Neema Paul ,TUDARCoÂ
Mbunge wa jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema kuna ushirikiano mdogo jimboni kwake kwa baadhi ya taasisi za Serikali kama vile DAWASA,TANESCO na TARURA katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hususani barabara hivyo kusababisha uharibifu.
Bonnah ameyasema hayo jana wakati wa ziara yake ambapo ametembelea Kata ya Mnyamani na Kimanga, huku akiandika barua inayoelezea changamoto hiyo kwa kudai kuwa mawasiliano hafifu baina ya taasisi hizo tatu za serikali ndio sababu ya tatizo.
“Watu wa TARURA wanajenga barabara lakini wakimaliza tu kujenga wanakuja watu wa DAWASA nao wanachimba wanaweka mabomba ya maji sasa hii si sawa,” amesema.
Aidha ametoa wito kwa taasisi hizo kushirikiana wakati wa ufanyaji kazi ili kuepusha uharibifu wa rasilimali na pesa unaotokea kipindi zinapokinzana katika ufanyaji kazi.
“Unapotokea ujenzi wowote naomba watu wa DAWASA, TARURA na TANESCO ili washirikiane na kuepusha uharibifu hii itawezekana kama tu kutakua na mawasiliano imara,” ameeleza Bonnah.
Mbunge huyo amezungumzia pia changamoto ya uhaba wa maji iliyopo katika jimbo lake kwa muda mrefu kwa kusema kuwa serikali kupitia DAWASA inajitahidi kwa kila hali kuondoa na kubadilisha mabomba ya zamani na kuweka mapya ya sasa hivi.
“Tatizo hili la miundombinu mibovu ya maji wanalijua,wanalishughulikia na wapo mbioni kulimaliza hivyo naomba msiwe na mashaka yoyote,” amesema Bonnah.