30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu akerwa DED, mweka hazina kuparurana

Mwandishi wetu -Shinyanga

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geoffrey Mwangulumbi pamoja na Mwekahazina wa manispaa hiyo, Pascal Makoye  kwa kuwataka wabadilike na waache kugombana na badala yake watekeleze majukumu yao ipasavyo.

Pamoja na hali hiyo, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack azisimamishe kazi kampuni zote zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato katika manispaa hiyo kwa kuwa zimeshindwa kufanya kazi vizuri na zina madeni.

Hayo aliyasema jana alipozindua nyumba 10 za askari polisi katika Manispaa ya Shinyanga eneo la Kambarage, ambapo mradi huo umetokana na fedha zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli kiasi cha Sh milioni 225.

Alisema viongozi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji wa mapato na kutoa kazi hiyo kwa kampuni zisizokuwa na uwezo, ambapo kwa mwaka jana walikadiria kukusanya Sh milioni 800 na badala yake walikusanya Sh milioni 500.

Alisema manispaa hiyo haiwezi kusonga mbele kimaendeleo iwapo viongozi wake hawaelewani wanagombana kila siku. 

“Mkurugenzi na wenzako nawaonya kwa mara ya mwisho badilikeni na hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato,” alisema Majaliwa

Akizungumzia kuhusu nyumba za askari polisi, Waziri Mkuu alisema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuhakikisha askari wanaishi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kutekeleza vizuri majukumu yao.

 “Ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao lazima wawe na makazi mazuri,” alisema 

Hata hivyo alitoa wito kwa askari waliopewa funguo kwa ajili ya kuishi katika nyumba hizo wahakikishe wanazitunza vizuri na hata inapotokea wamehamishiwa kwenda katika vituo vingine, wale watakaohamia wakute nyumba hizo zikiwa katika mazingira mazuri.

Alisema ujenzi wa nyumba hizo ni endelevu, ambapo pia amezitaka idara mbalimbali za Serikali ziendelee na mchakato wa ujenzi wa nyumba zake kwani wakiwa na nyumba nyingi itasaidia kupunguza idadi kubwa ya askari wanaoishi uraiani.

Awali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao,  alisema awali fedha zilizotolewa zilikuwa zijenge nyumba tisa za vyumba viwili lakini kutokana na ubunifu waliweza kuboresha mradi huo kwa kuongeza nyumba moja sambamba na kuongeza chumba kimoja, hivyo kuufanya mradi huo kuwa na nyumba 10 zenye vyumba vitatu vya kulala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles