24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge wa Chadema ahamishiwa Moi

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema), aliyepata ajali ya gari na kujeruhiwa akiwa na familia yake mkoani Dodoma amesafirishwa kwa ndege kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kunti amesafirishwa juzi usiku akitokea Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, akiwa pamoja na majeruhi wengine na kufikishwa moja kwa moja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam  jana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ilisema Kunti na wenzake walisafirishwa kwa ajili ya matibabu zaidi kutokana na hali zao baada ya kupata ajali hiyo.

“Hadi sasa, watu wawili wa familia yake wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na ajali hii iliyotokea eneo la Chemba, wakati Kunti na familia yake walipokuwa wakielekea Kondoa,” ilielezwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mbali ya mbunge huyo majeruhi wengine ni pamoja na dereva wa gari hilo, Stephen Massawe ambaye pia ni dereva wa Chadema Kanda ya Kati na watu wengine sita, wote ni wa familia yake.

“Tutaendelea kutoa taarifa kwa umma juu ya tukio hilo kadiri itakavyohitajika,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha alithibitisha kupokewa kwa majeruhi hao.

“Kweli walifikishwa hapa Muhimbili, wamelazwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI),” alisema Aligaesha.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alithibitisha kupokewa kwa majeruhi hao.

“Tulimpokea mbunge huyo na watoto watatu, walifikishwa saba usiku wa leo (juzi), mtoto mmoja amelazwa ICU amejeruhiwa kichwani.

“Mbunge na watoto wengine wamelazwa wodi binafsi 6B, wanaendelea kupatiwa matibabu, kulingana na madaktari wanaowahudumia hali zao zinaimarika,” alisema Mvungi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles