22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Mchunguzi Mkuu Takukuru alivyonaswa kwa rushwa

Kulwa Mzee Na Leonard Mang’oha, Dar es salaam

MCHUNGUZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Cosmas Batanyika (44) amefikishwa Mahakamani kwa uhujumu Uchumi ikiwemo kushawishi rushwa ya zaidi ya Sh milioni 200, kupokea na kutakatisha fedha.

Ofisa huyo ambaye tayari amefukuzwa kazi tangu Julai 30, mwaka huu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Kevini Mhina.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi na Simon Wankyo ulimsomea mshtakiwa mashtaka kwa nyakati tofauti.

Katika shtaka la kwanza Wakili Kadushi alidai, Februari 9, mwaka huu eneo la Upanga, mshtakiwa akiwa mwajiriwa na Takukuru kama Mchunguzi Mkuu, aliomba rushwa ya Sh Milioni 200 kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham kwa lengo la kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi tuhuma zilizokuwa chini ya uchunguzi .

Alidai katika shtaka la pili, inadaiwa kuwa Februari 10, mwaka huu Viwanja vya Maonyesho ya Biashara, Sabasaba vilivyopo Temeke Jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Faizal Hasham kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi zinazomuhusu Gulamal.

“Mheshimiwa Hakimu katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa Februari 13, mwaka huu katika ofisi za Makao Makuu ya  Takukuru, mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru, alishawishi rushwa ya dola za Marekani 50,000 kutoka kwa Thangavelu Nallavan Vall kama kishawishi cha kuharibu ushahidi wa tuhuma za kukwepa kodi zilizokuwa zinamkabili,”alisai Kadushi.

Wakili  Wankyo alidai katika shtaka la nne  kuwa Februari 14,mwaka huu barabara  wa Haile Selasie karibu na Merry Brown, Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa alishawishi rushwa ya dola za Marekani 20,000 kutoka kwa Nallavan Vall kama kishawishi cha kuharibu ushahidi uliokuwa chini ya Mamlaka yake.

Wankyo alidai shtaka la tano, Februari 10, mwaka huu eneo la  Sabasaba mshtakiwa akiwa mwajiriwa kama Mchunguzi Mkuu wa Takukuru, alitakatisha Dola za Marekani 20,000 wakati akijua fedha hizo ni za la rushwa.

Katika shtaka la sita kutakatisha, ilidaiwa kuwa Februari 19,mwaka huu eneo la Village Super Market katika dula la kubadilishia fedha za kigeni la Electron, mshtakiwa alibadilisha sehemu ya Dola za Marekani 7,000 (alipata Sh Milioni 16.1)kati ya 20,000 huku akijua ni zao la rushwa.

Wankyo alidai katika shtaka la saba, ilidaiwa kuwa Februari 19, mwaka huu eneo la Chamazi Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alinunua ardhi eneo ambalo halijapimwa lenye thamani ya Sh Milioni 15.8 huku akijua fedha hizo ni za kutakatisha na ni zao la rushwa.

Hakimu Mhina alisema kesi inayomkabili mshtakiwa inasikilizwa Mahakama Kuu kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi hivyo, mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza na kufanya maamuzi ya maombi yoyote.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23, mwaka huu kwa kutajwa na amepelekwa mahabusu kwa kuwa shtaka la kutakatishaji fedha linalomkabili halina dhamana .

Awali jana saa 5:00 asubuhi kabla ya Mchunguzi huyo Mkuu kufikishwa mahakamani 

Takukuru iliitisha mkutano na waandishi wa habari ikieleza hatua ilizomchukulia kwa tuhuma ya kupokea rushwa kiasi cha Dola za Marekani 40,000 zaidi ya Sh milioni 91.959 kutoka kwa wafanyabiashara wawili.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi Takukuru, Diwani Athumani, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa  Batanyita aliomba rushwa hiyo kutoka kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa wakichunguzwa na Takukuru kwa makosa mbalimbali ikiwamo ukwepaji kodi.

Alisema mnamo Februari mwaka huu Batanyita alipewa jukumu la kufanya uchunguzi dhidi ya wafanyabisahara hao ambapo badala ya kufanya uchunguzi kama matakwa ya sheria yanavyomwelekeza yeye aliomba hongo.

“Batanyita aliomwomba mfanyabiashara wa kwanza hongo ya Sh milioni 200 na baada ya majadiliano walikubaliana kuwa mfanyabiashara huyo atoe kiasi cha Sh milioni 50 ili aweze kumsaidia kwenye tuhuma zinazomkabili,”. 

“Baada ya makubaliano mfanyabiashara huyo alimpatia Cosmas Batanyita kiasi cha Dola 20,000…hakuishia hapo, alimwomba pia mfanyabiashara wa pili hongo ya dola za Marekani 50,000 na baada ya majadiliano walikubaliana kuwa mfanyabiashara huyo atoe kiasi cha cha dola za Marekani 20,000, ili aweze kumsaidia kwenye tuhuma zinazomkabili,” alisema Athumani.

“Napenda kutamka mbele ya umma kwamba kwa muda wote nikiwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, sitakuwa tayari  kumvumilia mtumishi yeyote awe ni wa Takukuru au nje ya Takukuru ambaye atajihusisha na vitendo vya rushwa,” alisisitiza.

Alisema sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ambayo ndiyo inayoongoza mapambano dhidi ya rushwa haibagui na kwamba wanawasihi wananchi wasisite kuwapelekea taarifa sahihi za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili wachukuliwe hatua mara moja.

TANZANIA YAONGOZA MAPAMBANO YA RUSHWA

Wakati huo huo Kiongozi huyo wa Takukuru ameeleza juu ya ripoti inayoonyesha kuwa Tanzania imekuwa ya kwanza kati ya nchi 35 za Bara la Afrika katika kipengele cha juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa kwa mwaka 2019 ikifuatiwa na Lesotho na Siera Leone.

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya utafiti wa kupima hali ya rushwa unaofahamika kama Global Corruption Barometer Africa 2019 iliyotolewa na taasisi za kimataifa za Transparancey International na Afro Barometer hivi karibuni.

Diwani Athumani, alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo Tanzania imefanya vizuri kutika maeneo makuu mawili ikiwamo utendaji mzuri wa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Athumani alilitaja eneo jingine kuwa ni katika kukuza imani ya wananchi kwa Serikali yao kutokana na jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa nchini.

“Kumekuwa na ongezeko la ididi ya Watanzania wanaoamini kuwa Serikali inafanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa kutoka asilimia 37 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 71 mwaka 2019,”. 

“Utafiti huu pia unaonesha idadi ya wananchi wanaofikiri kuwa rushwa imeongezeka nchini Tanzania ni ndogo yaani asilimia 10 tu ikilinganishwa na idadi ya asilimia 66 iliyoona hivyo mwaka 2015.

“Utafiti huu pia umeonesha kuwa idadi kubwa ya Watanzania wana imani na Serikali yao juu ya mapambano dhidi ya rushwa na wanaona vitendo vya rushwa vimepungua. Imani hii imeongezeka kutoka asilimia 13 kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 72 kwa mwaka 2019” alisema Athumani.

Alisema moja ya sababu za mafanikio hayo ni utashi wa kisiasa wa Rais Dk. Magufuli katika kuongoza mapambano hayo na kwamba kutokana na utashi huo imani ya wananchi kwa Serikali imeongezeka. 

Pia alisema nidhamu ya watumishi wa Serikali imeimarika na matumizi mabovu ya fedha ndani ya Serikali yamedhibitiwa.

Aliongeza kuwa matokeo hayo yanazidi kuipa ari na nguvu mpya taasisi hiyo kama chombo ambacho kimepewa dhamana ya kuongoza mapambano dhidi ya rushwa.

“Ni wito wangu kwamba ili tuweze kuendelea kufanya vizuri katika mapambano haya dhidi ya rushwa pamoja na jitihada tunazozifanya Takukuru, kila Mtanzania anapaswa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli ambaye sifa zake katika kuongoza mapambano dhidi ya wala rushwa na mafisadi zinaonekana kusifika ndani na nje ya nchi,” alisema Athumani.

AONYA MATAPELI 

Mkurugenzi huyo wa Takukuru pia ameonya matapateli wanaojifanya maofisa wa Takukuru na baadhi ya vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini ambao hutumia mbinu mbalimbali ikiwamo kuwapigia simu wananchi wakiwataka wawapatie rushwa ili wasiwachukulie hatua kwa madai kuwa wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya rushwa ambayo yanachunguzwa na taasisi hiyo.

“Kupitia taarifa hii ninatoa onyo kali kwa wale wote wanaotaka kuchafua taswira chanya ya Takukuru pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kuacha mara moja tabia hiyo yenye lengo la kuondoa imani ya wananchi kwa Serikali yao,”  alisema Athumani.

Alisema taasisi hiyo haifanyi kazi zake vichochoroni na kwamba ofisa wake hufanya kazi akiwa na kitambulisho pamoja na nyaraka halisi zinazompa mamlaka ya kufanya uchunguzi wake nje ya ofisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles