Mchungaji akamatwa na meno ya tembo

0
1027

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

JESHI la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia Mchungaji wa Kanisa la Anglikana wilayani Mpwapwa, Sekandi Mkombola (44) kwa tuhuma za kusafirisha vipande viwili vya meno ya tembo kwa kutumia pikipiki.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema tukio hilo lilitokea wiki iliyopita Kijiji cha Pwaga.

Kamanda Muroto alisema mchungaji huyo alikamatwa akiwa na meno mawili ya tembo yenye uzito wa kilogramu 15 sawa na tembo mmoja.

Alisema mchungaji huyo alikuwa akisafirisha kwa kutumia usafiri wa pikipiki aina ya Fekon yenye namba za usajili MC 772 AYK.

“Kijiji cha Pwaga, alikamatwa Sekandi Mkombola mkazi wa Mungui ambaye ni mchungaji akiwa na meno mawili ya tembo.

“Meno hayo yalikuwa na uzito wa kilogramu 15 sawa na tembo mmoja akiyasafirisha kwa pikipiki, uchunguzi bado unaendelea na washiriki wajisalimishe mara moja,” alisema Kamanda Muroto.

Katika tukio jingine, jeshi hilo linawashikilia wanaume wawili ambao majina yao yamehifadhiwa kwa tuhuma za kukutwa na vipande 16 vya meno ya tembo vilivyokatwa na kuwekwa katika madumu.

Kamanda Muroto alisema watuhumiwa walikamatwa stendi ya mabasi ya Nanenane mkoani Dodoma.

“Mbinu waliyotumia ni kuficha katika dumu la lita 20 lilokatwa juu na kutumbukizwa ndani ya mfuko wa shangazi kaja na juu yake kuweka mkaa,” alisema Kamanda Muroto.

Katika tukio jingine, Kamanda Muroto alisema jeshi hilo linawashikilia watu 10 kwa tuhuma za uvunjaji na wizi maeneo mbalimbali jijini hapa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here