekuwa ikifanya kazi na Tume ya Utumishi wa Umma Zanzibar.

Amesema Tume hiyo inayoratibu masuala ya ajira kwa watumishi wa umma ili kurahisisha zoezi la kutangaza nafasi za kazi na kuwafikia waombaji walio wengi kwa uharaka zaidi.

Amesema katika kuimarisha zaidi Muungano Wataalam wa rasilimaliwatu na hasa wanaojihusisha na masuala ya ajira kwa nyakati mbalimbali wamekuwa wakibadilishana uzoefu.

“Ushirikiano huu, umekuwa chachu ya kuendelea kudumisha Muungano wetu kwa kupata watumishi wenye sifa na weledi wa kutosha. Miongoni mwa taasisi ambazo watumishi wake wamepitia mchakato wa ajira unaoendeshwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni pamoja na Ofisi ya Rais.

“Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ofisi ya Waziri mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa,” amesema Waziri Simbachawene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles