Mbowe aanza kujitetea

0
1159

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe (58) ameanza kujitetea kwa kutoa mifano mizito ya watu waliouawa na kutekwa, huku akidai mazingira hayo yanakifanya chama chao kiamini hali katika nyanja ya usalama bado ni tatizo.

Mbowe anayeshtakiwa pamoja na viongozi wengine nane wa Chadema, alitoa utetezi huo jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akiongozwa na Wakili Peter Kibatala, alianza kujieleza maana ya jina lake Freeman kwamba ni mtu huru, alipewa na wazazi wake sababu alizaliwa wakati wa uhuru mwaka 1961 na alibatizwa siku ya uhuru Desemba 9, mwaka huo huo.

Alidai wazazi wake walikuwa wanasiasa, waasisi wa uhuru na marehemu baba yake alikuwa mwasisi wa Chama cha Tanu Kaskazini na mama yake alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho.

Maswali na majibu kati ya Wakili Kibatala na Mbowe yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Kibatala: Unasema nini kuhusu uzoefu wa shughuli za uchaguzi ngazi ya jimbo?

Mbowe: Nina uzoefu wa kutosha, nimeshiriki uchaguzi wote, mkubwa na mdogo kuanzia mwaka 1995.

Wakili Kibatala: Zaidi ya ubunge ulishiriki kugombea nafasi gani nyingine?

Mbowe: Mwaka 2005 niligombea urais ambapo ili ugombee lazima uwe na sifa za kugombea ubunge, elimu, uwezo wa kusoma na kuandika, uwe Mtanzania, uwe na akili timamu na usiwe na historia ya jinai.

Wakili Kibatala: Kina nani walikuwa katika kamati ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni?

Mbowe: Kamati wajumbe wake walikuwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Meya Boniface Jacob na Benson Kigaila.

Wakili Kibatala: Ngome yenu katika uchaguzi huo ilikuwa wapi?

Mbowe: Ngome yetu ilikuwa Magomeni, hatua chache kutoka ofisi za Manispaa ya Kinondoni ambapo ipo ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.

Wakili Kibatala: Kazi ya kusambaza mawakala hufanyika muda gani kwa uzoefu wako?

Mbowe: Usambazaji hufanyika usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi kwa sababu vituo vinafunguliwa saa 12 asubuhi.

Wakili Kibatala: Kinondoni mlikuwa na mawakala wangapi?

Mbowe: Wasiopungua 611.

Wakili Kibatala: Lengo la vyama vya upinzani ni nini?

Mbowe: Lengo kuwa na chaguzi huru na haki na kutafuta kuongoza dola ili kiweze kutekeleza sera na itikadi zake.

Wakili Kibatala: Kwanini mtake kuongoza dola wakati dola tayari inaongozwa?

Mbowe: Sisi Chadema tunaamini CCM imeshindwa kutekeleza ndoto ya Watanzania, kujenga maisha bora ya ustawi.

Wakili Kibatala: Imeshindwa maeneo gani?

Mbowe: Imeshindwa katika nyanja ya usalama, hali ya usalama bado ni tatizo, kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kuna matukio mbalimbali, haki za kiraia zimeshindwa kupatikana katika vyombo vya ulinzi kutoka Serikali ya CCM.

Wakili Kibatala: Mifano ipi?

Mbowe: Mfano mimi mwenyewe, nikishambuliwa na bomu, likaua wanawake watano katika mkutano uliofanyika Soweto Arusha, hakuna aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Wakili Kibatala: Mifano mingine, taja majina machache.

Mbowe: Daudi Mwangosi aliuawa na Polisi, mahakama ilithibitisha, Alphonce Mawazo aliuawa mchana kweupe, tulizuiwa kumuaga katika uwanja wa wazi hadi tukafika mahakamani, mahakama ikakubali maombi yetu.

Mfano mwingine, Ben Saanane alitekwa miaka miwili iliyopita, hadi leo hajapatikana, tumeomba waje wachunguzi wa nje maombi yetu yalikataliwa.

Mwingine Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, watu walipotaka kufanya maombi walizuiwa, waliotaka kuchangia damu walizuiwa, watu walijitokeza kuchangia matibabu, lakini Serikali na Bunge hawakuwa tayari.

MAWAKALA NA VITAMBULISHO

Akizungumzia mawakala kupewa vitambulisho, Mbowe alisema hadi asubuhi siku ya uchaguzi wa ubunge Kinondoni, mawakala wao walikuwa hawajapewa vitambulisho.

Alidai hali hiyo ilizua taharuki, mawakala wengi walijazana ngome na wachache walienda ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Mbowe alidai kutotoa vitambulisho chama kisingekuwa na mawakala katika uchaguzi na siku ya kufunga kampeni idadi kubwa ya mawakala walienda kwenye kampeni Mwananyamala.

Alidai mahali ulipokuwa mkutano na ngome ilipokuwa, ilikuwa ni sehemu ya kutembea kwa mguu.

Kesi iliahirishwa hadi leo kwa Mbowe kuendelea na utetezi.

Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa uchochezi, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya polisi iliyowataka watawanyike.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu – Bara, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here