MCHUJO MKALI MAUAJI KIBITI

0
456

WAANDISHI WETU, KILIMANJARO 

WAZIRI MKUU, Kassim majaliwa amesema Serikali imeongeza kasi katika kupambana na vitendo vya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia  katika Wilaya za Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani kwa kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema Serikali hivi sasa inafanya mchujo kubaini nani hasa wanashiriki katika mauaji hayo huku  ikichukua tahadhari  kuepuka kuingiza watu wasio husika.

Alikuwa akizungumza na waumini wa dini ya Kiislam katika Baraza la Idd El Fitr lililofanyika kitaifa katika Msikiti wa Riadha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro jana.

Majaliwa alisema kazi kubwa inayofanyika sasa ni ya kuchuja   kujua nani hasa anashiriki katika mauaji hayo.

Alisema Serikali inawashukuru baadhi ya Watanzania mbao wameanza kujitokeza kuwatambua na kubaini wauaji na kazi kubwa iliyopo sasa ni kufanya upelelezi na kuwakamata.

“Wananchi washirikiane na vyombo vya dola kuwabaini na kutoa taarifa sahihi juu ya wahusika ili sheria ichukue mkondo wake.

“Ninachoweza kuwaahidi ni kwamba wahalifu hawatapata mahala pa kukimbilia.

“Iwapo serikali itathibitisha ushiriki wa baadhi ya washukiwa wa mauaji hayo hatua kali za sheria  zitachukuliwa dhidi yao,”alisema Waziri Mkuu.

MADRASAT

Majaliwa pia alilitaka Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kuanza kuwatambua walimu wanaofundisha shule za Kiislamu (Madrasat) kuhusu elimu yao na msimamo wa vyuo walivyosomea.

“Ni vema BAKWATA muanze kuwatambua kwa kina ni kina nani hasa wanawafundisha watoto wetu elimu ya dini,

“Je, ni taratibu gani zinatumika kuwapata walimu?  Na je, wana elimu ya kutosha kuhusu dini ?

“Je, tunaifahamu misimamo ya vyuo walivyosomea?” alisema Waziri Mkuu na kuongeza:

“Bakwata mna wajibu wa kuyatafakari haya yote kwa kuhakikisha mnakomesha migogoro  kwa kuimarisha uongozi na kuwakutanisha waumini wote na kuzungumza nao mambo yanayowahusu”.

MUFTI ATAKA UCHUNGUZI KIBITI

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi bin Ally, ameitaka Serikali kuchunguza kwa makini mauaji   yanayoendelea mkoani Pwani kwa kuwa yanaliondolea taifa sifa na kutishia machafuko.

Pia ameitaka jamii kuacha imani potofu ya kuhusisha mauaji hayo aliyoyaita ya ugadi na imani ya dini ya Kiislamu kwa sababu  dini hiyo ni ya amani, mshikamano na inakemea maovu.

Akizungumza katika Baraza la Idd El Fitr jana, Mufti Zuberi alisema dini ya Kiislamu ni dini ya umoja na mshikamano na   inapohusishwa  na matukio ya ugaidi haipo tayari kulinyamazia suala hilo.

“Nataka jamii itambue kwamba dini ya Kiislamu  haifundishi ugaidi ni dini ya amani na suala hilo halikubaliki katika  dini yetu na wala si maadili ya Uislamu.

“Serikali ichukue hatua katika kubaini wahalifuwanaohusika na matukio ya mauaji yanayotokea Pwani.

“Baraza linaomba serikali iongeze umahiri   katika kushughulikia jambo hili linaloharibu sifa ya dini ya Kiislamu kutokana na baadhi ya wananchi kuamini kuwa Waislamu  tunahusika na mauji hayo,” alisema.

Mufti pia alisema kuwa waumini wa dini ya Kiislamu wanaungana na Serikali kupiga vita uuzaji, usambazaji na matumizi ya madawa ya kulevya ili kunusuru taifa.

“Umoja na mshikamano ndiyo jahazi pekee linaloweza kuleta maendeleo katika Taifa na kutokemeza madawa ya kulevya nchini  na kunusuru nguvu kazi ya Taifa.

“Baraza linatambua mchango wa Serikali ya awamu ya tano inayotoa kwenye taasisi za dini   na inavyopambana na ulinzi wa mali za Watanzania  kuweza kuwanufaisha wananchi wote,” alisema na kuongeza:

“Waislamu na watanzania wote kwa ujumla nawahusia juu ya umoja na mshikamno ambao ndio jahazi pekee linaloweza kutuvusha kwa maendeleo.

“Tuache magomvi tuliyo nayo na  mafarakano ambayo hayajulikani yanatoka wapi”.

Alisema imekuwapo   mifarakano ambayo imekuwa iiendelea kutokea kutokana na kuwapo  maslahi madogo ambayo hayana maana.

Alisema jambo hilo limekuwa likirudisha nyuma jitihada mbalimbali za maendeleo.

Mufti  aligusia mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii hususan kwa vijana na kusema kwamba ni jukumu la kila mzazi kusimamia malezi kwa watoto wake.

“Wenye jukumu la kusimamaia malezi ni sisi wenyewe hasa viongozi wa dini mchukue juhudi za makusudi kuhubiri kwa nguvu zote amani kutokana na kuwapo  viashiria vya uvunjifu wa amani,” alisema.

Sheikh wa Mkoa Arusha

Naye Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shabani bin Juma amewataka Waislamu kote nchini kuyaendeleza matendo mema yote yanayoamriwa katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, anaripoti ELIYA MBONEA.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa swala Idd el Fitri iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha jana na kuhudhuriwa na mamia ya waumini wa dini ya Kiislamu.

Akizungumzia umuhimu wa kumaliza mfungo wa Ramadhani, Sheikh Juma alisema Waislamu wanapaswa kuendelea ushirikiano kwa kusimamia mambo yote mema waliyokuwa wakiyafanya wakati wa mfungo.

“Niwaombe ndugu zangu Waislamu leo tunasherehekea Idd el Fitri baada ya kumaliza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, basi yale yote yaliyoamrishwa kwenye Mwezi Mtukufu tuyaendeleze katika maisha yetu ya kila siku,” alisema Sheikh Juma.

 MASHEIKH  UAMSHO

JUMUIYA ya Tàasisi za Kiislamu Tanzania imeitahadharisha serikali kwamba ili amani na utulivu viendelee kutawala nchini  lazima haki itendeke hasa kwa viongozi wa dini wakiwamo wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki) maarufu Uamsho ambao wanashtakiwa kwa tuhuma za ugaidi, anaripoti Patricia Kimelemeta.

Msemaji wa Jumuiya hiyo, Sheikh Rajab Katimba alisema   licha ya Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kufanya vizuri katika majukumu yake basi isishindwe kutenda haki kwa viongozi hao wa dini ambao wanaendelea kusota mahabusu kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuanza kusikilizwa mahakamani.

Alikuwa akizungumza   baada ya kumàlizika kwa swala ya Eid el Fitri katika Msikiti wa Mtambani   Dar es Salaam jana.

Sheikh Katimba alitoa kauli hiyo  ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kuitaka Serikali itende haki kwa kuwaachia huru masheikh hao wa Uamsho.

Alisema viongozi wa dini ni watu muhimu duniani na katika jamii inayowazunguka, hivyo wanaweza kutumiwa kama mabalozi wa amani ndani na nje ya nchi.

“Miongoni mwa watu wanaonyimwa haki ni viongozi wa dini wakiwamo wa Uamsho ambao wanasota rumande kwa tuhuma za ugaidi,” alisema.

Hata hivyo, alisema Jumuiya hiyo inaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kushughulikia mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwamo kusimamia miradi ya umma  na kupambana na ufisadi.

Sheikh Katimba pia alilaani mauaji yanayotokea Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani wa Pwani.

Aliitaka Serikali kuchunguza mauaji hayo  kujua chimbuko lake kuliko kutumia nguvu ambayo inawaumiza wengine wasio na hatia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here